Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Serikali yajipanga kuiokoa Tanesco
Serikali yajipanga kuiokoa Tanesco
By Habari Tanzania | Published  04/26/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Kulwa Karedia


SERIKALI inaandaa utaratibu maalum wa kifedha utakaoliwezesha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kukabiliana na tatizo la ukata unaolikabili kwa muda mrefu sasa.

Hatua hiyo ya serikali ambayo inatarajiwa kuanza katika mwaka ujao wa fedha baada ya kuwasilishwa katika bajeti ijayo, imekuja baada ya kubaini kwamba, shirika hilo linakabiliwa na mzigo mzito wa uendeshaji na madeni.

Kiongozi mmoja wa juu katika Wizara ya Nishati na Madini, aliieleza Tanzania Daima kwamba, hatua hiyo ya serikali itakwenda sambamba na mipango mingine kadhaa ya kulinusuru shirika hilo ambalo mbali ya kudaiwa, linawadai wateja wake kiasi cha sh bilioni 217.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, serikali tayari imeliagiza shirika hilo kuimarisha wigo wake wa ukusanyaji wa madeni, wakati yenyewe ikiendelea kujipanga kwa ajili ya kulisaidia kujiendesha.

“Ni kweli hali ya sasa ya TANESCO ni mbaya kama jana (juzi) mlivyomsikia Mkurugenzi Mtendaji, Dk. Idris Rashid akisema. Sasa tunaangalia uwezekano katika bajeti yetu ijayo namna ya kulisaidia shirika hili muhimu kwa nchi yetu ili isije ikafika siku likafa,” alisema kiongozi huyo ambaye hakuwa tayari kuandikwa jina kwa sasa.

Shirika hilo mpaka sasa linadai madeni ambayo yamelimbikizwa na wateja wake wakubwa na wadogo, hali iliyochangia kuyumba kimapato, na kusababisha kutangazwa kwa operesheni maalumu kukusanya madeni itakayoanza Mei 2 mpaka Novemba 30 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Dk. Rashid alisema hali ya shirika hilo ni mbaya, huku akilinganisha na gari chakavu ambalo haliwezi kusafiri mwendo mrefu.

Alisema mbali ya kudai madeni, TANESCO inahitaji kiasi cha sh trilioni moja ili kuweka mambo sawa, ikiwa ni pamoja na mfumo mpya wa uzalishaji na usafirishaji umeme toka maeneo unakozalishwa.

Desemba mwaka jana, maofisa kadhaa wa juu wa serikali, waliieleza Tanzania Daima kwamba, serikali ilikuwa imeanza kufanya mawasiliano na benki kadhaa kwa ajili ya kuisaidia kifedha TANESCO, ambayo ilikuwa tayari katika wakati mgumu kutokana na makali ya mgawo wa umeme.

Akizungumza na Tanzania Daima wakati huo, Waziri wa Fedha Zakia Meghji, alikiri kufikiwa kwa mazungumzo kati ya serikali na benki ambazo hata hivyo hakuzitaja.

Alisema wakati umefika sasa kwa TANESCO, taasisi pekee inayotambulika kisheria, yenye wajibu wa kusambaza umeme kwa watumiaji kitaifa, kuanza kujiendesha yenyewe badala ya kutegemea ruzuku kutoka serikalini.

Meghji ambaye alikuwa ameulizwa iwapo serikali ilikuwa imeshalikubali ombi la dharura la TANESCO la kuiangukia serikali, ikitaka ipatiwe sh bilioni 86 ili iweze kumudu gharama za uendeshaji, alisema ombi hilo ndilo ambalo wakati huo lingechukua sura ya mkopo badala ya ruzuku.

“Tayari serikali imeshazungumza na benki kadhaa za hapa ambazo zimekubali kutoa mkopo kwa TANESCO badala ya sisi kutoa ruzuku kama walivyotaka wao.

“Uamuzi huo ni sehemu tu ya mpango kabambe wa serikali wa kuinusuru sekta ya nishati ambayo hivi sasa ipo katika wakati mgumu kiuendeshaji kutokana na uwezo wa TANESCO kuzalisha umeme kupungua,” alisema Meghji na akalitaka gazeti hili kuwasiliana na Mkurugenzi wa Sera katika wizara yake, Mugisha Kamugisha kulizungumzia suala hilo kwa undani.

Tanzania Daima ilipowasiliana na Kamugisha kuhusu suala hilo, alisema kiwango ambacho TANESCO inakihitaji kutoka katika mabenki hayo, ni kati ya sh bilioni 200 na 250.

Kamugisha alisema ili kufanikisha kupata mkopo huo, serikali iliitafuta benki ya Stanbic ili iweze kuisaidia TANESCO kupata mkopo huo, ikiwa ni pamoja na kutafuta wawekezaji zaidi wa kusaidia harakati zake za kifedha.

Alisema serikali inaamini kwamba, ingawa wakati huo (Novemba 2006), uwezo wa serikali kumudu gharama za kuzalisha umeme ulikuwa umepungua, alikuwa ana imani kwamba, baada ya mvua kuanza kunyesha na mitambo inayosukumwa na maji ya Mtera na Kidatu kufanya kazi barabara, shirika hilo lingekuwa na uwezo wa kurejesha mkopo huo ambao tayari ulikuwa umepatikana kwa sehemu.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.