WAKATI Serikali ya Awamu ya Nne ikisisitiza viongozi wafanye kazi kwa bidii kuwatumikia wananchi, watendaji wengi katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, jana waliziacha ofisi zao na kuhamia katika ukumbi wa mikutano wa Jengo la NSSF-Water Front.
Kuondoka kwa watendaji hao walioelezwa kuwa walikuwa wanahudhuria warsha, kulisababisha wizara hiyo ionekane kama imefungwa kwani wageni wote waliokuja kupata huduma walizuiliwa na walinzi getini kwa maelezo kuwa, hakukuwa na ofisa yeyote wa kuwashughulikia wizarani hapo.
Hali hiyo ilisababisha usumbufu mkubwa kwa watu wengi waliofika kupata huduma, kwani walinzi waliokuwa getini walionekana kutowajali na kuwafokea wakiwataka waondoke kwa kuwa ‘wizara ilikuwa imefungwa.’
Tanzania Daima ambayo ilifika katika jengo la ofisi za wizara hiyo, iliwashuhudia wananchi wakirandaranda nje ya geti, huku wakiwa wanalalamikia maamuzi ya wizara hiyo.
Walinzi hao walikuwa wanatiwa nguvu na tangazo lililokuwa limeandikwa na ‘Utawala’ na kubandikwa katika kuta za ofisi za wizara hiyo.
Tangazo hilo lilikuwa linasomeka: “Wateja wote wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii mnaarifiwa kuwa kesho Ijumaa tarehe 4-5-2007 hakutakuwa na huduma kwa wateja. Watumishi wote wa wizara watatakiwa kuhudhuria semina elekezi ya Katibu Mkuu na watumishi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Makao Makuu.”
Alipotafutwa kwa njia ya simu, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa, alithibitisha kuwa watumishi wengi wa wizara hiyo hawakuwepo ofisini jana kwa kuwa walikuwa wanahudhuria semina hiyo elekezi.
Hata hivyo, Profesa Mwakyusa alisema kuwa kulikuwa na maofisa kadhaa wakifanya kazi ofisini hapo.
Akionyesha mshangao, Mwakyusa alisema walinzi hao walikuwa wamefanya makosa kuwazuia watu wote waliofika kwa kuwa, baadhi ya maofisa walikuwapo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wenye shida wizarani hapo.
“Wapo wafanyakazi wachache ambao wamebaki hapa, hata mimi na sekretari wangu tupo hapa ofisini, endapo utafika unaweza kusikilizwa shida yako na kupewa maelekezo.
“Kwa wale ambao itashindikana tumeelekeza waje Jumatatu ofisi zitakuwa wazi… kwa kweli kama huna maelezo ya uhakika lazima huduma zitakuwa hafifu,” alisema.