Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Manji anunua mechi
Manji anunua mechi
By Habari Tanzania | Published  05/6/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Deus Bugaywa, Mwanza


MASHABIKI wa soka nchini, leo wataandika historia ya pekee kwa kuishuhudia mechi ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho kati ya Yanga na Al-Merreikh ya Sudan bila kulipa kiingilio.

Kwa mujibu wa Crescentius Magori, Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), mechi hiyo itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa, haitakuwa na kiingilio.

Alisema, hiyo inatokana na gharama zote za mechi hiyo kulipwa na mfadhili wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji, hivyo kuwawezesha mashabiki wa soka kuiona mechi hiyo bure.

“Pengine mnaweza kushangaa ni kwa nini tumefanya hivi na nani kawezesha hili, ni kwamba mfadhili wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji ndiye ametoa kiasi cha sh mil 100 kama gharama za mechi hii,” alisema Magori.

Alisema, kutokana na hali hiyo, mashabiki wanatakiwa kufurika kwa wingi katika uwanja huo ili kuishangilia kwa nguvu Yanga ili iweze kushinda huku wakiweka mbele uzalendo.

“Tunawaomba mashabiki watakapoingia uwanjani waonyeshe uzalendo wao kwa kuishangilia Yanga kwa nguvu. Katika hili, isiwe katika kushangilia magoli tu bali kwa dakika zote 90,” alisema Magori.

Alisema, milango itafunguliwa saa 5 asubuhi na kufungwa saa 7:30 mchana na baada ya hapo, milango itafungwa na hakuna atakayeruhusiwa kuingia tena.

Alisema, kama uwanja utajaa mapema kabla ya muda huo, milango itafungwa na kama hautakuwa umejaa, haitafungwa hadi kufikia muda huo.

Mechi hiyo inatarajiwa kuanza saa 9 alasiri, na kwamba wale ambao watachelewa au kukosa nafasi ya kuingia muda uliopangwa, watalazimika kuishuhudia mechi hiyo kupitia kituo cha televisheni ya Star kitakachorusha matangazo ya moja kwa moja (live).

Magori alisema, wanatarajia mechi ya leo kufurika watu wengi kupita kiasi, hivyo ulinzi utakuwa ni wa hali ya juu, ambako polisi zaidi ya 200 wanatarajiwa kuhusika.

Aidha amewataka mashabiki kuwa watulivu na kuonyesha shukrani zao kwa Manji kwa kushangilia kwa amani bila vurugu.

Wakati hali ya mambo ikiwa hivyo, habari kutoka ndani ya Yanga, zinasema licha ya kukabiliwa na majeruhi, wachezaji walio fiti, wameapa kukata uteja wa kufungwa na Waarabu.

Kabla ya kununuliwa na Manji, viingilio vya mechi hiyo, vilikuwa ni sh 15,000 kwa Jukwaa Kuu na sh 3,000 Mzunguko.

Yanga inayokabiliwa na majeruhi kibao, inashuka kwenye Kirumba ikiwa ni siku 15 tangu ifungashwe virago katika uwanja huo na Esperance ya Tunisia katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni, Yanga iliangukia katika michuano ya Kombe la Shirikisho kwa kuthubutu kufika hatua ya tatu ya michuano ya Ligi ya Mabingwa.

Yanga iliyo chini ya Kocha, Mserbia, Sredejovic Milutin ‘Micho’, inawakabili Al-Merreikh bila nyota wake kadhaa kutokana na kuwa majeruhi na wengine kadi.

Kati ya hao ni beki wa kulia Shadrack Nsajigwa aliye nguzo muhimu kwa timu hiyo ambaye analazimika kuikosa mechi hiyo kwa kuwa na kadi mbili za njano.

Wengine watakaokosa mechi ya leo ni, sentahafu Hamis Yusuf, Gulla Joshua, Abdi Kassim, Credo Mwaipopo, Waziri Mahadhi na James Chilapondwa walio majeruhi.

Mazingira haya, ndiyo yanayompa wakati mgumu Micho kupanga kikosi chake, kwani hadi kufikia jana, wachezaji ambao walikuwa fiti ni 13 tu.

Ili Yanga ijiweke pazuri kuvuka kikwazo, inalazimika kupata ushindi mnono kabla ya marudiano wiki mbili zijazo nchini Sudan.

Aidha, Rais Jakaya Kikwete jana alituma salamu za kuiombea kheri Yanga kwa kusema, ushindi ni heshima kwa taifa.

“Nawatakia kheri katika mechi yenu ya Jumapili (leo), kushinda kwa Yanga itakuwa ni heshima kwa taifa,” alisema Kikwete baada ya ujumbe wa viongozi watatu wa klabu hiyo, kwenda Ikulu Ndogo ya jijini Mwanza, alikofikia akiwa katika ziara ya kiserikali.

Viongozi waliokwenda kumsalimu Kikwete, ni George Mpondela, Lucas Kisasa na Ahmed Mamba.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.