Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Msongamano Dar wamtesa Lowassa
Msongamano Dar wamtesa Lowassa
By Habari Tanzania | Published  05/1/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu


TATIZO la msongamano uliokithiri wa magari katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, bado linaendelea kumuumiza kichwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

Zaidi ya mwezi mmoja tangu alipouandikia uongozi wa jiji hilo kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo, Waziri Mkuu sasa ameikumbusha Serikali ya Japan kukumbuka ahadi yake ya kushiriki katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.

Waziri Mkuu ameiomba Japan ikamilishe utafiti kuhusu upanuzi wa barabara za Jiji la Dar es Salaam na kuharakisha ufadhili wa mradi huo ili kupunguza msongamano wa magari kama ilivyopata kuahidi siku zilizopita.

Lowassa alitoa ombi hilo jana wakati alipokutana na Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Bunge ya Bunge Kuu la Japan, Tetsaro Yano ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu alimwomba mwenyekiti huyo na ujumbe wake, waangalie uwezekano wa kusaidia ujenzi wa barabara za mzunguko jijini Dar es Salaam (The Ring Road Project) na kusisitiza kuwa, endapo suala hilo litapatiwa ufumbuzi, litaokoa muda mwingi wa kazi ambao unapotea barabarani wakati watu wako kwenye foleni ya kwenda ama kurudi kazini.

“Ujenzi wa Ring Road ni muhimu kwetu, kwa sababu tunataka kuokoa muda mwingi ambao watu wanaupoteza wanapokuwa kwenye foleni ama wakija kazini ama wakirudi nyumbani,” alisema Waziri Mkuu.

Alimweleza Yano kwamba, tayari Shirika la Misaada ya Maendeleo la Japan (JICA) lilishafanya utafiti wa jinsi ya kupanua miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam na kwamba kinachotakiwa ni kuweka takwimu za hivi karibuni (to update) kwenye ripoti ya utafiti huo.

Hata hivyo, Lowassa alisisitiza kuwa ujenzi wa barabara za mzunguko usije ukazuia ahadi yao ambayo waliitoa kuhusu ujenzi wa barabara ya Mangaka hadi Tunduru.

Septemba mwaka jana, aliyekuwa balozi wa Japan nchini, Katsyuda Ikeda, alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba, nchi hiyo ilikuwa tayari kujenga barabara hiyo, ila bado walikuwa wanatafuta fedha za kufanya ujenzi huo, na akamuahidi kuwa, kwa vile ombi la mradi wa ujenzi wa barabara za mzunguko jijini Dar es Salaam (The Ring Road Project) ni jipya itabidi balozi anayekuja aendeleze mazungumzo hayo na Serikali ya Tanzania.

Yano ambaye aliongozana na ujumbe wa wabunge watatu kutoka Japan, alimweleza Waziri Mkuu kwamba wenzake ambao ni wataalamu zaidi, watafuatilia mambo ya kiufundi ya suala hilo. Balozi wa Japan nchini, Makoto Ito pia alihudhuria mkutano huo.

Yano alimwomba Waziri Mkuu atembelee Japan mapema iwezekanavyo na kumuahidi kuwa, atafuatilia ufadhili wa ujenzi wa barabara za Dar es Salaam mara baada ya kurejea nchini kwao. Anatarajiwa kuondoka nchini kesho.

Lowassa anatoa tamko hilo zaidi ya mwezi mmoja tangu auagize uongozi wa Jiji la Dar es Salaam kuchukua hatua kadhaa za haraka kuboresha mazingira ya jiji, ikiwa ni pamoja na kupunguza msongamano wa magari na kuimarisha usafiri wa abiria.

Katika barua yake ya Machi 9, 2007 aliyowaandikia Meya wa Jiji na wa manispaa za Ilala, Kinondoni na Temeke, na nakala yake kwa rais, Lowassa alitaka awe amepata taarifa ya utekelezaji wa maagizo hayo ifikapo Mei 15, mwaka huu.

Pamoja na kupunguza msongamano wa magari barabarani na kuimarisha usafiri wa abiria, Lowassa aliuagiza uongozi wa jiji kusimamia kikamilifu sheria na taratibu za barabarani na kuweka taa sehemu mbalimbali na hasa barabarani.

Maagizo mengine aliyotoa wakati huo ni pamoja na kuanzisha usafiri wa “tram” (mabasi kama treni yanayokwenda kwa umeme jijini), kusafisha jiji, kupanda miti na maua, kupaka majengo rangi na kuweka utaratibu wa kuwaonyesha watalii maeneo ya jiji.

Alisema kuwa, maagizo yote hayo yanapaswa kutekelezwa mara moja bila ya kusubiri na kwa yale mengine ambayo yanahitaji muda zaidi kama vile kuwatembeza watalii na usafiri wa “tram” mikakati ya utekelezaji ianze.

Waziri Mkuu alisema anaelewa kuwa kuna mipango ya muda mrefu ya kuanzisha usafiri unaoeleweka na kuondoa mabasi madogo, lakini haiwezekani kukaa kimya na kuwatazama wananchi wakipata shida.

“Yapo malalamiko mengi ya magari ya abiria kukatisha njia na madereva na makondakta kuwa jeuri kwa abiria. Ni wajibu wa mamlaka zinazohusika kuhakikisha kuwa sheria zote zinazohusu usalama barabarani na hasa zinazohusu magari ya abiria zinasimamiwa vizuri,” alisema.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.