Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wabunge waiamsha serikali usingizini
Wabunge waiamsha serikali usingizini
By Habari Tanzania | Published  04/30/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Irene Mark


WABUNGE wanaonekana kuitumia vema fursa ya kuishauri serikali kuhusu vipaumbele katika bajeti ijayo, walipoamua kuiamsha kutoka katika lindi la usingizi ambao umeifanya isahau kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa taifa.

Wakati serikali inaonekana kukidharau, wabunge bado wanaamini kuwa kilimo ndio sekta ambayo inaweza kulikomboa taifa, na wameitaka serikali kuhakikisha kuwa inatoa kipaumbele katika sekta hiyo kuanzia bajeti yake ijayo.

Wakizungumza katika kikao kilichofanyika mjini Dodoma cha kuishauri serikali kuhusu bajeti ya mwaka wa fedha ujao, hivi karibuni, wabunge walisema serikali ina nafasi ya kurekebisha makosa yake ya nyuma na kuonyesha kuwa bado inakiona kilimo kama uti wa mgongo wa taifa kwa kukitengea fungu linalostahili katika bajeti yake ijayo.

Walisema kuwa ili kuinua kilimo, serikali inapaswa kuangalia mbinu na njia bora za kuboresha miundombinu yake, kama njia mojawapo ya kuinua sekta ya uzalishaji mali kwa lengo la kuongeza ajira na kuinua pato la taifa.

Kuporomoka kwa sekta hiyo kumetokana na watawala wa awamu ya tatu kushindwa kuweka msisitizo kwenye kilimo, wabunge walibainisha na kusema kuwa, hali hiyo ilisababisha gharama za uingizaji wa bidhaa za nje kupanda.

Walisema kuwa ili kuboresha kilimo, ni lazima serikali katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha kufanya mapinduzi katika sekta hiyo kwa kuhakikisha mkulima anapewa vitendea kazi vya kisasa.

Aidha, serikali inatakiwa kujenga barabara kwa kiwango cha kuridhisha maeneo ya vijijini na kumwondoa mkulima kwenye jembe la mkono ambalo humpatia mazao kidogo yaliyo chini ya kiwango.

Inaelezwa kuwa, matatizo yanayoikumba nchi wakati huu yanatokana na watawala kuthamini zaidi wafanyabiashara na kuingiza bidhaa za nje kwa gharama kubwa ambayo inawagharimu zaidi wananchi wa kipato cha kawaida.

Akizungumzia kilimo, Mbunge wa Iramba Mashariki, Mgana Msindai (CCM), alisema kuwa kupanda kwa gharama hizo, kumezidisha mfumuko wa bei na kupaa kwa deni la nje hali inayozidisha umaskini kwa Watanzania walio wengi wanaotegemea kilimo.

Takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa, mfumuko wa bei umepanda kutoka asilimia 6.8 hadi 7.3 na wabunge walihusisha hali hiyo na sekta ya kilimo kupewa kisogo na wakulima kubaki maskini.

Kadhalika, kutokuwepo kwa wafadhili katika sekta hiyo kumeongeza idadi ya walanguzi wa pembejeo za kilimo na kusababisha kukwama kwa sekta ya kilimo nchini.

Ikiwa serikali itaiwezesha sekta binafsi hususan kwenye kilimo katika bajeti ijayo, iwepo pia mikakati ya kufufua mazao ya biashara kama kahawa, pamba, chai, korosho na mkonge.

Baadhi ya mikoa iliyokuwa maarufu kwa kilimo cha kahawa, hivi sasa mashamba yake yametelekezwa na baadhi ya wakulima kuweka mahindi kwenye mashamba hayo kutokana na kushuka kwa bei ya zao hilo kwa wanunuaji binafsi kwa kuwa haina ubora wa kutosha.

Kwa mujibu wa Msindai, kiwango duni cha mazao ya biashara kinatokana na uhaba wa pembejeo kwa wakulima, ubovu wa miundombinu kutoka shambani hadi sokoni na kilimo cha jembe la mkono.

Naye Mbunge wa Ubungo, Charles Keenja (CCM), alishauri bajeti ijayo kuweka kipaumbele katika kilimo kutokana na ukweli kuwa sekta hiyo muhimu imepoteza dira na mwelekeo wake.

Alisema ni lazima serikali ijibane katika bajeti hiyo kwa kupunguza matumizi kwenye baadhi ya maeneo ili kuweka fedha nyingi zaidi kwa wakulima na wataalam wa kilimo.

Aidha, alishauri pia kuwepo na mchakato wa ‘Master Plan’ katika kilimo nchi nzima itakayojumisha wataalam wa kilimo kutoka vyuo vya elimu ya juu watakaotoa elimu, dawa na pembejeo bora kwa wakulima.

Kadhalika, wabunge hao walitaka serikali pia kuweka kipaumbele katika elimu, hasa ya juu ambayo kwa siku za hivi karibuni imekumbwa na matatizo ya migomo kwa wanafunzi wake.

Katika hilo, serikali imetakiwa kuhakikisha vyuo vilivyopo vinazalisha wahitimu bora kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa kuliko kuacha mwendelezo wa migomo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.