Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Serikali yalitisha Tanzania Daima
Serikali yalitisha Tanzania Daima
By Habari Tanzania | Published  04/28/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Mwandishi Wetu


SERIKALI imetoa kile ilichokielezea kuwa ni onyo kali kwa gazeti la Tanzania Daima, ikilishutumu kutumia lugha ya matusi dhidi ya viongozi wakuu wa serikali, hususan Rais Jakaya Kikwete, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Taarifa ya Serikali iliyotolewa jana jioni, ililitaja Tanzania Daima kuwa moja ya magazeti mawili ambayo yamejenga tabia ya kutumia lugha za namna hiyo na zile za uchochezi dhidi ya umoja, mshikamano na utaifa wa Watanzania. Gazeti lingine ni Mwana HALISI.

Saa chache kabla ya kutolewa kwa taarifa hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Kassim Mpenda alimuita kwa dharura, Mhariri Mkuu wa magazeti ya Tanzania Daima na Sayari, Absalom Kibanda na akamueleza msimamo wa serikali kuhusu mwenendo huo.

Mpenda ambaye alikuwa na nakala ya gazeti hili la Jumatano ya wiki iliyopita, aliitaja makala inayoandikwa na Freeman Mbowe iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho, Waraka wa Mbowe kwa Kikwete (4), kuwa mfano mmojawapo wa makala zinazotumia lugha mbaya dhidi ya kiongozi mkuu wa nchi.

Kwa mujibu wa Mpenda, makala hiyo ya Mbowe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), inayochapishwa katika gazeti hili kila Jumatano kwa jina la ‘Tafakuri ya Mbowe’, ilikuwa na maneno mengi yaliyokuwa yakionyesha dharau kwa rais, ambaye ni kiongozi anayebeba dhamana ya kuliongoza taifa.

Hata hivyo, katika taarifa ya serikali iliyotolewa baadaye jana, jina la Mbowe wala safu yake hiyo halikutajwa kabisa zaidi tu ya baadhi ya maneno kutoka safu hiyo kutumiwa kama mfano wa matusi.

Kikubwa kinachoonekana kuikera serikali, ni maneno yafuatayo katika mada hiyo ya Mbowe; “Woga wangu ni kuwa taifa hili linaanza kuamini kauli za rais ni usanii. Ni uzushi. Ni danganya toto. Ni funika kombe mwanaharamu apite. Ni ubabaishaji. Rais anazungumza asichoelewa, asichokijua, asichoamini!

“Kama sivyo, basi ni kuwa rais wetu ni dhaifu; na wasaidizi wake wanamwona hivyo. Na wao ni dhaifu, pengine zaidi. Ni kwamba rais ana ubia na watu katika utawala wake, na hana kauli ya mwisho.

“Sifa zote hizi si sifa nzuri. Sisi watiifu kwa nchi yetu na kwako tunakueleza, kwani tunajua hao unaojaribu kuwakingia kifua, ndio hao hao wanaotumia fursa hiyo kuonyesha udhaifu wako. Nchi hii haijapata kupata kiongozi wa sifa mbaya kama hizi.

“Kiongozi mwongo, asiyeaminika hakika ni sifa mbaya isiyo na kifani. Ukimya wako si ushindi, ni uthibitisho wa hofu hiyo. Kataa sifa hiyo. Mtandao wako hauwezi kukusaidia kwenye hili. Onyesha kwa vitendo kuwa kweli huna ubia na wanamtandao, bali una ubia na wananchi wako.” Mwisho wa kunukuu.

Katika taarifa hiyo kali ya serikali ambayo kwa namna yeyote ile inaonyesha kusudio la serikali ama kulisimamisha au kulichukulia hatua za kisheria gazeti katika siku na wakati wowote ujao, serikali imesema bayana kwamba haitakuwa tayari kuivumilia hali hiyo iendelee bila ya hatua kuchukuliwa dhidi ya vyombo hivyo vya habari.

“Hata hivyo, vyombo vya habari ambavyo vitaendelea kukiuka uungwana na maadili ya habari, vyombo vya habari ambavyo vitaendelea kukiuka sheria za nchi, serikali haitasita kuvichukulia hatua, ili kulinda hadhi na heshima ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jershi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, kulinda hadhi na heshima ya taifa letu na kulinda maslahi ya umma,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inaeleza pia kwamba, kwa kusema hiyo haina nia ya kupinga kukoselewa na vyombo vya habari au mtu yeyote na kuongeza kwamba, serikali itaendelea kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari kama sehemu muhimu ya ujenzi wa demokrasia, utawala bora na haki za binadamu.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.