SERIKALI ina mpango wa kuikodisha nyumba aliyowahi kuitumia hayati Mwalimu Julius Nyerere wakati wa harakati za kudai uhuru, iliyopo Mtaa wa Ifunda, Magomeni, Dar es Salaam.
Hatua hiyo inafikiwa licha ya kuwa nyumba hiyo, ni moja ya maeneo ambayo yanahesabiwa kuwa ni makumbusho ya taifa.
Dhamira ya serikali inathibitishwa wazi wazi na ukarabati unaoendelea katika nyumba hiyo, ambayo inahifadhi sehemu muhimu ya historia ya nchi.
Kabla ya ukarabati huo, nyumba hiyo ilikuwa imechakaa na kuonekana kama gofu, huku kukiwa na juhudi finyu za kuutangaza umuhimu wake katika harakati za kudai uhuru.
Akizungumza na Tanzania Daima, Mhifadhi Mkuu wa nyumba hiyo, ambayo kwa sasa ni kituo kilicho chini ya Idara ya Mambo ya Kale, Samiu Mbegu, alisema baada ya Mwalimu Nyerere kuondoka Magomeni, aliikabidhi nyumba hiyo kwa viongozi wa Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania (JUWATA).
Aidha, Mbegu alithibitisha kuwa, kabla ya viongozi wa JUWATA kuishi humo, nyumba hiyo ilikuwa ikikaliwa na ndugu wa Mwalimu na baada ya kuondoka kwa JUWATA, nyumba hiyo ilikabidhiwa kwa Idara ya Mambo ya Kale.
Mbegu, aliendelea kueleza historia fupi ya nyumba hiyo na kusema, Mwalimu Nyerere, aliishi kwenye nyumba hiyo kwa miezi minane (kati ya 1958 na 1959) akiwa Rais wa TANU na kiongozi wa harakati za kuleta uhuru wa iliyokuwa Tanganyika.
Mwalimu alijenga nyumba hiyo kwa gharama ya sh 2,500 alizozipata baada ya kuacha kazi ya kufundisha katika Shule ya Sekondari ya Pugu, alikolipwa stahili zake.
“Hii nyumba ilijengwa kati ya mwaka 1957 na 1958 kwa fedha alizolipwa Mwalimu baada ya kuacha kazi Pugu Sekondari… humu aliishi kwa miezi minane, mwanzoni mwa 1959 Mwalimu alihamia Selander Bridge, wakati huo Mwalimu alikuwa na watoto wanne.
“Alipoondoka, Mwalimu aliacha nyumba hii kwa nduguze ambao hakuishi sana nao wakaondoka kwa vile ilishakabidhiwa kwa viongozi wa JUWATA,” alisema Mbegu.
Aliendelea kubainisha kuwa dhumuni la Serikali kuifanya nyumba ile kuwa kituo cha utalii na makumbusho ya Baba wa Taifa linakwamishwa na viongozi wa juu wa serikali kushindwa kuipa uangalizi mzuri.
Kadhalika, Mbegu alitupia lawama viongozi wa TANU na CCM kwa kushindwa kumuenzi muasisi huyo wa taifa na kuitelekeza nyumba hiyo, hali iliyosababisha kusahaulika kabisa.
“Nimekuwa mwangalizi wa nyumba hii chini ya Idara ya Mambo ya Kale kwa miaka 20 sasa, hakuna ndugu, jamaa wala kiongozi wa juu serikalini aliyewahi kutoa mchango katika nyumba hii kwa lolote.
“Kuna kipindi nikiwa na mkuu wangu wa kazi ambaye sasa ni marehemu, Mama Christine, tulienda kwa Joseph Butiku, yule wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, tukamweleza kuhusu nyumba hii, lakini hakuna alichotusaidia,” alisema Mbegu.
Kuhusu kukodisha nyumba hiyo, Mbegu alisema hilo linawezekana na iwapo atapatikana mwekezaji wa nje ama ndani, kwani hiyo ni moja ya vitega uchumi vya serikali vilivyopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mbegu alifafanua kuwa sheria inatoa ruhusa kwa wizara husika kumpa mwekezaji maeneo kama hayo, naye anaweza kufanya chochote, isipokuwa kuharibu ama kubadili mazingira ya eneo hilo.
“Hatuwezi kuuza maeneo ya kumbukumbu kama haya, kilichopo ni kumpa mtu kwa mkataba maalumu afanye anavyoweza, akiamua kuweka hoteli, baa au chochote ni juu yake,” alisema Mbegu.
Aidha, aliupongeza utawala wa Awamu ya Nne kwa kuonyesha kuijali nyumba hiyo kutokana na misaada mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwatafutia wafadhili kwa ajili ya ukarabati.
Alisema, Julai 11 mwaka 2001 mjane wa Mwalimu, Mama Maria Nyerere, alikwenda kuitazama nyumba hiyo, ambapo alikaa kwa saa mbili na kuondoka.