WATU wanne, wanaoaminika kuwa majambazi, wamemuua kwa kumpiga risasi kifuani, askari mmoja wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) mkoani hapa.
Watu hao, waliokuwa na bunduki moja aina ya SMG, mapanga na rungu, walimpiga risasi askari huyo kifuani na kusababisha kifo chake, katika tukio la utekaji wa gari juzi jioni.
Akielezea tukio hilo la ujambazi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Patrick Byatao, alisema kwamba watu hao waliliteka lori aina ya Fuso, lililokuwa linatoka Kijiji cha Ilagala kuelekea Kigoma mjini majira ya saa 12 jioni, likiwa na abiria zaidi ya kumi.
Alisema kwamba gari hilo, lililokuwa linaendeshwa na Kayusa Abdallah, lilitekwa katika Kijiji cha Nyamori. Alisema watekaji hao walimuua askari huyo kabla hawajaanza kuwapora wasafiri fedha na simu za mkononi.
Alisema kuwa, fedha na vifaa vilivyoporwa vinakadiriwa kuwa na thamani ya sh milioni 1.2.
Kamanda Byatao amemtaja askari aliyeuawa na majambazi hayo kuwa ni MT 44491 Sajenti Raphael Kayungilo wa 24KJ, aliyekuwa anatoka kambi ya JKT Bulombora, kuelekea mjini Kigoma.
Akisimulia tukio hilo, Byatao alisema baada ya kumlazimisha dereva kusimamisha gari hilo, mmoja wao alipomwona askari huyo, alimuamuru mwenzake aliyekuwa na silaha kumuua kwa hofu ya kudhibitiwa kabla ya kutekeleza malengo yao.
Aliwataja abiria ambao waliporwa fedha na mali nyingine kuwa ni pamoja na dereva wa gari hilo, Kayusa, aliyeporwa sh 700,000, Athuman Mbano alinyang’anywa sh 500,000 na simu ya mkononi aina ya Nokia na wengine walioporwa kiasi kidogo kidogo cha fedha.
Katika tukio hilo, wananchi wakiongozwa na dereva wa gari hilo, ambaye pia amepitia mafunzo ya mgambo, walifanikiwa kuipokonya SMG hiyo kutoka kwa mmoja wa wavamizi hao. Silaha hiyo ilitambuliwa kuwa ni SMG yenye namba 15135679, ikiwa na magazine moja na risasi 20.
Jambazi huyo aliyenyang’anywa silaha alipigwa vibaya na watu hao na kusababisha alazwe katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma, Maweni kwa matibabu akiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Aidha, kamanda huyo alisema kuwa polisi bado wanaendelea na upelelezi kuwabaini watu wengine waliohusika na tukio hilo la ujambazi.
Byatao alitoa mwito kwa wananchi mkoani hapa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili wahusika watiwe mbaroni sambamba na viongozi wa vitongoji, vijiji na kata kutoa taarifa kwa jeshi hilo pindi wanapowaona watu wasiowafahamu katika maeneo yao.
Mwili wa marehemu umesafirishwa kupelekwa nyumbani kwao wilayani Kibondo kwa ajili ya mazishi.