BUNGE la Jamhuri, moja ya mihimili ya dola, halijaridhishwa na msimamo wa serikali wa kuficha mikataba mikubwa, ambayo imeingia na kampuni za nje katika sekta mbalimbali za uchumi.
Spika wa Bunge la Muungano, Samuel Sitta, jana aliliambia gazeti hili kuwa, Bunge halijaridhishwa na msimamo wa serikali kuhusu kuficha mikataba hiyo.
Alisema kuwa Bunge haliridhishwi na sababu inayotolewa na serikali kwamba kuipeleka mikataba hiyo bungeni ni kuingilia mgawanyo wa madaraka kati ya Bunge na serikali.
Kwa hali hiyo, Sitta alisema sasa hivi, Kamati ya Uongozi ya Bunge, inafanya utaratibu wa kutaka kukutana na serikali, ili wajadiliane na kuliweka suala hilo sawa, kabla Bunge halijaanza kujadili mikataba mbalimbali ambayo serikali imeingia kwa niaba ya wananchi.
Hata hivyo, Sitta aliliambia gazeti hili kuwa, wakati jitihada hizo zikiendelea, ili kuweka utaratibu wa kudumu kuliruhusu Bunge kuijadili mikataba hiyo, mkataba wa kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond, ambao umepigiwa kelele sana, utajadiliwa na Bunge wakati wa kikao kijacho.
Alisema Richmond ni moja ya masuala yaliyomo katika ripoti iliyowasilishwa kwake na Kamati ya Kudumu ya Uwezeshaji na Biashara, ambayo inatakiwa kujadiliwa.
Sitta alisema ripoti hiyo haikuweza kujadiliwa katika mkutano wa saba uliomalizika wiki iliyopita, kutokana na ufinyu wa muda.
Alisema tayari ameshapata ripoti ya Kamati ya Uwezeshaji na Biashara inayoongozwa na Mbunge wa Bumbuli, William Shelukindo (CCM), yenye kurasa zaidi ya 100, ambayo ina taarifa mbalimbali na moja kati yake ikiwa ni Richmond.
Sitta alitoa kauli hiyo jana wakati alipoombwa kutoa ufafanuzi wa kauli ya Naibu Waziri wa Mipango na Uwezeshaji, Gaudence Kayombo aliyekaririwa akisema Bunge haliwezi kujadili mikataba mbalimbali iliyoridhiwa na serikali kwani kufanya hivyo ni kuingilia mgawanyo wa madaraka kati ya Bunge na serikali.
Katika mkutano uliopita, akijibu swali la Mbunge wa Bububu, Cosmas Masolwa, aliyetaka kujua iwapo serikali ina mpango wa kuileta mikataba mbalimbali ili iangaliwe na Kamati za Bunge, Kayombo, alisema serikali haina mpango huo kwani kwa kufanya hivyo itakuwa ni kuingilia mgawanyo wa madaraka kati ya Bunge na serikali.
Kauli kama hiyo iliwahi kutolewa Februari mwaka jana na Dk. Juma Ngasongwa wakati huo akiwa Waziri wa Viwanda na Biashara. Alisema: “Hatuwezi kuleta mikataba hiyo bungeni. Ninachowashauri wabunge wawe wanawahoji mawaziri wanaohusika na sekta husika na siyo kudai mikataba iletwe hapa bungeni.”
Akifafanua kauli hiyo, Sitta alisema Kamati ya Uongozi wa Bunge inatarajia kukutana na serikali kujadili juu ya suala hilo, ambalo limeanza kuleta sura mbaya na kutaka kupora haki za wabunge.
Alisema wabunge hawaruhusiwi kuhoji mikataba iliyoko kwenye mchakato wa maridhiano, lakini mikataba hiyo ikishakubaliwa, inakuwa si siri tena na wabunge na wananchi, wana haki ya kujua kilichomo ndani yake.
“Mikataba inapokuwa kwenye mchakato, pale ni sawa na jikoni, Bunge haliwezi kuingilia, lakini ikisharidhiwa, hapo si siri tena, na kama wabunge wanataka kuhoji, wanaweza kufanya hivyo.
“Sawa na mtu mnamtuma kwenda Canada, kule anachozungumza ni kitu chenye manufaa kwa taifa, lakini akirudi unamwambia ulichozungumza huko ni siri, haiwezekani,” alisema Sitta.
Alisisitiza kuwa, wabunge ni wawakilishi wa wananchi ambao wana haki ya kujua mambo mbalimbali kupitia wabunge wao, ikiwemo suala la mikataba mbalimbali inayoridhiwa na serikali.
Hata hivyo, Sitta alisema suala la mkataba wa Richmond ni suala dogo katika taarifa ya kamati hiyo, kwani ina mambo mengine mengi na kuhoji uhalali wa vyombo vya habari kung’ang’ania suala la mkataba wa Richmond.
Mbali ya kupingana na msimamo huo wa serikali, Sitta pia alipinga kauli inayodaiwa kutolewa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU), Edward Hosea, kwenye vyombo vya habari kuwa, suala la Richmond lipo mikononi mwa ofisi yake na kwamba kwa sasa haliwezi kujadiliwa na Bunge wala taasisi yoyote.
