BASI la Akamba lililokuwa likisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Nairobi, Kenya, jana lilipinduka na kujeruhi watu takribani 35 baadhi yao vibaya katika maeneo ya Langejavi, Arumeru mkoani hapa.
Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 10:30 jioni, ambako inadaiwa chanzo cha ajali hiyo ni dereva kujaribu kumkwepa twiga na hivyo basi hilo kupinduka.
Tanzania Daima ilishuhudia magari kadhaa yakiwafikisha majeruhi hao kwenye Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, ambako walipokewa na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, waliokuwa wakisaidiana na manesi na madaktari wa hospitali hiyo.
Mamia ya wananchi walifurika huku wakiwa na majonzi kuangalia majeruhi hao waliokuwa wakifikishwa hospitalini hapo kwa matibabu, ambako baadhi hali zao zilikuwa ni mbaya, wengine wakiwa wamekatika mikono, miguu na majeraha mengine.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kanali Samwel Ndomba, akiongozana na Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Wenslaus Magoha, waliwasili mapema hospitalini hapo na kushuhudia baadhi ya majeruhi wakifikishwa hospitalini hapo.
Kanali Ndomba alisema habari zilizopatikana kutoka eneo la ajali ni kuwa, dereva wa basi hilo alikuwa katika harakati za kumkwepa twiga aliyekuwa eneo la barabara na hivyo kutokea kwa ajali hiyo.
Mkuu huyo wa mkoa alitoa wito kwa madereva kuzingatia usalama barabarani kwa kuendesha mwendo wa wastani ili kuepukana na ajali ambazo zinapoteza maisha ya Watanzania wengi.
Pia Kanali Ndomba alishuhudia Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa Mount Meru, Omar Chande akichelewa kufika hospitalini hapo licha ya kuwa ametaarifiwa.
Tanzania Daima ilifika hospitalini hapo majira ya saa 10:45 jioni na hadi saa 11:25 alipofika Mkuu wa Mkoa, mganga huyo alikuwa bado hajafika.
Baadhi ya majeruhi walifikia hatua ya kuandikiwa PF 3 na askari waliokuwako hospitalini hapo na kwenda kutibiwa hospitali nyingine.
Kanali Ndomba aliagiza majeruhi wenye hali mbaya ikiwamo waliokatika viungo, wafanyiwe utaratibu wa kuhamishiwa Hospitali ya KCMC.