GHANA , jana iliendelea kulibeba Bara la Afrika katika michuano inayoendelea ya Kombe la Dunia, baada ya kuifumua Marekani kwa mabao 2-1 na kukata tiketi ya kucheza raundi ya pili ya michuano hiyo itakayoshirikisha timu 16.
Ikicheza soka ya uhakika mjini hapa, Ghana inayoshiriki kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia, lakini inayotema cheche za kutisha, iliandika bao la kwanza katika dakika ya 22, mfungaji akiwa Haminu Dramani. Kabla ya kufunga alimzidi kete mkongwe Claudio Reyna na kisha kuvuta kasi kidogo kabla ya kuachia kombora lililomshinda Kasey Keller.
Dakika 21 baadaye, baada ya kuhaha sana , Marekani ilifanikiwa kuilaghai ngome ngumu ya Ghana na kupachika bao la kusawazisha, mfungaji akiwa Clint Dempsey.
Kabla ya kufunga, DaMarcus Beasley ‘alimpora' mpira beki Derek Boatend na kumimina ‘majalo' iliyomkuta mfungaji ambaye bila kufanya ajizi aliachia shuti kali lililomshinda kipa Richard Kingston.
Lakini kuingia kwa bao hilo kuliiongezea nguvu zaidi Ghana iliyohaha kusaka bao. Na katika dakika ya 45, nahodha Stephen Appiah, aliifungia Ghana bao la pili kwa njia ya penalti iliyotolewa na mwamuzi Markus Merk wa Ujerumani, baada ya beki Mmarekani mwenye asili ya Nigeria , Onyewu Oguchi, kumfanyia madhambi Razak Pimpong.
Matokeo hayo yameivusha Ghana hadi raundi ya pili, baada ya kufikisha pointi sita zinazoiweka katika nafasi ya pili ya Kundi ‘E'.
Italia imeshika usukani wa kundi hilo kutokana na kuvuna pointi tisa. Katika mchezo ujao, Ghana itamkosa kiungo Michael Essien, mwenye kadi mbili za njano.
Ghana ‘ Brazil ya Afrika' iliyolala kwa 2-0 kwa Italia, lakini ikazindukia kwa Czech na kuilamba 2-0, sasa inasubiri kuchuana na mshindi wa Kundi ‘F' ambaye bila shaka atakuwa Brazil . Jana usiku ilitarajiwa kuumana na Japan huku Australia ikicheza na Croatia katika michezo itayoamua timu za kusonga mbele. Brazil ilishajihakikishia baada ya kufikisha pointi sita.
Katika mchezo mwingine, Czech inayoshika nafasi ya pili kwa ubora duniani, iliiaga michuano hiyo baada ya kufungwa mabao 2-0 na Italia.
Marco Materazzi aliyeingia badala ya Alessandro Nesta, alipachika bao katika dakika ya 26 baada ya kuruka juu na kuinasa kwa kichwa kona ya Francesco Totti. Filippo Inzaghi alipiga bao la pili katika dakika ya 86.
Kwa matokeo hayo, Italia imeshika usukani wa Kundi ‘E' baada ya kuzoa pointi zote tisa mbele ya Ghana , Marekani na jana Czech.
Itacheza hatua inayofuata na mshindi wa pili wa Kundi ‘F' lenye bingwa mtetezi Brazil , Japan , Croatia na Australia .
Michuano hiyo inaendelea leo kwa mechi nne za kufunga dimba hatua ya makundi. Tunisia itakipiga na Ukrane kuanzia saa 11:00 jioni muda ambao Saudi Arabia itakuwa inacheza na Hispania. Saa 4:00 usiku, Togo itaaga kwa Ufaransa na Uswisi itacheza na Korea Kusini. Ivory Coast na Angola pia kutoka Afrika, zimeiaga michuano hiyo