“Hili tulishalikataa tangu zamani na hata kwa akili ya kawaida, suala likiwa TAKURU haliwezi kuzuia kujadiliwa, lakini linapofikishwa mahakamani, hapo huwezi kuhoji.
“Kwa mfano, kesi ya Kasusura, alipokuwa mahakamani, wabunge hawawezi kusema ooho kaonewa au…, lakini Richmond kuwa mikononi mwa TAKURU haitupi sababu ya Bunge kutojadili,” alisema Sitta.
Kauli hiyo ya Sitta inafuatia kuulizwa na gazeti hili kuhusu barua aliyoandikiwa na Kamati ya Uwekezaji na Biashara ya Bunge iliyopendekeza kwa Spika, Bunge liunde kamati ndogo ya dharura kuchunguza mchakato mzima uliosababisha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuingia mkataba na kampuni iliyokosa sifa ya Richmond Development Corporation kwa lengo la kuzalisha umeme wa dharura.
Barua hiyo ya Februari 5, mwaka huu, ambayo Tanzania Daima ina nakala yake, ina kichwa cha habari kisemacho: ‘Haja ya suala la kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond kuchunguzwa na Bunge sasa’.
Kamati hiyo ilisema inajiuliza maswali mengi kuhusu Richmond, kama wanavyojiuliza wananchi wengi, lakini kwa vile haiwezi kuuona hata huo mkataba kati ya Richmond na TANESCO, hivyo kamati inaona haja na dharura kwa Bunge kuunda kamati teule kuchunguza mchakato mzima uliosababisha kampuni iliyokosa sifa stahili kuruhusiwa kutekeleza mradi mkubwa wa kitaifa,” ilisema barua hiyo.
Katika barua hiyo, kamati hiyo inasema moja ya hadidu za rejea za kamati teule itakayoundwa kuchunguza suala hilo, iwe ni kupata maudhui ya mkataba kati ya Richmond na TANESCO na kupendekeza kwa Bunge sampuli ya mikataba inayofaa kwa taifa, ambayo itafuatwa kwenye mikataba ya baadaye ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa nishati ya umeme nchini.
“Mheshimiwa Spika, hoja ya kuunda Kamati Teule tumeijenga kwenye ripoti ya kamati kuhusu utekelezaji wa shughuli za kamati kwa mwaka 2006, taarifa ambayo kamati inakuomba uitafutie muda ili iwasilishwe bungeni katika mkutano huu (uliopita), kuiwezesha hoja hiyo kupata baraka za Bunge,” ilisema barua hiyo.
Barua hiyo ilitaja maswali yanayohitaji majibu ya serikali kuwa ni kwanini TANESCO iliamua kuingia mkataba na kampuni hiyo ya Marekani, ambayo toka mwanzoni ilidhihirisha kutokuwa na uwezo wa kiutendaji na kifedha kuweza kutekeleza mradi huo.
“Kwa mradi nyeti kitaifa kama huo wenye kugharimu fedha nyingi, iliwezekanaje kwa TANESCO na Wizara ya Nishati na Madini kuiamini kampuni ya kigeni bila kuifanyia uchunguzi wa awali hata kwa kutumia ubalozi wetu Marekani katika hali ya dharura?
“Kamati ina taarifa za maamuzi ya mwisho kabisa katika mchakato huo kufanywa na Government Negotiating Team (GNT), iliyoundwa na Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. GNT ilisukumwa na sababu zipi za msingi kuiteua Richmond wakati ushauri wa kitaalamu wa TANESCO ulionyesha wazi kuwa kampuni hiyo haikuwa na sifa stahili?” iliendelea kuhoji barua hiyo.
Barua hiyo iliendelea kuhoji sababu za TANESCO kutovunja mkataba na Richmond baada ya kampuni hiyo kushindwa kutekeleza sehemu ya mkataba wake.
“Ni nini kilichoshawishi TANESCO kuikubali Richmond kurithiwa na kampuni nyingine huku shirika hilo la umma likitambua wazi kuwa hatua hiyo ingesogeza utekelezaji wa mradi huo mbele zaidi?
“Athari za kusogeza mbele utekelezaji wa mkataba huo, ni utekelezaji kuanza kipindi ambacho taifa halihitaji kabisa umeme wa ziada (kama sasa), huku taifa likilazimika kulipia mabilioni ya fedha kila mwezi kwa mitambo iliyofungwa tu, lakini haizalishi umeme,” ilisema barua hiyo.
Taarifa ya kamati hiyo ilitokana na kikao chake na Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Januari 25, kuhusu utekelezaji wa maagizo ya kamati ya kipindi cha fedha, mipango ya shirika ya muda mfupi na muda mrefu na maendeleo ya miradi ya uzalishaji umeme wa dharura.
Katika barua hiyo, kamati ilimtaka Spika kuipangia muda hoja hiyo ili ijadiliwe bungeni, lakini Sitta anasema hoja hiyo haikujadiliwa kwa sababu ya kukosa muda.