JUZI kwenye viwanja vya Gymkhana mjini Zanzibar, Kampuni ya simu za mkononi ya Zantel ilitoa msaada wa vifaa na fedha vyenye jumla ya sh mil 16.1.
Kiasi hiki ni jumla ya thamani ya vifaa na pesa taslimu kwa timu za taifa za mchezo huo za wanaume na wanawake zinazojiandaa na mashindano ya Mataifa ya Afrika, yatakayofanyika Juni mwaka huu nchini Namibia.
Kwa muda sasa kambi ya timu hiyo ambayo inajiandaa na mashindano hayo makubwa kabisa barani Afrika kwa mchezo wa netiboli, ilikuwa ikisuasua kutokana na ukata na hata kusababisha kambi iliyokuwa imewekwa mjini Zanzibar kuvunjwa kutokana ukosefu wa fedha.
Ni wazi, msaada huu umekuja wakati muafaka kwani hiki ni kilio cha muda mrefu cha vyama vya mchezo huo Bara (CHANETA) na Zanzibar (CHANEZA) kuhusu umuhimu kwa kupigwa tafu katika kuziandaa timu hizo.
Hata hivyo, ni faraja kubwa kwa maendeleo ya mchezo huo baada ya Zantel kusikia kilio hicho na kutoa msaada huo ambao, unaweza kuwa ni mkubwa ambao haujawahi kutolewa kwa miaka ya hivi karibuni, ikiwa imebaki takribani mwezi mmoja tu wa maandalizi kwa timu hizo kabla ya mashindano hayo yatakayoshirikisha mataifa mengine 17 ya Afrika katika kinyang’anyiro hicho.
Ingawa msaada huu hauwezi kumaliza matatizo yote ya timu hii, lakini tunaamini utasaidia kwa kiasi kikubwa kwani asiyeshukuru kwa kidogo, ni hivyo hata apewe kiasi kikubwa.
Tunaamini, fedha hizi zitatumika kwa kazi iliyokusudiwa katika kuindaa timu ili kwenda kwenye mashindano ikiwa shindani na si shiriki au sindikizaji.
Sisi wa Tanzania Daima, tukiwa sehemu ya wadau wa michezo na maendeleo kwa ujumla, hatuna budi kuupongeza uongozi wa Zantel si kuonyesha mfano tu, bali kutoa msaada huu mkubwa kwa timu zetu za taifa.
Ni msaada uliokuja wakati muafaka, hasa ukizingatia ushindi bila maandalizi ni vigumu, hivyo Zantel timu husika zitauchukulia msaada huu kama changamoto ya wao kujiandaa vema ili kuwa washindani.
Huu ndio msaada wa kweli, kwani kwa msaada huu kutolewa katika kipindi hiki cha maandalizi, ni muhimu zaidi tofauti na wale ambao husubiri kupongeza timu inapofanya vizuri, ingawa pia si vibaya.
Zaidi ya hapo, Zantel imekuwa ni mfano wa kuigwa kwani baadhi ya kampuni zimekuwa zikichagua michezo ya kusaidia hususan soka wenye umaarufu zaidi huku mingine ikitelekezwa licha ya kuhitaji kupigwa jeki.
Kwa kuzingatia mafanikio ya mchezo wa netiboli ndani ya miaka mitatu, ambako Tanzania imekuwa ikishikilia mataji ya Afrika Mashariki, ikaona ni vema ikatoa msaada huo ili kuendeleza sifa nzuri ya Tanzania nje ya mipaka.
Kwetu tunasema, msaada huu wa Zantel, uwe chachu kwa wachezaji na viongozi wa netiboli na serikali kwa ujumla, kuongeza msukumo ili kufanikisha Tanzania inakuwa shindani katika mashindano kwa maslahi ya nchi.
Wachezaji kadhalika, msaada huu uwe changamoto ya kujiandaa na kujituma zaidi kwa mchezaji mmoja mmoja kisha kama timu, kwani hiyo ndiyo siri kubwa ya mafanikio.
Hiyo ni kwa upande mmoja wa shilingi, hatusiti kuwakumbusha viongoizi wa vyama husika kama alivyosema, mlezi wa mchezo huo, Mama Sadya Karume, kuwa viongozi nao waamke usingizini kwa kubuni vyanzo vya fedha kuondokana na kuwa ombaomba.
Hii ni changamoto nyingine kwa viongozi wa vyama vyote Bara na Visiwani, kwamba wawe na mikakati imara ya kujiwekea vyanzo vya mapato kwani ni vigumu kutegemea msaada wa wahisani kila yanapofika mashindano kimataifa au kitaifa.
Tunaamini, changamoto hii itafanyiwa kazi na viongozi wa vyama hivi yaani Bara (CHANEZA) na Visiwani (CHANETA), kwani kwa kufanya hivyo, wataondokana na utegemezi kila kukicha.
Hatusemi vyama hivi havistahili kuomba msaada, la hasha, bali jitihada za viongozi wa vyama husika nazo zinahitajika katika kuhakikisha vyama vyao vinaondokana na utegemezi, hivyo msaada wa serikali uwe pale inapolazimu kufanya hivyo.
Itakumbukwa mashindano hayo yalianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2002 nchini Ghana, lakini licha ya kuwa na nafasi, Tanzania ilishindwa kushiriki kutokana na ukata.
Hata hivyo, shime kwa wadau wa michezo na maendeleo kwa ujumla, kuwa tayari kuzisaidia timu zetu kwani Zantel, wameonyesha mfano, hivyo wengine wafuate.
Tunaamini, timu yetu itakwenda Namibia ikiwa shindani, hivyo kurejea nchini na ushindi kwa sifa ya Tanzania na kuondokana na dhana kuwa, Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu katika michezo kimataifa.
Tunamaliza kwa kusema, hongera Zantel kwa kuona umuhimu wa kuusaidia mchezo huu ambao umekuwa ukitengwa na baadhi ya wadau kwa sababu mbalimbali.