Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kenya Airways yahofiwa kuua 115
Kenya Airways yahofiwa kuua 115
By Habari Tanzania | Published  05/6/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mkolo Kimenya


AJALI ya ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) iliyoanguka Cameroon na kuhofiwa kuua abiria wote 115, imemlazimu mwanasiasa maarufu wa Kenya, Uhuru Kenyatta kusitisha ziara yake ya kikazi nchini.

Kenyatta, Mwenyekiti wa Chama cha KANU na mgombea wa Urais aliyeshindwa katika uchaguzi mkuu wa Kenya mwaka 2002, aliiambia Tanzania Daima Jumapili jana kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza kwamba, amepata mshituko mkubwa uliomlazimu kurejea haraka nchini mwake.

Mwanasiasa huyo kijana na mfanyabiashara maarufu, alikuwa nchini kuhudhuria mkutano wa ukaguzi wa hesabu za serikali na usimamizi wa rasilimali.

Kenyatta mwenye umri wa miaka 46, anayeterajiwa kuipeperusha bendera ya KANU katika uchaguzi mkuu wa Kenya mwishoni mwa mwaka huu, pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wakaguzi wa Mahesabu Kenya (APC).

Akiwa mwenye majonzi, alisema: “Nimepata ujumbe unaoelezea kupotea kwa ndege yetu ikiwa na abiria 115 na wafanyakazi wanane.

“Hakuna mwenye habari za uhakika kuhusu kilichoipata ndege hiyo hadi hivi sasa (jana asubuhi), lakini taarifa zilizopo ni kuwa ndege imepotea ikiwa angani katika eneo la misitu,” alisema.

Kenyatta alisema alifanikiwa kuzungumza na ofisa mmoja wa Kenya Airways ambaye alimhakikishia kuwa ndege hiyo imepotea.

Alimkariri ofisa huyo akisema kuwa ndege hiyo ilikuwa itue Nairobi majira ya saa 12:15 jana asubuhi, lakini hadi kufikia majira ya saa nne ilikuwa haijatua na hakuna aliyekuwa anajua ilipo.

“Ni habari mbaya, nami siwezi kuendelea kuwepo katika mkutano ingawa nilipenda nibaki hadi mwisho, na pia kutembelea maeneo kadhaa ya Dar es Salaam, lakini sina jinsi, lazima niondoke,” alisema Kenyatta kwa masikitiko.

Ndege hiyo iliyonunuliwa miezi sita iliyopita, inadhaniwa kuanguka kusini mwa Cameroon karibu na mji wa Niete wakati ikielekea Nairobi kutoka nchini Ivory Coast.

Kwa mujibu wa redio ya serikali ya Cameroon, ndege hiyo ilipeleka taarifa ya mwisho kabla ya kupoteza mawasiliano katika mnara wa kuongozea ndege uliopo nchini humo muda mfupi baada ya kuruka.

Ndege hiyo KQ 507 aina ya Boeing 737-800 iliyokuwa ikitokea Abidjan, Ivory Coast na kuondoka Cameroon usiku wa saa tano kuamkia jana, ilipaswa kuwasili Naironi saa 12.15 asubuhi.

Kenya Airways ambayo ni shirika la umma, ina rekodi nzuri ya usalama, ingawa mwaka 2000 watu 169 walifariki wakati moja ya ndege zake ilipopata ajali.

Habari zilizopatikana baadaye zinasema kwamba, miongoni mwa waliokuwa kwenye ndege hiyo ni Mtanzania mmoja, Wacameroon 35, Wahindi 15, Wakenya tisa waliokuwa wafanyakazi wa ndege hiyo, Waafrika Kusini saba. Pia kulikuwa na raia wa China, Ivory Coast na Nigeria ambazo kila moja ilikuwa na raia sita.

Waingereza watano pia walikuwa kwenye ndege hiyo iliyobeba pia Wakongo wawili. Nchi nyingine zilizotajwa kuwa na raia wake kwenye ndege hiyo ni Niger, Afrika ya Kati, Ghana, Sweden, Togo, Mali, Uswisi, Comoro, Misri, Mauritius, Senegal, Marekani na Burkina Faso.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.