Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Jamii  »  Tuna wasiwasi na hali ya usalama wa taifa
Tuna wasiwasi na hali ya usalama wa taifa
By Habari Tanzania | Published  05/4/2007 | Jamii | Rating:
MATUKIO ya kukamatwa kwa raia wa kigeni wanaoingia nchini, kinyume cha sheria za uhamiaji, ambayo katika siku za karibuni yameibuka kwa kasi, yametushitua na kutufikisha mbali.

Tumeshitushwa na idadi kubwa ya raia kutoka nchi za Somalia na Ethiopia waliokamatwa hapa nchini wakiwa hawana vibali vya kuwaruhusu kuingia katika kipindi cha wiki moja.

Kikubwa kilichotushitua, ni idadi kubwa ya wanajeshi kutoka nchini Somalia waliokamatwa mkoani Mbeya wakiwa njiani kwenda Afrika Kusini.

Sisi tunadhani kwamba, baada ya kutangazwa kwa habari za kukamatwa kwa wanajeshi hao ambao idadi yao ilitajwa kuwa ni 99, Watanzania ambao hapo awali walikuwa hawashituki wanapoona mgeni katika maeneo yao, sasa wamebadilika, wamekuwa makini na kila mgeni anayeonekana nchini.

Kudhani kwetu hivyo, kumetokana na ongekezo la kukamatwa kwa raia wa kigeni katika kipindi kifupi kilichopita baada tu ya kukamatwa kwa wanajeshi kutoka Somalia.

Lakini pamoja na kushitushwa na taarifa hizo, kuna mambo kadhaa yaliyotufikirisha mbali.

Tumejiuliza bila kupata majibu kuhusu hali ya ulinzi katika mipaka yetu ikoje? Tuna ulinzi wa uhakika mipakani au mipaka yetu iko wazi kiasi kwamba kila mgeni anayetaka kuingia anaweza kufanya hivyo bila kizuizi chochote?

Kama ulinzi mipakani ni legelege, kwa nini serikali haishitushwi na hali hiyo kwa kuzingatia kuwa ulinzi wa mipakani unapokuwa legelege hata hali ya usalama wa taifa nayo inakuwa shakani? Tunatamka wazi kuwa matukio haya yametufanya tuwe na wasiwasi juu ya hali ya usalama wa taifa letu.

Lakini kilichotufikisha mbali zaidi katika kufikiri, ni taarifa zilizotangazwa jana na baadhi ya vyombo vya habari kuwa, mpaka wa Tanzania katika eneo la Sirari mkoani Mara, unalindwa na kampuni binafsi.

Kampuni hiyo, ambayo imetajwa kuwa ni Mara Security Guards Limited, askari wake ndio wamepewa jukumu la kuruhusu au kuzuia magari yanayoingia na kutoka Tanzania.

Tunajiuliza, Tanzania imepungukiwa askari waliopewa mafunzo ya uhakika na ambao wamefundishwa kuwa na moyo wa kizalendo, walioapa kuilinda nchi hii, wa kuangalia usalama wa mipaka yetu, mpaka kufikia kuajiri kampuni binafsi kusimamia jukumu hilo kubwa?

Sababu ya kujiuliza hivi ni moja tu, kwamba kampuni hii binafsi iliyopewa jukumu la kulinda mipaka yetu, askari wake wana ujuzi kiasi gani katika shughuli za ulinzi?

Ingawa imeelezwa kuwa kituo hicho kina maofisa wanne tu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), ambao katika hali ya kawaida hawawezi kumudu kutekeleza majukumu yote yanayowakabili katika kituo hicho kwa ukamilifu, lakini hatutaki kuamini kuwa hiyo ndiyo sababu ya kuajiri kampuni binafsi ya ulinzi kulinda lango la kuingilia nchini mwetu.

Tunaamini kuwa, ulinzi wa kampuni binafsi katika mipaka yetu, ndio chanzo cha matatizo ya kuingizwa kwa bidhaa haramu na zisizofaa nchini mwetu na pia chanzo cha kuingia kwa raia wengi wa kigeni kinyume cha taratibu.

Hatutaki kuamini kuwa walinzi wa kampuni ya ulinzi binafsi wanaweza kufanya kazi sawa na maofisa uhamiaji au polisi. Na hili tunaamini serikali imelisikia na italifanyia kazi haraka.

Shaka yetu hiyo ndiyo imetufanya tufikiri na kuona kuwa, idadi kubwa ya wageni haramu wakiwemo wanajeshi wa nchi za nje waliokamatwa hapa nchini na kuacha mipaka yetu ilindwe na kampuni binafsi za ulinzi, vinaliweka taifa letu katika hali ya hatari.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.