Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Jamii  »  JK, ya Ukerewe sawa, lakini…
JK, ya Ukerewe sawa, lakini…
By Habari Tanzania | Published  05/6/2007 | Jamii | Unrated
AKIWA Nansio, Ukerewe katika ziara yake inayoendelea mkoani Mwanza, miongoni mwa mambo aliyozungumza Rais Jakaya Kikwete, ni juu ya mikakati ya kuisaidia Ukerewe kupiga kasi kiuchumi.

Amewashauri Wanaukerewe kujikita katika kilimo cha ndizi, huku akiahidi kuwapeleka wataalamu wa zao hilo kutoka Chuo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian, Arusha.

Aidha, amewataka kuanzisha kilimo cha maembe ya kisasa yanayoweza kuanza kutoa matunda baada ya miaka mitatu tu.

Na zaidi ya kilimo, amewahimiza madiwani kuhakikisha wanatafuta fedha za kujenga kiwanda cha kusindika matunda hayo, lengo likiwa kuwapa wakulima soko la uhakika na pia kuwahakikishia ajira ya kudumu kupitia kilimo au kazi za kiwandani.

Sisi wa Tanzania Daima, tunaamini kwamba, haya ndiyo mawazo ya kimapinduzi katika kilimo na kiuchumi kwa ujumla.

Kwa maana nyingine, Rais Kikwete hapa amepatia na anastahili kuungwa mkono katika hili.

Hata hivyo, tunapenda kushauri kwamba, wananchi wa Ukerewe wanahitaji zaidi ya ushauri wa wataalamu.

Kutokana na wakulima wengi kuwa na uwezo mdogo kifedha, ni vyema serikali ingeangalia jinsi ya kuwasaidia kwa mitaji ya kuanzisha aina ya kilimo kinachoshauriwa.

Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba, si mazao yanayoweza kuvunwa ndani ya kipindi kifupi, na bila shaka yatahitaji uangalizi wa karibu, unaokwenda sambamba na gharama.

Tunaamini hilo lipo ndani ya uwezo wa serikali, na ikiwa na dhamira kama inavyokazania katika mambo mengine kama ya ununuzi wa rada na ndege ya rais, bila shaka haitaishia kuwasha cheche za maendeleo Ukerewe pekee, bali katika maeneo mengine mengi nchini, kwa mfano Dodoma ambako mbali ya zabibu, ni wakulima wazuri wa karanga.

Hali kadhalika Tanga ambako utajiri wake wa matunda kama machungwa yanageuka chakula cha ndege, nako kunahitajika kuangaliwa mara mbilimbili, ili wananchi waweze kunufaika na jasho lao linalopotea bila faida kila mwaka.

Kwa ujumla, karibu mikoa mingine nchini kila mmoja una utajiri wake, lakini kinachoshindikana ni kukosa mitaji ya kusukuma mbele kasi ya kujituma kujitafutia maendeleo.

Kwa serikali yenye kuona mbali, hili linapaswa kutiliwa mkazo, kwani licha ya kuwaongezea kipato wananchi wake na nchi kwa ujumla, kwa kiasi kikubwa itasaidia kupunguza wimbi la vijana wanaokimbilia mijini kila kukicha.

Tunasema huko anakozunguka Rais Kikwete, ndiko ziliko ajira milioni moja na zaidi, na njia pekee ya kutimiza ndoto hizo ni kuwapa uwezo wananchi, ikiwezekana hata kwa kukata mirija ya mashangingi na aina nyingine ya anasa zisizo na matunda ya moja kwa moja kwa mwananchi wa kawaida.

Ndiyo maana tunasema, ya Ukerewe tumekupata Rais Kikwete, lakini nguvu ya serikali iwe kubwa kuliko maneno ya jukwaani.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.