SERIKALI jana ilitangaza zawadi ya Siku ya Malaria Afrika, kwa kutoa bure dawa za kukabiliana na ugonjwa huo hatari unaopoteza maisha ya wananchi wengi hapa nchini, hususan watoto na wajawazito.
Uamuzi huo wa serikali ulitangazwa jana wakati wa maadhimisho ya siku hiyo katika sherehe zilizofanyika kitaifa katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa.
Pamoja na hilo, Profesa Mwakyusa alitoa onyo kali kwa watu wenye mtindo wa kuiba dawa kutoka katika bohari za serikali na kuziuza katika maduka ya dawa yanayomilikiwa na watu binafsi, hasa wafamasia na madaktari.
Alisema kuwa, endapo mfanyabiashara au mfanyakazi yeyote atabainika kutumia ujanja huo, basi sheria itachukua mkondo wake.
“Serikali inaagiza dawa zitolewe bure kwa wananchi, lakini wafanyabiashara wa dawa hutumia ujanja kuziuza dawa hizo ambazo mwananchi alistahili kupata bure… ole wao wale wanaoyeyusha dawa zetu na kupeleka kwenye mashirika… vyombo vya sheria vitachukua mkondo wake,” alisisitiza Profesa Mwakyusa katika hotuba yake iliyotangazwa moja kwa moja na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD).
Aidha, Profesa Mwakyusa aliziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinasimamia sheria ya maangamizi ya mbu, iliyokuwa ikitumika miaka ya sabini, ambayo mtu yeyote ambaye hazingatii maangamizi ya mbu, ikiwa ni pamoja na kufukia madimbwi na kufanya usafi, alikuwa akichukuliwa hatua za kisheria.
Kwa mujibu wa Profesa Mwakyusa, sheria hiyo ilizaa matunda na kupunguza maambukizi ya malaria na kusema kuwa, kama sheria hiyo itazingatiwa ipasavyo, maambukizi yaliyopo hivi sasa yanaweza kupungua.
Aidha, alisema kuwa hivi sasa wizara yake inajiandaa kutumia dawa ya kupuliza ya DDT, ili kupata uhakika wa kumaliza mbu na hivyo kupunguza maambukizi ya malaria kwa kiasi kikubwa.
Alisema nchi ambazo zimetumia DDT katika kuangamiza mbu, zimefanikiwa kumaliza malaria.
Akizungumzia hali ya ugonjwa wa malaria nchini, alisema kuwa umeendelea kuwa tishio, hasa kwa wajawazito na watoto wadogo, ambapo hivi sasa vifo vinavyotokana na ugonjwa huo vinaongoza.
“Hivi sasa watoto laki moja hufariki dunia kila baada ya saa moja, na asilimia 80 ya vifo vya watoto wadogo chini ya miaka mitano hutokana na malaria, wakifuatiwa na wajawazito ambapo malaria huchangia asilimia 20 ya vifo vyao,” alisema.
Alisema utafiti wa wizara yake umebaini kuwa, mtoto aliyepatwa na malaria asipopata matibabu ndani ya saa nane, kuna uwezekano mkubwa wa kumsababishia kifo.
Kwa mantiki hiyo, Waziri Mwakyusa alisisitiza watu kuwahi matibabu pindi wanapoona dalili za ugonjwa huo.
Akizungumzia siku hiyo ya malaria ya Afrika, ambayo kaulimbiu yake ya mwaka huu ni ‘Ifanye Afrika iwe huru dhidi ya malaria sasa, shinda malaria, uongozi bora na ushirikishwaji wadau huleta maendeleo’, Profesa Mwakyusa alisema kuwa siku hiyo ilitengwa na wakuu wa nchi za Afrika, ambao walikubaliana kupunguza tatizo la malaria kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2010.
Alisema malengo hayo yatafanikiwa kupitia kutekeleza maazimio yanayolenga kudhibiti dalili pia na kupata tiba, kudhibiti mbu kwa kufukia madimbwi.
Maadhimisho hayo yalikwenda sambamba na uzinduzi wa dawa mpya ya mseto ya kutibu malaria (Alu), ambapo waziri huyo alisema kuwa utaratibu unaandaliwa ili kila mtu aweze kupata dawa hiyo.
Akielezea sababu za kubadilisha dawa za malaria mara kwa mara, Profesa Mwakyusa alisema kuwa ni kutokana na kuwepo kwa usugu wa malaria kwa dawa zilizopita na kwa kuzingatia hali hiyo ndio maana serikali imekuwa ikifanya mabadiliko ya dawa.