Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  CCM inao mkono mzozo wa vyuo vikuu?
CCM inao mkono mzozo wa vyuo vikuu?
By Habari Tanzania | Published  05/5/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Lucy Ngowi


SURA ya mzozo unaowahusisha wanafunzi wa vyuo kadhaa nchini, imeendelea kubadilika na kuchukua kile kinachoonekana sura ya kisiasa.

Hali hiyo imebainika baada ya baadhi ya wanafunzi wa vyuo hivyo wanaopinga tamko la kuomba msamaha kwa Rais Jakaya Kikwete, kuutuhumu Umoja wa Serikali za Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (TAHLISO), kuwa ulifikia uamuzi huo kwa shinikizo la kisiasa.

Kikubwa kilichosababisha hali hiyo kutokea, ni kubainika kwamba, mmoja wa makamishna wa TAHLISO ambaye alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliotoa tamko hilo la kuomba msamaha kwa Rais Kikwete, ni kada na kiongozi wa CCM Mkoa wa Kigoma.

Mwanafunzi huyo ambaye hivi sasa anasoma katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, ni Mussa Chowo, ambaye taarifa zilizothibitishwa naye mwenyewe, zinaonyesha kuwa yeye ni Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Kigoma.

Kauli ya Chowo kuvitupia lawama kali vyama vya siasa wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumatano wiki hii, imetafsiriwa na baadhi ya wanafunzi kuwa alichukua uamuzi huo akilinda maslahi ya CCM.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu jana jioni, Chowo pamoja na kukiri kwamba yeye ni kada na kiongozi wa CCM, alisema msimamo wa TAHLISO hauna uhusiano wowote na masuala ya kisiasa.

“Mimi nilikwenda pale kama mwanafunzi wa Chuo Kikuu Huria na Kamishna wa TAHLISO na wala si kama kiongozi wa CCM,” alisema Chowo.

Alipotakiwa kueleza iwapo haoni kwamba msamaha aliokuwa akiutaka kutoka kwa Rais Kikwete ulikuwa ni rahisi kuhusishwa na masuala ya kisiasa, hasa ukizingatia kuwa yeye (Kikwete) ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Chowo alipinga madai hayo.

“Sisi tumemuomba msamaha Rais wa Jamhuri ya Muungano na si Mwenyekiti wa CCM. Nataka utambue kuwa madai ya wanafunzi ni ya msingi kabisa, isipokuwa tatizo ni njia tuliyotumia kufikishia madai hayo,” alisema.

Chowo alikanusha pia madai yaliyotolewa na baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, ambao wamekuwa wakidai kutoitambua TAHLISO.

Katika maelezo yake, Chowo alisema walifanya vikao vitano ambavyo viliwashirikisha Waziri Mkuu na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (DARUSO), ambavyo ndivyo vilivyofikia uamuzi huo wa kuomba msamaha.

Aidha, Chowo aliieleza Tanzania Daima kwamba, akiwa kiongozi na kada wa CCM, nafasi yake ya kimamlaka inaishia Kigoma na hana uwezo wa kufanya lolote katika ngazi ya taifa.

Chowo pia alikanusha madai ya baadhi ya wanafunzi wanaodai kuwa yeye alishamaliza kipindi chake cha ukamishna wa TAHLISO.

“Si kweli kwamba katiba inatoa mwaka mmoja tu. Ukimaliza muhula wa mwaka mmoja, unaweza ukachaguliwa tena kipindi kingine. Wakati uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni mwaka mmoja, sisi Chuo Kikuu Huria ni miaka miwili, na mimi nimechaguliwa na viongozi wawili kuwa kamishna.

“Sikupenda viongozi wa vyama vyote vya siasa watuingilie, wakiwamo wa CCM,” alisema mwanafunzi huyo ambaye pia ni mwanasiasa kwa kujiamini.

Alisema wanapodai maslahi ya wanafunzi wakiwa chuoni, huwa hawaangalii maslahi ya kiitikadi na ndiyo maana wakati fulani kiongozi wa juu wa DARUSO alipata kuwa mwanachama maarufu tu wa Chadema, jambo ambalo wao hawakuliona kuwa ni tatizo kabisa.

Jumatano wiki hii, TAHLISO waliitisha mkutano wa waandishi wa habari na wakatoa barua waliyomuandikia Rais Kikwete, wakimuomba awaonee huruma wanafunzi waliosimamishwa masomo, na awaombee warudi shuleni wakati matatizo yao yakiendelea kushughulikiwa kwa taratibu zinazofaa.

