MUUNGANO wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania miaka 43 iliyopita, umeendelea kubakia kidonda kilichozaa misuguano isiyokoma katika kipindi chote hicho.
Pamoja na ukweli kwamba, makundi mbalimbali na yenye mitazamo tofauti yamekuwa yakiuelezea muungano huo kuwa ni jambo lenye manufaa makubwa kwa pande zote mbili, bado muundo wake na namna unavyoathiri mustakabali wa ndani na wa nje, umebakia kuwa chanzo kikubwa cha ukinzani wa hoja.
Wachambuzi kadhaa wa masuala ya kisiasa, kwa miaka kadhaa sasa, wamekuwa wakisema kwamba, sababu zilizosababisha uharaka wa uundwaji wa Muungano zimekuwa zikipoteza maana kadiri siku zinavyosonga mbele, hata kusababisha kuwapo kwa haja ya lazima ya kuangaliwa upya kwa muungano huo.
Hivi sasa, Muungano unapita katika kipindi kingine kigumu kabisa, wakati huu nchi wanachama waasisi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; Kenya, Uganda na Tanzania, zinapojadili kuhusu haja ya kuharakishwa kwa uundwaji wa shirikisho la nchi hizo tatu.
Ingawa kwa upande wa Tanzania kumekuwa na maswali mengi, kubwa na gumu linaloonekena kukosa jibu ni lile la Wazanzibari, ambao wamekuwa wakilalamikia hata kufikia kupinga namna nchi yao, iliyo na serikali yake, inavyolazimishwa kuingia katika ushirikiano kwa mgongo wa Serikali ya Muungano.
Aidha, muundo wa serikali mbili ambao umekuwa ukifanyiwa marekebisho ya hapa na pale, kimekuwa ndicho chanzo kikubwa kabisa cha migogoro ya kisiasa kutoka pande zote mbili, hali ambayo kwa vipindi tofauti katika kipindi cha miaka ya mwisho ya uhai wake, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mmoja wa waasisi wa muungano huo alilazimika kuchomoza na kuutetea bila mafanikio.
Muundo huo wa muungano, leo hii umekuwa chanzo kikuu cha serikali ‘kurushiwa mawe’ kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, kila upande ukiona ukionewa au kunyimwa fursa zake sawasawa.
Mbali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali zake kuendelea kutetea muundo wa serikali mbili kwa maelezo kuwa ndiyo sera ya chama chao, wanasiasa wa upinzani wamekuwa wakiuelezea muundo huo kuwa ni uliopitwa na wakati na chanzo kikuu cha kile kinachoitwa kero za Muungano.
Ingawa hata viongozi wakuu wa kiserikali, akiwamo Rais Jakaya Kikwete wamekuwa wakikiri kuwapo kwa kero za Muungano, bado msimamo wao umekuwa ni kuendelea na mazungumzo kupitia katika vikao kati ya Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi vyenye lengo la kuainisha kasoro na kuzitafutia ufumbuzi, pasipo kulazimika kubadili muundo wake.
Hata hivyo, kwa upande wa Zanzibar, nje ya CCM, muundo huo umekuwa ukitajwa kuwa mbinu ya kuvimeza visiwa hivyo kimadaraka, hasa kutokana na mabadiliko ya 11 ya sheria kumpokonya Rais wa Zanzibar nafasi ya kuwa makamu katika Serikali ya Muungano.
Wakati Wazanzibari wenye msimamo mkali wamekuwa wakitaka kumuona rais wao akichukua nafasi ya umakamu, Watanzania Bara wao wamekuwa wakipinga muundo huo kwa maelezo kwamba unatoa upendeleo wa wazi kwa Wazanzibari.
Mwenyekiti wa taifa wa Chadema, Freeman Mbowe anaamini kuwa, kuwapo kwa wabunge zaidi ya 60 katika Bunge la Muungano wanaoamua kuhusu masuala mbalimbali yasiyo ya Muungano, ilhali kukiwa hakuna Watanganyika wanaoamua lolote kuhusu Zanzibar, ni moja ya kasoro kubwa kabisa katika Muungano.
Kwa mujibu wa Mbowe, tatizo la muundo wa serikali mbili, limekuwa likilalamikiwa kwa kiwango kikubwa hata na viongozi wa CCM wenyewe ambao wamekuwa wakilalamikia chinichini wakati katika majukwaa ya wazi wakitetea mfumo wa serikali mbili.
Msimamo mkali wa Mchungaji Christopher Mtikila, wa kutaka kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika unaoungwa mkono na sera za vyama kadhaa vya upinzani kama NCCR-Mageuzi na Chadema, ni moja ya mambo ambayo yameendelea kuufanya Muungano kuendelea kubakia kidonda ndugu kisicho na tiba.
Tukio la hivi karibuni kabisa la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kukataa kutumika kwa Sheria ya Rushwa iliyopitishwa na Bunge hivi karibuni, ikitoa sababu kuwa rushwa si suala la Muungano, limezusha kelele nyingi na za chinichini bara na visiwani.
Wapinzani wa hoja hiyo ya SMZ, wamekuwa wakisema kuwa, uamuzi huo ni kichekesho kwani katika masuala mengine kadhaa yenye neema za wazi, tena yasiyo na sura ya Muungano na yaliyopitishwa na Bunge, kama vile mabilioni ya Kikwete, yamekuwa yakikubaliwa pasipo kuwekwa kwa vikwazo vyovyote.
Hata hivyo, hadi hivi sasa, jitihada kubwa zaidi ya kupigania mabadiliko ya muundo wa Muungano, zinaendelea kubakia kuwa ni zile za kundi la wabunge wa G 55 la wana CCM wote ambao walijenga hoja ya kutaka kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika, msimamo uliopingwa vikali na Mwalimu Nyerere, hata kumlazimu aliyekuwa Rais wakati huo, Ali Hassan Mwinyi, kumbadili Waziri Mkuu wake, John Malecela.
Matukio kama yale ya machafuko ya hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar, ya mwaka 1984 yaliyosababisha Mzee Aboud Jumbe apoteze urais wa visiwani kwa nguvu, uteule wa Amani Abeid Karume kuwa mgombea urais wa Zanzibar kinyume cha matakwa ya wajumbe wengi wa Kamati Maalum ya CCM Zanzibar, ni mifano miwili tu ya namna Muungano wetu ulivyo na matatizo makubwa ya kiuendeshaji.
Kwa ujumla, ukifanya uchambuzi wa kitu kinachoitwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ni kipi kati ya muungano na mgongano, unaweza kupata jibu moja kwamba vyote sawa.
Licha ya nia nzuri ya waasisi wa Muungano, Mwalimu Nyerere na Abeid Karume, ukweli ni kwamba Muungano huu haukufuata utaratibu, yaani kuanzishwa na ridhaa ya wananchi limebakia kuwa moja ya maswali yaliyokosa majibu ya kuridhisha.
Wadadisi wengine wa mambo wanasema kwamba, Muungano ulioanzishwa na watawala wetu wa kwanza, umeendelea kuwa mali ya watawala, huku wananchi wakilazimishwa kuukubali na kuaminishwa kuwa ni kitu bora kuwa nacho.