Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mambo yaenda kombo serikalini
Mambo yaenda kombo serikalini
By Habari Tanzania | Published  05/6/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Mwandishi Wetu


KUNA kila dalili sasa hali ya mambo kwenda kombo serikalini, jambo ambalo limeanza kuwatesa viongozi wakuu wa nchi, huku likiacha maswali mengi magumu kwa wananchi.

Hali hiyo inatokana na kutotekelezeka kwa ahadi za serikali ya awamu ya nne za kuwapatia maisha bora Watanzania pamoja na mwenendo mbaya wa uchumi wa taifa.

Mwenendo huu wa mambo, unaonekana wazi kuwatisha Watanzania ambao sasa wameanza kuitazama serikali kwa jicho la kuisuta na hata kufikia hatua ya kuinyoshea kidole, wakitaka iache kufuja fedha za walipakodi kwa kufanyia starehe na anasa.

Kitendo cha kuitia kasoro serikali hadharani kimefanyika kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, na Rais Kikwete amekuwa kiongozi wa kwanza wa taifa hili kufikishiwa ujumbe wa kuikosoa serikali yake kwa njia ya maandamano ya wafanyakazi.

Huku akiwa hajapata jibu la matumizi mabaya ya fedha za serikali, wafanyakazi waliyatumia maandamano yao ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi) kuelezea kusikitishwa kwao na matumuzi makubwa yasiyozingatia uwezo wa nchi, yanayofanywa na serikali.

Wakionekana dhahiri kutoridhika na matumizi makubwa ya fedha yanayofanywa na maofisa wa serikali, wafanyakazi walimwambia Rais Kikwete kupitia risala yao waliyomsomea katika Uwanja wa CCM Kirumba alikokuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Mei Mosi kuwa, inasikitisha kuona kuwa wakati kuna matumizi makubwa serikalini, wao wameachwa wakihangaika kwa kupata mishahara duni, isiyotosheleza mahitaji yao ya msingi.

Waliishangaa serikali ambayo pamoja na uchumi wake kuwa mdogo, bado matumizi yake katika baadhi ya maeneo ni makubwa kuliko hata katika nchi ambazo uchumi wake ni mkubwa.

Katika hili, jambo ambalo linaonekana kuwa mzigo mkubwa kwa serikali ni matumizi ya viongozi wa serikali wanapofanya ziara mikoani na wilayani huku wakiwa katika misafara mirefu ya magari ya kifahari yaliyonunuliwa kwa bei ghali na mtindo wa kununua samani za ofisi za serikali nje ya nchi kwa gharama kubwa.

Malalamiko haya ya wafanyakazi yametolewa siku chache baada ya Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, kukaririwa na vyombo vya habari akitetea matumizi ya magari ya kifahari yanayotumia fedha nyingi kuyahudumia, kwa viongozi wa serikali.

Jambo jingine linaloonekana kuitikisa serikali, ni mgomo wa wanafunzi wa vyuo vikuu, ambao sasa umebadilika sura na kuwa wa kisiasa zaidi, huku ukionekana wazi kumuelemea Rais Kikwete peke yake kutokana na ahadi aliyoitoa Februari, alipozungumza na wanafunzi wa elimu ya juu kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Ingawa msingi wa mgomo huo ni madai ya wanafunzi kupinga kuchangia asilimia 40 ya gharama za masomo yao, vyama kadhaa vya siasa nchini vimeudaka na kuufanya ajenda kabla ya kupanga kwenda mahakamani vikitaka wanafunzi hao waondolewe kero zao.

Rais Kikwete ambaye kwa kipindi kirefu amekuwa na uhusiano mzuri na wanafunzi wa elimu ya juu, ambao tangu wakati wa harakati zake za kuwania urais, walikuwa wakimuunga mkono, sasa amekuwa akitizamwa katika hali tofauti.

Kikubwa kinachomuweka katika hali hiyo, ni madai kwamba tangu alipotoa ahadi ya wanafunzi wa elimu ya juu kutofukuzwa kwa kukosa ada, amekuwa akikwepa kukutana na wasomi hao na kueleza mustakabali wa ahadi yake hiyo licha ya kuitwa zaidi ya mara tatu.

Rais Kikwete anadaiwa kupuuza wito wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa maelezo kuwa amebanwa na shughuli nyingine za kitaifa na wakati huo huo akihudhuria mahafali na ufunguzi wa shule mbalimbali za sekondari hapa nchini.