Kwa mujibu wa TAHLISO, wengi wa wanafunzi walishindwa kutumia njia sahihi katika kufikisha madai yao ya kuitaka serikali iwaondolee mchango wa asilimia 40 ya gharama za masomo.

Hata hivyo, siku moja baada ya tamko hilo, baadhi ya wanafunzi katika Bunge la Serikali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO) walijitokeza na kupinga tamko hilo na kusema kuwa umoja huo hautambuliki kwani tokea waanze harakati za kupinga asilimia 40, hawakuwahi kushirikiana nao.

Wakati huo huo, ofisi ya uhusiano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam imetoa taarifa ya kuongezwa kwa muda wa mwisho wa kupokea maombi ya kurejeshwa tena chuoni hadi Mei 9, mwaka huu. Muda wa mwisho uliokuwa umepangwa awali, kwa wanafunzi kuwasilisha barua na malipo hayo ni jana.

“Kutokana na msongamano na milolongo mirefu iliyojitokeza kwenye matawi ya NBC na ofisi za Posta, iliyosababishwa na wanafunzi waliosimamishwa masomo wakati wa kutuma maombi ya kurejeshwa tena chuoni, uongozi wa chuo kikuu umeongeza muda wa mwisho wa kupokea maombi ya kurejeshwa tena chuoni hadi Mei 9, 2007,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa, masharti yote tisa yaliyotangazwa kwenye taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari kuhusu suala hilo, lazima yatimizwe kikamilifu na wanafunzi wote wanaotaka kurejeshwa masomoni.

“Wanafunzi wanakumbushwa kuwa, barua ambazo hazitakuwa na viambatanisho vya risiti za malipo ya fedha ambazo mwanafunzi anadaiwa, hazitashughulikiwa,” iliongeza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, majina ya wanafunzi ambao wataonekana hawana hatia baada ya kufayiwa mchujo, yatachapishwa kwenye magazeti Mei 12, mwaka huu.

“Ni kwa wanafunzi wale tu ambao majina yao yatachapishwa kwenye magazeti Mei 12, ndiyo watakaotakiwa kuripoti chuoni kwa ajili ya kuanza masomo,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa iliongeza kuwa, barua za maombi ya kurejeshwa tena chuoni ambazo zitatumwa baada ya Mei 9, hazitashughulikiwa mpaka mwaka ujao wa masomo.

Wakati huo huo, baadhi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili katika Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), wameulalamikia uongozi wa chuo hicho kwa kuwasimamisha masomo pasipo kupewa barua ya kuelezea makosa waliyoyafanya.

Mmoja wa wanafunzi hao, ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema kuwa, mfumo uliotumiwa na chuo hicho kuwasimamisha ni batili kwani wamesimamishwa bila kujua makosa yao kwa kuwa hawakupewa barua.

“Tumesimamishwa masomo, lakini haijatolewa sababu yoyote juu ya kusimamishwa kwetu, wakati sisi tumesimamishwa, wenzetu wanaanza masomo Mei 9 na mitihani wanaanza Mei 28… hatujui hatma yetu,” alisema mwanafunzi huyo.

Juzi, uongozi wa SUA ulitangaza rasmi kuwa Mei 9 mwaka huu ndiyo siku ya kuanza masomo kwa wanafunzi ambao hawamo katika orodha ya wanafunzi 34 waliosimamishwa masomo.

Wanafunzi hao pamoja na wengine, walifanya mgomo huo kama shinikizo la kuitaka serikali kurekebisha mfumo wa uchangiaji wa elimu ya juu nchini hali iliyosababisha kusimamishwa kwa muda kushiriki masomo chuoni hapo kuanzia Aprili 18, mwaka huu.

Hata hivyo, uongozi wa SUA haukuwa tayari kuweka bayana sababu za wanafunzi hao kutolewa uamuzi tofauti na wengine, muda halisi wa kusimamishwa kwao, masharti ya kurejeshwa chuoni hapo kama watahitaji kufanya hivyo na mambo mengine kadhaa.

Wakati huo huo, Kaimu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Taifa wa Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, amethibitisha kuwa viongozi wa chama hicho wataungana na viongozi wengine wa vyama vya upinzani katika maandamano na mikutano ya hadhara itakayofanyika mjini Morogoro kwa nia ya kuishinikza serikali ibadili mfumo wa uchangiaji wa elimu ya juu nchini.

Mnyika ambaye alizungumza na Tanzania Daima jana akiwa mkoani Mwanza, alisema kuwa, leo asubuhi ataondoka na ndege kwenda Dar es Salaam, ambapo yeye atakuwa kiongozi wa msafara.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.