Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Vyuo vikuu kituko
Vyuo vikuu kituko
By Habari Tanzania | Published  05/4/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Lucy Ngowi


WANASIASA, wanafunzi na wanaharakati mbalimbali, wamejitokeza kulaani tamko lililotolewa na Umoja wa Serikali za Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (TAHLISO), wakiiomba radhi serikali kwa mgomo wa wanafunzi.

Aidha, kwa upande wao, wanasiasa walilaani vikali tamko lililotolewa na umoja huo kuvitaka vyama vya siasa viache kuutumia mgogoro baina ya wanafunzi na serikali kama mtaji wa kisiasa.

Hayo yametokea siku moja tu baada ya TAHLISO kusema kuwa, imemwandikia Rais Jakaya Kikwete, kuomba radhi kutokana na mambo yaliyotokea wakati wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), na baadhi ya vyuo vikuu vingine walipogoma mwezi uliopita.

Wanasiasa waliozungumza na gazeti hili, waliwaelezea viongozi hao wa TAHLISO kama watu wasio makini, na kusema maamuzi wanayofanya ni ya kitoto.

Akizugumza na Tanzania Daima jana, Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi, James Mbatia, alisema kuwa umaarufu wa vyama vya siasa hautokani na mgomo wa wanafunzi hao.

Mbatia alisema kuwa, wakati vyama vya NCCR – Mageuzi, Tanzania Labour (TLP), Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) walipotoa matamko yao mara mbili, walizungumza kama wazazi.

Mwenyekiti huyo alihoji kwa nini TAHLISO ivionye vyama vya upinzani ilhali hata Umoja wa Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) mkoani Arusha, wamewahi kutoa matamko kuhusu sakata hilo.

Katika tamko lake, UDASA iliutaka uongozi wa UDSM kulegeza masharti ya kuwataka wanafunzi kurudi chuoni ikisema kuwa masharti yaliyowekwa ni magumu na ni wanafunzi wachache wanaweza kuyamudu.

“Statement ya wanafunzi ni ya kitoto sana. Ni kwamba taifa linazalisha watoto waliodumaa akili kwa kuwa hawawezi kufanya hili suala ni la wanasiasa pekee, kwa kuwa hata UDASA na TUCTA walilizungumza.

“Inaonyesha jinsi upeo wao wa mawazo ulivyo mdogo… wanafikiria sehemu hiyo tu, pia wanakubali kutumika. Wanajidhalilisha, ninawaonea huruma jinsi wanavyojishusha hadhi yao,” alisema Mbatia.

Kwa mujibu wa Mbatia, viongozi wa wanafunzi waliotoa tamko hilo kwa niaba ya wenzao, hawafai kuwa viongozi kwa kuwa wana mawazo yaliyodumaa na kuwa kama wangekuwa viongozi mahiri, wangeuzuia mgomo huo usitokee.

“Kama wao ni viongozi mahiri, kwa nini hawakuzuia huo mgomo? Sasa wameshagoma na wameleta hasara kwa taifa, ndiyo wanawanyoshea wanasiasa vidole. Si viongozi makini, wanachofanya ni utoto,” alisisitiza Mbatia.

Mbatia alisema kuwa, vyama vya siasa haviwezi kujitafutia umaarufu kwa kupitia mgomo wa wanafunzi.

Alisema kama walivyopanga awali, kesho muungano wa vyama vya upinzani wataanza maandamano yao katika Mkoa wa Morogoro, kuhamasisha mgomo wa wanafunzi nchi nzima, endapo serikali haitatengua uamuzi wake.

Wakati huo huo, baadhi ya wanafunzi katika Bunge la Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO) nao walijitokeza wakipinga tamko lililotolewa na viongozi wa TAHLISO juzi, na kusema kuwa umoja huo hautambuliki kwani tangu waanze harakati za kupinga asilimia 40, hawakuwahi kuwa na wanafunzi hata kwa kutoa tamko.

