VYAMA vinne vya upinzani nchini vinajiandaa kwenda mahakamani kufungua kesi dhidi ya serikali kuitaka mahakama itoe tamko la kufuta masharti magumu yaliyotolewa kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili warejee masomoni.
Hayo yalisemwa jana na viongozi wa vyama hivyo, katika mkutano wao na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi ya makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF) yaliyoko Buguruni, Dar es Salaam.
Vyama vya upinzani vilivyoungana na kutoa kauli ya dhamira ya kwenda mahakamani ni CUF, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tanzania Labour Party (TLP) na NCCR-Mageuzi.
Viongozi wa vyama hivyo waliikumbusha serikali kuwa walishatoa notisi ya siku 21, kuitaka serikali iwarejeshe wanafunzi hao chuoni bila masharti yoyote, lakini hadi notisi hiyo inakaribia kumalizika, serikali haijaonyesha nia ya kutekeleza.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimetoa masharti tisa mgumu kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliosimamishwa masomo wanaotaka kurejea chuoni hapo.
Wanafuzni hao walisimamishwa masomo kufuatia mgomo walioufanya kuishinikiza serikali iwapatie mikopo ya kugharamia elimu ya juu kwa asilimia 100. Chini ya utaratibu wa sasa, wanafunzi wanapaswa kulipa asilimia 40 ya gharama hizo na serikali, kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, hutoa asilimia 60.
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kuwa taratibu za maandalizi ya kwenda mahakamani zimeshakamilika, hivyo inasubiri serikali itoe tamko la kubatilisha masharti yake kwa wanafunzi kuchangia asilimia 40, vinginevyo hatua za kisheria zitachuliwa dhidi ya serikali.
“Suala la kuipeleka serikali mahakamani litaambatana na kuwahamasisha wananchi pamoja na wanafunzi wa vyuo vyote vilivyofungwa kwamba wananchi ndiyo walipa kodi na si serikali,” alisema Profesa Lipumba.
Profesa Lipumba alisema kuwa haiwezekani serikali ikavunja sheria namba 9 (2004) inayosema wanafunzi wote watasoma bila ya kuchangia gharama zozote. Alisema sheria hiyo ilipitishwa na Bunge, na kitendo cha serikali kuacha kuitekeleza kinamaanisha kuwa Bunge halifanyi kazi zake ipasavyo.
Alisema serikali imesahau kuwa kipato cha mwaka mzima cha wananchi wengi ni chini ya sh 400,000, hivyo wengi wa Watanzania hawamudu kuchangia elimu ya juu kwa asilimia 40 iliyowekwa.
“Iwapo serikali itang’ang’ania suala la wazazi kuchangia asilimia 40, wengi hawatasoma na tutakuwa tunajenga taifa la watu mbumbumbu.
“Rais Jakaya Kikwete alishasema kuwa watoto wa maskini watasoma bure, Waziri wake Mkuu, Edward Lowassa, anapinga na kushabikia kufukuzwa kwa wanafunzi chuoni na kudai lazima watalipa hiyo asilimia 40, uwajibikaji wa utendaji wa pamoja uko wapi ikiwa kauli za kiutendaji zinapishana?” alihoji Profesa Lipumba.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Wilbrod Slaa, alisema kuwa Tanzania ni nchi pekee ambayo viongozi wake wamekuwa wakifanya maamuzi yanayotofautiana.
“Tunakwenda mahakamani ikiwa ni pamoja na kuhamasisha umma juu ya suala hilo, na pia kupambana na mwanasheria mkuu ili mahakama itamke kuwa wanafunzi wanapaswa kusoma bure kama sheria inavyotaka,” alisema Dk. Slaa.
Katika maandalizi ya kuhamasisha umma, Dk Slaa alisema Jumamosi ijayo vyama hivyo vitaandaa maandamano ya amani pamoja na mkutano wa hadhara wa pamoja mkoani Morogoro.
Katika hatua nyingine, Dk. Slaa aliitaka serikali kuwalipa fidia wanafunzi wote waliosimamishwa masomo kutokana na matatizo waliyoyapata katika harakati za kuwahi kuondoka katika maeneo ya vyuo.
Alisema baadhi ya wanafunzi walipotelewa na vitu vyao na baadhi ya wanafunzi wa kike walilazimika kujiingiza katika tabia za ajabu ili kupata fedha za kujikimu.
Naye Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, aliitaka serikaili kuacha tabia ya kutisha, kushindana na kukomoa kwa visasi.
“Wasione kuwa suala hili limeingiliwa na vyama vya siasa wao wakachukua hatua zaidi za kuwaumiza wananfunzi,” alitahadharisha.
“Uongozi huu unaogopa vibonzo vinavyowakosoa lakini vya kusifia wanavihitaji…hii ni aibu na wanakotaka tufike tumeshapajua, hawajui kuwa utawala wa Madagascar na Indonesia uling’olewa na migomo ya vyuo vikuu… vyuo 52 kwa Tanzania si vidogo,” alisema Mbatia.