Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kanisa Katoliki Z’bar lapinga Mahakama ya Kadhi
Kanisa Katoliki Z’bar lapinga Mahakama ya Kadhi
By Habari Tanzania | Published  05/4/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Mwandishi Wetu


KANISA Katoliki Jimbo la Zanzibar, limepinga kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara kwa madai ni kwenda kinyume cha katiba ya Muungano ya mwaka 1977.

Hayo yalijitokeza katika kikao kilichowashirikisha viongozi wa kanisa hilo Zanzibar na viongozi wa Tume ya Kudumu ya Kurekebisha Sheria ambayo ipo Zanzibar chini ya Kamishna wake Jaji mstaafu Edward Mwesiumo.

Wakisoma tamko lao katika kikao kilichofanyika jana, viongozi wa kanisa hilo walisema kwamba Serikali ya Muungano haipaswi kuanzisha mahakama za kadhi na badala yake jukumu hilo liachiwe Baraza Kuu la Waislamu nchini (BAKWATA).

Akisoma tamko hilo, Mchungaji Peter Minja, alisema hatua hiyo inaweza kuathiri umoja wa kitaifa kwa wananchi wa Tanzania kwa vile mahakama hizo zitapaswa kuhudumiwa na walipa kodi wote nchini.

“Kwa vile ombi hili limetoka serikalini, tunachoweza kufanya si kuingilia bali ni kuishauri serikali kwamba imeacha njia yake, hasa kwa kuzingatia serikali haina dini,” alisema Mchungaji Peter katika kikao kilichohudhuriwa na wachungaji na watawa zaidi ya 40 kutoka Unguja na Pemba.

Alisema kwamba Kanisa Katoliki linaamini chanzo cha kuibuka kwa mjadala wa kuibuka kwa mahakama za kadhi ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa vile kiliahidi katika Ilani yake ya uchaguzi ibara ya 108, kuanzisha mahakama za kadhi Tanzania Bara iwapo kitashinda katika uchaguzi.

“Tunakishauri Chama Cha Mapinduzi kutoibua mijadala isiyokuwa na faida na pia tunakiomba kisivae kofia mbili, yaani serikali na kofia ya dini na kinapaswa kujisahihisha,” alisema mchungaji huyo.

Alieleza kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Muungano, chama chochote cha siasa kinapaswa kuzingatia suala la umoja wa kitaifa na kufanya mambo yake bila ya kuwepo ubaguzi wa dini, kabila wala rangi.

“Tunafahamu kuwa mpango huu wa Chama Cha Mapinduzi ulikuwa na lengo lake kuu moja, kutumia ushawishi au hisia za kidini, kwa lengo la kupata kura, kwa maana moja wameanza kuigawa Tanzania,” alisema.

Alieleza kwamba, Mahakama ya Kadhi Zanzibar imeanzishwa muda mrefu, lakini hata hivyo inafanya kazi zake kinyume cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwa vile serikali inalazimika kuihudumia utendaji wake na kulazimika kutumia mapato ya serikali.

Viongozi hao walisema Kadhi Mkuu wa Zanzibar anateuliwa na Rais wa Zanzibar na serikali kuhudumia gharama za usafiri uendeshaji, nyumba kitendo ambacho ni kinyume cha Ibara ya 19 ya Katiba ya Zanzibar ambayo inasema serikali aina dini.

Alisema kwamba pamoja na mahakama kama hizo kuwepo Zanzibar, bado zimekuwa hazitendei haki Wakristo, kwa vile watoto wa Kikristo wanapokamatwa ugoni, huozeshwa na mahakama hizo bila kuzingatia imani zao za kidini.

“Fedha zinazotumika kugharamia mambo hayo zote zinatoka katika kodi za wananchi. Je, walipa kodi ni Waislamu tu?” alihoji.

Akizungumzia suala hilo, Katibu wa Mufti Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga, alisema hakuna ubaya wowote kwa Serikali ya Zanzibar kuhudumia Mahakama Kadhi kwa vile zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa Zanzibar ni Waislamu.

Alisema kwamba ni jambo la kushangaza baadhi ya watu wanahoji kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi Tanzania wakati Tanzania ina ushirikiano na Vatican.

Alisema kwamba mahakama za kadhi Zanzibar zimeanzishwa kabla ya mapinduzi na zimefanya kazi kubwa ya kusimamia kazi ya kutafasiri sheria za Kiislamu.

Alieleza kwamba mahakama hizo kazi yake kubwa ni kusimamia matatizo ya urithi, ndoa na wakfu kwa mambo yanayohusu Waislamu pekee na bado nafasi imetolewa kukata rufaa Mahakama Kuu iwapo mhusika hakuridhishwa na maamuzi ya Mahakama ya Kadhi.

“Kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara hakutaathiri umoja wa kitaifa kwa vile mahakama hizi kazi zake ni kutafasiri sheria za Kiislamu katika mambo ya ndoa, urithi na wakfu,” alisema.

Mapema kabla ya kukutana na viongozi wa Kanisa Katoliki ambao walikuwa wakiongozwa na Mchungaji Cosmas Amani Shayo, tume hiyo ilikutana na masheikh wakiongozwa na Sheikh Omar Makungu.

Kamishna wa tume hiyo, Jaji mstaafu Edward Mwesiumo, alisema kwamba tume hiyo imeshatembelea mikoa mbalimbali Tanzania Bara na imeamua kufika Zanzibar ili kupata uzoefu wa mahakama za kadhi zinavyofanya kazi zake na kuona muundo wake.

Alisema kwamba tume hiyo inakusanya maoni kama utekelezaji wa maagizo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Muungano na baadaye ripoti yake itajadiliwa na wadau mbalimbali kabla ya kuwasilishwa kwa Waziri wa Katiba na Sheria ambaye ataiwasilisha katika Baraza la Mawaziri kabla ya kufikishwa bungeni.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.