“Maamuzi ya bunge la SUA na DARUSO ni mgomo. Ndiyo njia stahiki, hivyo maamuzi ya viongozi wa TAHLISO ni kinyume cha matakwa ya mabunge yao,” alisema mmoja wa wanafunzi hao.

Wanafunzi hao walisema kuwa, tamko la TAHLISO ni la kisiasa, na umoja huo hauna mamlaka ya kumzuia Mtanzania yeyote kuhoji masuala ya kisera na utendaji wa serikali kuhusu elimu ya juu.

“Elimu ya juu inahusu wazazi na hata vijana ambao hawajaingia vyuo. Wanakataa siasa kwa kuwaponda wapinzani na kutetea msimamo wa UV-CCM,” alisema mmoja wa viongozi wa DARUSO.

Mwanafunzi mwingine aliyejitambulisha kuwa anasoma katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), aliushangaa umoja huo kuibuka hivi sasa wakati mgogoro umeshafika hatua ya wanafunzi kusimamishwa masomo.

“Kwanza ni umoja ambao hautambuliki, waziri hautambui kwani serikali ilishakataa kuusajili… sasa wanapata wapi mamlaka ya kutoa tamko kwa niaba ya wanafunzi?” alihoji.

Katika tamko lililotolewa na Kaimu Mkurugenzi Haki za Binadamu na Mahusiano na Umma wa CUF, Mbaralah Maharagande, chama hicho kilisema kimeshangazwa na taarifa iliyotolewa na TAHLISO, kutaka vyama vya siasa kuacha kutafuta umaarufu kupitia matatizo ya wanafunzi.

“CUF – Chama cha Wananchi, kinatambua kuwa wajibu wa vyama vya upinzani ni kuikosoa, kuishauri na kuishinikiza serikali katika mambo mbalimbali ambayo aidha haiyatekelezi au kuacha kuyatekeleza kwa jamii husika, hasa katika maslahi ya taifa kama vile suala la mgogoro wa malipo ya asilimia 40 katika elimu ya vyuo vya juu yaliyojitokeza hivi karibuni,” alisema Maharagande.

Aliwataka viongozi wa TAHLISO kufahamu kuwa, elimu ya juu si suala la mtu mmoja au chama fulani, bali ni la Watanzania wote, wakiwemo wanafunzi, wazazi wao ambao baadhi ni wanasiasa pamoja na wengine ambao hawana vyama.

“Sisi kama vyama, kulisemea hilo tuko sahihi na wala hatutafuti umaarufu wowote, isipokuwa ni wajibu wetu na watoto wetu wasome na tupate wataalam wa nchi hii,” alisisitiza.

Aidha, Maharagande aliwakumbusha TAHLISO kuwa, katika maadhimisho ya kutimiza miaka 30 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanafunzi hao walivalishwa sare za CCM, kuhutubiwa na mwenyekiti wake katika Ukumbi wa Diamond na baadhi yao kukabidhiwa kadi, na pia kupewa ahadi ya kuwa hakuna mwanafunzi atakaekosa kusoma kwa sababu ya kukosa mkopo.

Hata hivyo, alisema kuwa hali haikuwa kama walivyoahidiwa kwani baadhi yao wameshafukuzwa chuoni na hivi sasa wanahangaika.

CUF ilisisitiza na kuitaka serikali itoe asilimia 100 ya mikopo kwa wanafunzi na kuwarejesha wote waliosimamishwa masomo bila masharti yoyote.

Wakati huo huo, Tanzania Daima jana ilishuhudia wanafunzi wengi wakiendelea kulipia asilimia 40 ya gharama za ada, fedha za matibabu pamoja na kutuma barua kwa ajili ya kuomba kurejeshwa chuoni.

Hata hivyo, baadhi ya wanafunzi walikiri kuwa wametuma barua bila kuambatanisha na stakabadhi za malipo kwa kuwa wazazi wao hawana uwezo wa kuwalipia kwa mkupuo.

Mmoja wa maofisa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema mwitikio wa wanafunzi hao unaonyesha kuwa wameanza kuelewa sababu za serikali kupanga gharama za mikopo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.