Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kikwete: Nimepata mahali pa kuanzia
Kikwete: Nimepata mahali pa kuanzia
By Habari Tanzania | Published  05/1/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu


RAIS Jakaya Kikwete, amesema tatizo la udhibiti mbaya wa mapato na matumizi ya fedha za umma limekuwa likimkosesha amani kwa muda mrefu.

Aliyasema hayo ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumza na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Murilo Portugal, aliyekwenda kumtembelea.

Alisema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imemwezesha kupata mahali pa kuanzia, patakapomuwezesha kuchukua hatua dhidi ya halmashauri zitakazoshindwa kusimamia vyema fedha za umma.

Aidha rais alizitaka halmashauri hizo kutambua kuwa, agizo alilolitoa kwao halikuwa la masihara, kwani alikuwa akikusudia kuchukua hatua kali kwa halmashauri ambazo zitashindwa kutekeleza maelekezo yake.

“Ripoti hii ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imenipa mahali pa kuanzia, kwani ni tatizo ambalo limekuwa likininyima raha, na maneno niliyoyasema jana (juzi) kwenye mkutano wangu na watendaji wa serikali za mitaa, si maneno ya vitisho tu bali ninamaanisha yale niliyoyasema. Sitasita kuzivunja halmashauri zitakazoendelea kufanya vibaya na kuitisha uchaguzi mwingine,” alisisitiza.

Naye Portugal alieleza kuridhishwa na hatua anazochukua Rais Kikwete katika kuhakikisha udhibiti wa mapato na matumizi serikalini.

Alielezea kufurahishwa na hatua ambazo rais ameanza kuchukua katika kuhakikisha kwamba, kunakuwa na uwajibikaji katika udhibiti wa mapato na matumizi katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

“Nimesoma katika magazeti ya leo juu ya kauli yako kuhusu matumizi mabaya ya fedha za serikali na hatua unazokusudia kuchukua, huu ni mwanzo mzuri, na ninaamini kwamba kutakuwa na matokeo bora,” alisema Portugal.

Aliongeza kuwa, hatua hiyo pia imepokelewa vema na wabunge wa Kamati ya Fedha wakiongozwa na Mbunge wa UDP, John Cheyo, ambao alikutana nao jana, na kumueleza kuwa sasa wana imani kwamba wana rais ambaye anaunga mkono uwajibikaji.

Naibu Mkurugenzi Mkuu huyo wa IMF alisema, tatizo la matumizi mabaya ya fedha za serikali haliko Tanzania peke yake bali ni tatizo linalozikumba karibu nchi zote duniani.

Alibainisha kwamba wakati Serikali Kuu zinajitahidi kurekebisha makosa yao, hali bado ni mbaya katika Serikali za Mitaa.

Alimweleza rais kwamba fedha za serikali katika nchi yoyote ni lazima zitumike vizuri ili kuleta matokeo yaliyotarajiwa na kwamba udhibiti wa fedha hizo na uhakiki wa matumizi yake ni jambo la msingi.

Katika mazungumzo hayo, Naibu Mkurugenzi Mkuu alitaka, pamoja na mambo mengine kupata maelezo kutoka kwa rais kuhusu mipango mbalimbali ya maendeleo na kiuchumi inayofanywa na serikali.

Aidha, alisema kuwa, IMF inaridhika na hali ya mambo ilivyo nchini pamoja na juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali, na kuahidi kwamba, itaendeleza ushirikiano wake na Tanzania pamoja na kutoa misaada ya kiufundi na kimawazo wakati wowote Tanzania itakapohitaji msaada wa aina hiyo.

Kwa upande wake, Rais Kikwete alisema, bado Tanzania itaendelea kuhitaji misaada kutoka IMF katika mambo mbalimbali yanayohusu uchumi, maendeleo ya jamii na uendelezaji wa miundombinu na nishati.

Aidha, alionyesha kuridhishwa kwake na uhusiano na ushirikiano uliopo hivi sasa kati ya serikali na IMF.

Alisema kuwa serikali yake itaendelea kuweka mkazo katika uendelezaji wa kilimo ili kiwe cha kisasa na hivyo kuongeza tija kwa mkulima na kuboresha maisha yake.

Aidha, alisema mchakato za kupanua na kuboresha huduma za elimu, afya, nishati na miundombinu, ni mchakato endelevu, na kwamba ukusanyaji wa mapato na uwezeshaji wa chombo kinachohusika na ukusanyaji wa mapato hayo ni jambo linalopewa kipaumbele na serikali.

Mazungumzo kati ya Rais na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IFM, yalihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, Gavana wa Benki Kuu, Daudi Balali na Katibu Mkuu Fedha, Gray Mgonja.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.