BENKI ya Exim, jana ilizindua kadi mpya (Master Card) itakayotumika kuchukulia fedha ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Sabetha Mwambenja, alisema mtumiaji wa kadi hiyo ataweza kuitumia hata akiwa nje ya nchi.
Mwambenja alisema wameamua kuanzisha kadi hiyo ili kuwasaidia wateja kutosafiri na fedha nyingi mifukoni wanapokuwa na safari nje ya nchi.
“Tumeamua kwa makusudi kuanzisha huduma hizi kwani zitasaidia wateja kutobeba maburungutu ya fedha ambapo wanaweza kupoteza au hata kuibiwa, lakini ukiwa na kadi si rahisi kuibiwa,” alisema.
Mwambenja alisema wateja watakaohitaji fedha zaidi kwenye akaunti zao kwa kutumia kadi hizi, wataweza kukopeshwa na watakapoingiza fedha zitakatwa kufidia.
Benki hiyo ina jumla ya wateja 80 ambao tayari wanatumia huduma ya kadi hiyo.