Kadhalika, kama ilivyo kwa vyama vya upinzani ambavyo vimekwisha kutangaza kuwaunga mkono wanafunzi na hata kutishia kuiburuza serikali mahakamani, kuishinikiza ibadili msimamo wake wa kuwafukuza wanafunzi hao, Chama Cha Mapinduzi (CCM) nacho kinaonekana kutia mkono wake katika mzozo huo.

Hilo linatokana na kubainika kwamba, mmoja wa makamishina wa Umoja wa Serikali za Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (TAHLISO), ambaye alikuwa miongoni mwa wanafunzi, waliotoa tamko la kuomba msamaha kwa Rais Kikwete, ni kada na kiongozi wa CCM Mkoa wa Kigoma.

Tatizo jingine kubwa ambalo linaonekana kuitikisa serikali, ni wimbi la wageni haramu wakiwemo wanajeshi wa Somalia waliokamatwa hapa nchini.

Pamoja na kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa mwaka jana wakati akizungumza na wazee wa Mkoa wa Mwanza kuwa, vyombo vya ulinzi na usalama viko makini kulinda mipaka ya nchi, udhaifu mkubwa umeonekana wazi katika ulinzi wa mipaka.

Udhaifu huo unathibitishwa na idadi ya Wasomali 199 waliokamatwa katika mikoa mitatu tofauti hapa nchini pamoja na taarifa zilizoripotiwa hivi karibuni za mpaka wa Sirari mkoani Mara kulindwa na kampuni binafsi ya ulinzi, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa taifa.

Sambamba na tatizo hilo la wageni haramu kufurika nchini, wimbi la ujambazi ambalo limekuwa likimuumiza kichwa Rais Kikwete tangu alipoingia madarakani, sasa linaonekana kuibuka upya, jambo ambalo huenda likamlazimisha kufanya operesheni maalumu ya kuwaangamiza majambazi nchini.

Hatua hii inaweza kufikiwa na Rais Kikwete baada ya mafanikio yaliyoonekana awali katika vita dhidi ya ujambazi kuonekana kama mafanikio ya muda tu kutokana na wimbi la ujambazi wa kutumia silaha kuanza kurejea kwa kasi.

Lakini kikubwa kichachoonyesha kuwa hali ya mambo haiendi vizuri serikalini, ni kuzidi kuporomoka kwa uchumi hali inayoibua hisia za wasiwasi miongoni mwa wananchi wa kada mbalimbali.

Ingawa hakuna kiongozi yeyote wa serikali aliyekwishakiri hadharani mpaka sasa kuhusu kudorora kwa hali ya uchumi, mwenendo wa mambo unaonekana si shwari serikalini.

Taarifa kadhaa zilizokwishatolewa na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, zikielezea kutoyumba kwa uchumi wa taifa, zinaonekana kuwa za kisiasa zaidi kutokana na kukinzana na hali halisi ya mambo.

Ripoti za kila mwezi za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na ile ya miezi mitatu zinazoonyesha kupanda kwa mfumo wa bei hadi kufikia asilimia 7.3 kwa Februari kutoka 7.0 Desemba, mwaka jana, zinatoa picha kuwa ndoto za kuendelea kuwa na mfumuko usiofikia asilimia 10 huenda zisiwepo.

Mambo mengine yanayoendelea kuitisa serikali, ni kuongezeka kwa deni la nje kutoka sh trilioni saba hadi tisa, matumizi mabaya ya serikali yanayokaribia sh trilioni moja, na nakisi ya sh bilioni 650 katika bajeti ya serikali.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Ngurudoto)
    Rating
    Mr. President needs to fire his PM, Mr. Edward Lowassa because he does not help him at all and he has nothing new to offer. Secondly, PM's office was the first to spend more that 3.5M for furnitures and other bogus reasons he gave to the parliament as soon as Lowassa was sowrn in as PM. This was like a down payment to him for accepting the job. Also, this money was just another way of showing how corrupt this man. Third, it is Lowassa who is blocking most of the debate in the parliament that are of vital importance to the developement of Tanzania. Also, he has presidential ambition so he sometimes sabotage his boss to make him looks bad.With this kind of a guy in the PM's office, we should not expect much from Kikwete.
     
Submit Comment


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.