SIKU tano kuanzia leo umma utashuhudia utekelezwaji wa agizo la uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa wanafunzi waliorejeshwa makwao baada ya kugoma. Huu ni utekelezaji wa masharti ya kurejea chuoni ifikapo Jumatatu Mei 14, 2007.
Kwamba pamoja na mambo mengine, yaani kila mwanafunzi kuandika barua na kueleza jinsi alivyoshiriki katika mgomo, pia wanatakiwa wawe wamekwisha kulipa asilimia 40 ya gharama za masomo katika elimu ya juu kama sera ya serikali inavyosema.
Kwa maneno mengine, sera ya uchangiaji wa elimu ya juu ambayo kwa zaidi ya miaka 15 imekuwa ikipingwa na kila kizazi cha wanafunzi kinachopita katika vyuo vya elimu ya juu nchini, sasa inatakiwa itekelezwe! Haya ndiyo maagizo ya ajabu kabisa ya uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hapana shaka una baraka zote za serikali.
Tujaribu kutafakari suala hili kwa kina. Kwa mara ya kwanza serikali ilitangaza sera ya kuchangia gharama za elimu ya juu mwanzoni mwa miaka ya 90. Uamuzi huo ulipingwa na umekuwa ukiendelea kupingwa kwa nguvu zote na wanafunzi, na bila shaka hata na wazazi.
Kwa nini wanafunzi wanapinga sera hii? Wanapinga sera hii kwa sababu moja kuu, kwamba taifa hili ni maskini na vivyo hivyo watu wake ni maskini kiasi kwamba hawawezi kushurutishwa kuchangia gharama za elimu ya juu kutoka mifukoni mwao.
Ni ukweli usiopingika kwamba kutokana na umaskini wa Watanzania ndiyo maana katika kutokujitambua kwa serikali ndiko kulikoisukuma kukubali kutekeleza sera za ajabu kama hizi za kuchangia elimu ya juu. Kwenye miaka ya mwisho ya 80 na mwanzoni mwa miaka ya 90 katika kutekeleza sera ya kuchangia gharama za elimu nchini, ilikuja kugundulika kwamba wazazi wengi waliacha kabisa kuwapeleka watoto wao shule. Yaani shule za msingi. Idadi ya wanafunzi wenye umri wa kwenda shule ambao walitakiwa wawe shule ilishuka sana hadi kufikia kwenye asilimia 60.
Hali hii haiwezi kusingiziwa sababu nyingine yoyote isipokuwa ni kutokana na wazazi kushindwa kumudu gharama za elimu ya msingi. Michango ilikuwa mingi. Kuanzia ada ya UPE, dawati, jengo na mlolongo mrefu wa michango ambayo kimsingi Watanzania wengi hawakuwa na uwezo wa kuimudu.
Baada ya kugundua kwamba sera hiyo ilikuwa mbovu na hailingani na hali wala uwezo wa Watanzania walio wengi, serikali yenyewe ikaamua kufuta ada kwa shule za msingi, na kweli wanafunzi wengi zaidi sasa wako shuleni kuliko hata ilivyokuwa baada ya serikali kuanzisha sera ya Universal Primary Education (UPE) mwaka 1975, elimu ikitolewa bure.
Kulingana na takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, idadi ya wanafunzi wa shule ya msingi walioko darasani leo hii ikilinganishwa na ilivyokuwa wakati wa UPE miaka ya sabini, kwa uwiano leo wanafunzi wengi zaidi wako shule.
Kwa maana hiyo gharama za kuchangia elimu nchini iwe kwa ngazi yoyote imekuwa na athari hasi kwa idadi ya wanafunzi wanaokuwapo shule. Hili likijulikana wazi, ndiyo maana chini ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) unatajwa kwamba umefanikiwa sana kwa sababu uliwaondolea Watanzani mzigo wa kuchangia gharama za elimu moja kwa moja kupita ada na michango mingine.
Huu ni ushahidi wa kisayansi. Kwamba kila suala la kuchangia gharama za elimu linapoibuliwa, madhara yake yamekuwa ni makubwa kwa elimu ya taifa hili.
Ndiyo maana tunasema Jumatatu ni siku muhimu kuhusu mustakabali wa elimu ya juu ya taifa hili. Ni siku muhimu kwa sababu watawala na warasimu wanataka iwe ndiyo siku ya kuamua ama kuwafukuza wale wanafunzi wa watoto maskini ambao hawezi kumudu kuchangia asilimia 40 ya gharama za elimu juu nchini.
Wanafunzi wanaoingia kwenye mkumbo huu ni wale waliolazimishwa kusaini mikataba ya kilaghai ya kuwashurutisha kukubali kuchangia kiwango hicho cha gharama.
Si uzushi kusema kwamba walilazimishwa kusaini mikataba hiyo ya kuchangia asilimia 40 kwa sababu katika hali ya kawaida, hawakuwa na mbadala. Wanafunzi hawa walisaini mikataba hiyo si kwa hiari yao ila walijua kwamba wanafanya hivyo ili kupata nafasi ya kuingia chuoni na baada ya hapo mapambano mapya yaanze kutafuta hizo asilimia 40 ambazo hazipo katika mikopo yao.
