BAADA ya muda mrefu wa malumbano na mabishano kuhusu kile kinachoitwa kero za Muungano, serikali sasa imeamua kuishirikisha sekta binafsi ili kuukuza.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein, wakati alipokuwa anazungumza na jumuiya ya Watanzania wanaoishi Geneva, nchini Uswisi, ambako alikuwa katika ziara ya kiserikali.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema serikali imebaini kuwa sekta binafsi ina nafasi kubwa katika kukuza ushirikiano baina ya watu wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Hivyo, wakati umefika sasa wa kuishirikisha sekta hiyo, kama njia mojawapo ya kuhakikisha kuwa kero za Muuungano zinashughulikiwa.
Chini ya mpango huo wa kuishirikisha sekta binafsi, Dk. Shein alibainisha kuwa, serikali ina mpango wa kuandaa miradi ya kiuchumi ya pamoja itakayoishirikisha sekta binafsi.
Alisema ni matumaini ya serikali kuwa, mipango hiyo ya uchumi, ambayo utekelezaji wake upo mbioni, itasaidia kukuza uchumi wa pande zote mbili za Muungano.
Aidha, Dk. Shein alibainisha kuwa, Serikali ya Muungano na ya Zanzibar, tayari zimeshaanza kuchukua hatua madhubuti katika utekelezaji wa dhamira ya kuondoa kero zote za Muungano kwa lengo la kuimarisha umoja wa kitaifa.
Alibainisha kuwa, katika kufanikisha azma hiyo, Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, wamekwishakutana mara mbili, katika vikao ambavyo vimefikia maamuzi mbalimbali yanayolenga kutatua kero za Muungano.
Dk Shein aliwaambia Watanzania hao kuwa, mikutano inaonekana kuzaa matunda kwani baadhi ya mambo ambayo yanaonekana kuwa kero katika Muungano, yameanza kupatiwa ufumbuzi wakati masuala mengine yapo katika hatua ya kumalizika.
Aidha, katika hicho Dk. Shein alizungumzia jitihada zilizochukuliwa na serikali katika kukabiliana na changamoto za ujambazi, ukame na magonjwa mbalimbali ikiwemo homa ya bonde ya ufa (RVF), iliyojitokeza nchini mwanzoni mwa mwaka huu pamoja na masuala ya kuimarisha elimu, kilimo na ukusanyaji wa mapato kwa ujumla.