BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA), limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha sita, huku kiwango cha kufaulu kwa watahiniwa waliopata daraja la kwanza hadi la tatu kikiwa kimeshuka kwa asiliamia 19.9, ikilinganishwa na mwaka jana.
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa, shule zinazomilikiwa na serikali bado zimeendelea kupata matokeo mabaya kwa kulinganisha na shule binafsi.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, katika shule 10 bora zilizokuwa na watahiniwa 25 au zaidi, kulikuwa na shule nne tu za serikali.
Aidha, katika kundi la shule 10 zilizoshika mkia zenye watahiniwa 25 au zaidi, kuna jumla ya shule tisa za serikali dhidi ya moja tu ya binafsi.
Katika kundi hilo hilo la shule 10 zenye watahiniwa wa idadi hiyo hiyo ya wanafunzi 25 au zaidi, shule ya wasichana ya Kifungilo iliyoko Tanga, ndiyo iliyoongoza huku Shule ya Sekondari ya Mahiwa iliyoko mkoani Lindi ikishika mkia.
Kama ilivyokuwa kwa matokeo ya kidato cha nne, shule za Zanzibar bado zimeonekana kuendelea kuwa na matokeo mabaya kulinganisha na zile za bara.
Matokeo yaliyotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Joyce Ndalichako yanaonyesha kuwa, kiwango cha kufaulu kwa jumla kimeshuka kwa asilimia sita.
Dk. Ndalichako alisema: “Ubora wa kufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahimiwa wa shule unaonyesha kuwa, jumla ya watahiniwa 17,572 sawa na asilimia 66.7 wamefaulu katika daraja la I-III.
“Mwaka 2006, asilimia ya watahiniwa waliopata madaraja ya kwanza hadi ya tatu ilikuwa asilimia 86.6, hivyo idadi ya watahiniwa wa shule waliopata daraja la kwanza hadi la tatu imeshuka kwa asilimia 19.9, ikilinganishwa na mwaka jana,” alisema.
Ndalichako alisema jumla ya watahiniwa 29,239 sawa na asilimia 87.21 ya waliofanya mtihani huo wamefaulu na kwamba mwaka jana asilimia 93.31 ya watahamiwa wote waliofanya mtihani huo walifaulu, hivyo kiwango kushuka kwa asilimia sita. Kufaulu kwa jumla huchukua idadi ya watahiniwa waliofaulu kuanzia daraja la kwanza hadi la nne.
Pia alisema baraza limefuta matokeo yote ya mtihani wa kidato cha sita yaliyofanyika Februari mwaka huu ya watahiniwa 36 waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani huo.
Alisema watahiniwa wa shule waliofaulu ni 24,166 sawa na asilimia 91.32 ya waliofanya mtihani. Mwaka jana asilimia 96.26 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo walifaulu, hivyo watahiniwa waliokuwa shuleni waliofaulu imeshuka kwa asilimia 4.89 ikilinganishwa na mwaka jana.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, waliofaulu ni 5,073 sawa na asilimia 71.78 ya watahiniwa wote. Mwaka jana asilimia 82.28 walifaulu mtihani huo, hivyo ufaulu kwa watahiniwa hao umeshuka kwa asilimia 10.5.
Akizungumzia mahudhurio, alisema watahiniwa 35,214 walisajiliwa kufanya mtihani huo katika vituo 398, wasichana wakiwa 12,262 sawa na asimilia 34.8 na wavulana 22,952 sawa na asilimia 65.2. Watahiniwa 33,522 sawa asilimia 95.20 walifanya mtihani.
“Mwaka jana watahiniwa 28,147 walisajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha sita, hivyo kuna ongezeko la watahiniwa 7,067 sawa na asilimia 25.1 ikilinganishwa na watahiniwa waliofanya mtihani mwaka jana,” alisema.
Alizitaja shule 10 bora zenye watahiniwa 25 au zaidi kuwa ni Kifungilo Girls (Tanga), Mpanda Girls (Rukwa), St James Seminary Kilema (Kilimanjaro), Changarawe (Iringa), Nyerere High School-Migoro (Iringa), JJ Mungai (Iringa), Marian Girls (Pwani), Sanu Seminary (Manyara), St Joseph-Kilicha Seminary (Iringa) na Kantalamba (Rukwa).
