Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Siasa zavuruga Chuo Kikuu Dar
Siasa zavuruga Chuo Kikuu Dar
By Habari Tanzania | Published  04/25/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

*Wahadhiri Kitivo cha Sanaa wavutana na wa Uhandisi
*Baadhi ya viongozi washangilia serikali kuharibikiwa

Na Waandishi Wetu

MGOMO wa wanafunzi wa vyuo vikuu uliofuatiwa na tukio la wanafunzi hao kutimuliwa vyuoni, umeonekana kuibua mambo mapya kadri siku zinavyozidi kwenda.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwepo hali ya kubadilika kimtazamo na kifikra, kutoka kwa wahadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) hasa wale wanaotokea vitivo vya Sanaa, ambao siku za nyuma walikuwa wakiwaunga mkono wanafunzi katika harakati za kupigania haki zao, lakini sasa wanaonekana kushikamana na maamuzi ya viongozi wa chuo hicho sambamba na yale ya serikali.

Kabla ya kustaafu kwa Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Mathew Luhanga, mapema mwaka huu, wahadhiri hasa wa vitivo vya sanaa, walikuwa wakipinga maamuzi ya kuwafukuza wanafunzi vyuoni baada ya migomo.

Sasa wahadhiri hao wanaonekana kupinga kauli zao za zamani na kuungana na utawala wa Makamu Mkuu wa Chuo mpya, Profesa Rwekaza Mukandala. Profesa Mukandala awali alikuwa mhadhiri katika Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii, Idara ya Siasa na Utawala wa Umma.

Kulikuwa na hali ya wahadhiri wa vitivo vya Sanaa kuupinga wazi uongozi wa Profesa Luhanga, lakini sasa wanaonekana kukubaliana na huu wa Mukandala.

Hali ya kupinga kauli zao za zamani sasa inaonekana wazi kutokana na wao kudhani kuwa, chuo hicho kilikuwa kikiongozwa katika nafasi zote za juu na wahadhiri kutoka Kitivo cha Uhandisi na hivyo kupuuza kwa makusudi mawazo kutoka kwa wahadhiri wa vitivo tofauti na Uhandisi.

Mgomo wa sasa na kutimuliwa kwa wanafunzi ni wazi umeingiliwa na siasa za hali ya juu na wachunguzi wa mambo wanaeleza kuwa, inaweza kuathiri mwenendo wa uendeshaji wa chuo na hasa maisha ya wanafunzi chuoni hapo ambayo yamekuwa duni kadri siku zinavyokwenda.

Kumeingia siasa za vyama na nafasi kubwa ikiwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimekuwa kikijichukulia wanachama katika vyuo vya elimu ya juu.

Hata Rais Jakaya Kikwete alipotaka kuzungumzia ushughulikiaji wa suala la ulipiaji wa asilimia 40 za gharama za masomo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza na Sh100,000 kwa ajili ya matibabu kwa wanafunzi wanaoendelea na shahada ya kwanza, alifanya hivyo katika kikao cha CCM badala ya vikao vya serikali.

Kama ilivyo kwa upande wa wahadhiri chuoni hapo, pia ndani ya CCM makundi yaliyojiunda ndani yake baada ya kuteuliwa baadhi ya wenzao katika nafasi za juu serikalini, wapo wanaoshangilia mgomo huo wakidhani upande mwingine unaharibikiwa.

Habari zilizotufikia zinaeleza kuwa wamo baadhi ya mawaziri wa serikali hii ya awamu ya nne, ambao ni vinara wanaosherehekea kuharibikiwa kwa wanamtandao wenzao.

Wakati hayo yakiendelea, ni dhahiri mabango ya wanafunzi hao waliyokuwa wakiyaonyesha wakati wa mgomo na kubeba ujumbe wa kuiumbua serikali yanaonekana kuiudhi serikali, hivyo nayo kuamua kuwatunishia misuli.

Kitendo cha viongozi wa vyama vya upinzani kuipa serikali muda wa siku 21 ili chuo hicho kiwe kimefunguliwa rasmi bila masharti kwa wanafunzi, ni moja ya sababu inayoelezwa sasa kutumika kuwaumiza wanafunzi zaidi.

Kuna hali ya kuogopa kutekeleza wazo la kuwarejesha wanafunzi mapema kwani kama itafanyika hivyo, wapinzani wataonekana washindi kutokana na vitisho vyao kwa serikali.

Wakati akifunga kikao cha Bunge wiki iliyopita, Waziri Mkuu Edward Lowassa, alisema serikali inaunga mkono maamuzi yote yaliyochukuliwa na uongozi wa Chuo Kikuu, ikiwa ni pamoja na kuwarejesha nyumbani wanafunzi wa shahada ya kwanza.

Gazeti hili limebaini pia kuwepo hali ya kutofautiana kwa viongozi wa wanafunzi ambao wanaamini kuwa, watabakizwa nyumbani na kupata adhabu nyingine na kama chuo kitafunguliwa mapema, hatma yao inaweza isijadiliwe haraka huku pia nguvu ya wanafunzi wenzao kuwatetea ikipotea.

Wakati huo huo, UDSM imesisitiza kuwa itaendelea na msimamo wake wa kuwataka wanafunzi kutimiza masharti tisa yaliyotolewa kwa wanaotaka kurejea chuoni hapo, anaripoti Jonas Songora.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa na uongozi wa chuo kwa wanafunzi, uongozi umesema umepokea kwa mshangao taarifa iliyoandikwa na gazeti moja  kwamba chuo huenda kikalegeza masharti kiliyoyatangaza.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, wanafunzi walikuwa wameitwa jana kuchukua barua zenye maelekezo ya namna ya kurejea chuoni hapo.

Taarifa hiyo ya Afisa Uhusiano wa UDSM, Julius Sauli, imesisitiza kuwa wanafunzi wote wanaotaka kurejea masomoni ni lazima watekeleze masharti hayo yaliyotolewa na chuo mwishoni mwa wiki iliyopita.

Masharti hayo ni pamoja na kuwataka wanafunzi kulipia asilimia 40 ya fedha zote za mkopona pia kulipia Sh100,000 za matibabu. Pia imesisitiza kuwa wanafunzi watakaopokelewa ni wale watakaowasilisha risiti ya malipo kupitia benki ya NMB tawi la Mlimani kwa akaunti numba 040103001709.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Constantino Mkude)
    Rating
    Habari hii ni nzuri na inajitosheleza.Hata hivyo ingeweza kuwa nzuri zaidi kama angalau ingeonyesha hasara ya kutowarudisha mapema wanafunzi both kwa serikali na wanafunzi wenyewe.
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.