Kwa hiyo, wanafunzi hawa wana haki ya kukataa kulipa asilimia hii 40 kwa sababu kwanza walisaini mikataba wao wakiwa vulnarable katika makubaliano hayo, walifanya hivyo kujisetiri kwa wakati ule, kujipa nafasi kujipanga kupigania haki yao na ni katika kupigania haki yao ndiyo maana wamejikuta wakifukuzwa chuo kwa wiki kadhaa sasa.
Lakini jambo jingine la msingi ambalo serikali inashindwa kutambua pengine hata uongozi wa mwanazuoni kama Profesa Mukandala, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kushindwa kuliona ni kwamba inakuwaje kwa zaidi ya miaka 15 sasa wanafunzi wanapinga sera hii ya kuchangia elimu ya juu ? Ina maana wanafunzi wote waliopita hapo kuanzia waliomaliza mwaka 1991 hadi sasa wana akili pungufu kiasi cha kuichukia tu hii sera ya kuchangia gharama za elimu ya juu ? Kwa nini serikali haijiulizi swali la msingi, inakuwaje kwa miaka zaidi ya15 wanafunzi kwa vipindi tofauti, kwa intake tofauti wanapinga sera hii ?
Suala jingine ambalo serikali ama inashindwa kujua ni kwamba, inakuwaje imeamua kujitoa kutoa elimu ya juu ? Tunajua sasa hivi wanafunzi wa elimu ya juu wanapewa mikopo ambayo watalazimika kuja kuilipa mara watakapomaliza masomo yao wakishaanza kufanya kazi, kwa hiyo serikali imejitoa kwenye utoaji elimu ya juu.
Inakuwaje serikali inaelekeza nguvu nyingi za ajabu kwenye elimu ya msingi na sasa sekondari lakini inashindwa kuelekeza nguvu kwenye elimu ya juu ? Inataka kuwa na watu wa aina gani katika taifa hili ? Inataka kujenga kizazi cha wasindikizaji katika ushindani wa kila kitu katika dunia ya leo?
Nilipata kuandika huko nyuma kwamba kinachoiponza serikali yetu hadi kufikia hatua ya kushindwa kutatua mgogoro huu kwa miaka 15 sasa ni kuamua kuahirisha kufikiri.
Ukitaka kujua kwamba serikali imeahirisha kufikiri jaribu kuangalia mfano huu. Inatakiwa kwamba wanafunzi wote waliomaliza elimu ya juu waliopewa mkopo na serikali kuanzia mwaka 1994 wawe wanalipa mikopo hiyo. Serikali iseme ni wafanyakazi wangapi leo wanalipa mikopo hiyo, iseme wako wapi na iseme wanalipa kiasi gani kila mwezi.
Ninathubutu kusema Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu haijui nani alipewa nini na yuko wapi na atapatikana vipi ?
Kwa maana hiyo maelezo kwamba hakuna fedha za kuweza kuwalipia wanafunzi mikopo kwa asilimia 100 si sahihi. Si sahihi kwa sababu kwao (wizara) kujisumbua ni kero, kujibidiisha ili kutatua adha hii kwa miaka 15 ni sawa na kuwaogopa wanafunzi.
Mawazo haya ya kuvimbishiana misuli na kusahau mambo ya msingi ndiyo kwa hakika yamefikisha mfumo mzima wa elimu ya juu hapo ulipo leo.
Ninasema ni kuvimbishiana misuli kwa sababu wakati wote serikali inadhani na kuhisi tu kwamba wanafunzi ni wakorofi hawataki kulipa gharama ya asilimia 40 bila kujiuliza kwamba hivi anayelipa hii asilimia 40 ni nani hasa?
Wanafunzi hawana kipato, wanategemea wazazi au walezi wao kuwalipia. Hili linahitaji utaalamu gani kulijua? Je, hawa wazazi mishahara yao si inajulikana, sasa serikali inataka asilimia hii wakakope wapi?
Kinachoendelea hapa na kwa hakika kama hatutabadili mwelekeo wa fikra zetu kama taifa, migogoro ya elimu ya juu haiwezi kwisha kwa sababu wapo watu waliokaa katika meza za maamuzi lakini hawataki kutambua kwamba asilimia 40 haitekelezi.
Kuna fedha chungu nzima ambazo serikali ingeweza kukusanya kutoka kwa wanafunzi waliofaidika na mkopo, kwa bahati mbaya wanaokaa kwenye meza ya maamuzi hawataki kutafuta njia sahihi ya kupata fedha hizo ili kila mwanafunzi mwenye sifa za kusoma apewe mkopo kwa asilimia 100 na baadaye aje kulipa.
Tunasubiri mgogoro mwingine Jumatatu, kwa sababu tumeamua kuacha kufikiri na badala yake tunadhani misuli itatusaidia.