Shule 10 za mwisho zenye watahiniwa 25 au zaidi ni Lake (Mwanza), Ifunda Girls (Iringa), Maswa Girls (Shinyanga), Zanzibar Commercial (Zanzibar), Lumumba (Zanzibar), Hammamni (Zanzibar), Ifunda Techn (Iringa), Longido (Arusha), Fidel Castro (Pemba) na Mahiwa (Lindi).
Pia alizitaja shule 10 bora zenye watahiniwa chini ya 25 ni Rubya Seminary (Kagera), Uru Seminary (Kilimanjaro), Kaengesa Seminary (Rukwa), Maua Seminary (Kilimanjaro), Masama Girls (Kilimanjaro), Itamba (Iringa), Genesis High School (Iringa), Likonde (Ruvuma), Dungunyi Seminary (Singida) na St Mary’s Sem-Mbalizi (Mbeya).
Shule 10 za mwisho zenye watahiniwa chini ya 25 ni Dongobesh (Manyara), Mount Kilimanjaro (Kilimanjaro), Tweyambe (Kagera), Popatlal (Tanga), Dodoma Central (Dodoma), Masjid Qubah (Dar es Salaam), Bukoba (Kagera), Mvumi (Dodoma), Al-farouq Seminary (Dar es Salaam) na Aldersgate (Dar es Salaam).
Wasichana 10 waliofanya vizuri kitaifa na shule walizosoma zikiwa kwenye mabano ni Mhandala Daudi (Dakawa-Morogoro), Tabu M. Said (Mukodoma-Arusha), Augusta D. Kalamule (St. Mary’s-Tanga), Zuhura M. Ally (Nangwa-Tabora), Jane Nelson (Sangu-Mbeya), Doreen E. Tesha (Kilakala-Morogoro), Rebecca Michael (Mpanda-Rukwa), Loveness George (Loleza-Mbeya), Hildegarde Augustine (St Mary Goreti-Kilimanjaro) na Tosi M. Mwakyamdile (Kifungilo-Tanga).
Kwa upande wa wavulana 10 bora kitaifa ni Martin J. Chegere (Pugu-Dar es Salaam), Japhet Fredrick (Mwika-Kilimanjaro), Ditrick Rwegasira (Kibaha-Pwani), Prosper J. Mrutu (Feza-Dar es Salaam), Mohamed A. Nassor (Feza-Dar es Salaam), Boniface Chacha (Ilboru –Arusha), David J. Mwasota (Kibaha-Pwani), Moses R. Mwageni (St. Joseph Kilocha-Iringa), Abel A. Mhagama (Changarawe-Iringa) na Salim Y. Ally (Ruaha (Iringa).
Hata hivyo, Katibu Mtendaji huyo alisema baraza limesitisha kutoa matokeo ya mtihani wa kidato cha sita kwa watahiniwa 94 ambao hawajalipa ada ya mtihani. Matokeo yao yatatolewa mara watakapolipa.
Pia alisema baraza limesitisha kutoa matokeo ya watahiniwa 20 wa Shule ya Sekondari Mudio kutokana na mkuu wa shule hiyo kutolipa ada ya watahiniwa.
Kwa upande wa mtihani wa stashahada ya ualimu, jumla ya watahiniwa 3,831 walisajiliwa kufanya mtihani huo kutoka vyuo 23. Vituo viwili vya Nkrumah na B. Mkapa vya Zanzibar havikufanya mtihani huo na kwamba vitaufanya Mei mwaka huu.
Alisema wahatiniwa 3,710 sawa na asilimia 97.73 wamefaulu masomo yote. Watahiniwa 83 sawa na asilimia 2.19 wamefaulu baadhi ya masomo, hivyo wanatakiwa kurudia masomo waliyofeli. Watahiniwa watatu hawakufaulu kabisa.
Matokeo ya kidato cha sita yataanza kuonyeshwa katika shule za sekondari za Jangwani, Zanaki, Azania, Tambaza, St. Anthony’s Mbagala, Kinondoni, Makongo, Jitegemee, Forodhani, Al-Haramain, Mbezi Beacha kuanzia leo.
Pia matokeo hayo yanapatikana katika tovuti ya NECTA, www.necta.go.tz na tovuti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, www.moec.go.tz
Katibu Mtendaji huyo alisema watahiniwa walioko nje ya Dar es Salaam wanaweza kupata matokeo yao kupitia kwenye tovuti hizo au kutoka shule walizosomea na katika Ofisi za Maofisa Elimu wa Mikoa.