MWENENDO wa uchumi wa taifa ni wa kusuasua, hasa baada ya takwimu muhimu kuonyesha mwelekeo usioridhisha.
Ukweli huo ulibainishwa jana wakati wa mkutano wa wabunge na serikali, uliofanyika mjini hapa chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.
Takwimu za kiserikali zilizotolewa na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji mbele ya wabunge hao, zimeonyesha kuwa, mfumuko wa bei umepanda hadi kufikia asilimia 7.3 kutoka asilimia 6.8 ya Juni mwaka jana.
Kupanda huko kwa mfumuko wa bei, kumekuwa ni jambo linaloendelea kwa miezi 16 tangu Serikali ya Awamu ya Nne iingie madarakani baada ya mfumuko huo kuwa asilimia 5.7 wakati wa miezi ya mwisho ya mwaka 2005.
Mbali ya hilo, ilibainishwa pia kwamba, deni la nje ambalo Tanzania inadaiwa, lilikuwa limepanda kutoka sh trilioni saba hadi kufikia tisa, hali ambayo ilionyesha kumtisha Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee (CHADEMA).
Mwenendo huo wa mambo iwapo hautadhibitiwa, basi kuna hatari kwamba, ndoto ya serikali ya awamu ya tatu ya kuhakikisha kuwa mfumuko huo unakuwa ni wa tarakimu moja tu (one digit inflation rate), ukiwa chini ya asilimia 10, inaweza ikagota na hivyo kuwaongezea wananchi wa kawaida machungu kwa bidhaa kupanda bei.
Meghji aliyekuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya serikali katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2006/2007, alizitaja sababu za kupanda kwa mfumuko wa bei kuwa ni ukame ambao ulisababisha upungufu wa chakula, mgawo wa umeme na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
“Sababu zilizofanya kupanda kwa mfumuko wa bei ni uhaba wa chakula, tatizo la umeme nchini na bei ya mafuta katika soko la dunia hali ambayo hatuwezi kuizuia,” alisema Meghji.
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa, mapato ya nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2006/2007, yalifikia sh bilioni 1,311.697 kiasi ambacho ni asilimia 53 ya lengo kwa mwaka mzima.
Aidha, katika kipindi cha Julai mwaka jana hadi Februari mwaka huu, mapato ya ndani yalipanda hadi kufikia sh bilioni 1,733.085 kiwango ambacho ni asilimia 70.4 ya makadirio ya mwaka mzima.
Hata hivyo, Meghji aliirudia tena kauli iliyowahi kuzusha utata mkubwa pale aliposema, tatizo la umeme halikuathiri sana pato la taifa, wala kuyumbisha uchumi wa nchi kutokana na serikali kuliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuhakikisha umeme katika viwanda haukatwi ili kuendeleza uzalishaji na ukusanyaji wa mapato.
Kuhusu misaada ya wahisani, Meghji alisema walikuwa wameshatoa sh bilioni 732.176 kiasi ambacho ni sawa na asilimia 91 ya matarajio ya mwaka mzima.
Alisema misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ilifikia sh bilioni 333.1 kwa kipindi cha mwaka wa fedha uliopita na katika kipindi cha Julai hadi Februari, zilitolewa sh bilioni 544.587, sawa na asilimia 49.8 ya makisio.
Aidha, Waziri Meghji alibainisha kuwa, katika kipindi cha Julai mwaka jana na Februari, serikali ilitumia sh trilioni 2.98, kiasi ambacho ni asilimia 61.5 ya bajeti ya mwaka mzima wa 2006/2007.
Akifafanua matumizi hayo, Meghji alisema sh trilioni 1.8 zilitumika kwa matumizi ya kawaida kwa kulipa mishahara wafanyakazi wa serikalini na pensheni za wastaafu na sh bilioni 906.519 zilitumika katika shughuli za maendeleo.
Alisema katika bajeti hiyo, kiasi kikubwa cha fedha za maendeleo kilitegemea wahisani na mikopo mbalimbali kutoka nje ya nchi kwa kuwa nchi haijaweza kuendesha bajeti yake.
Baada ya taarifa ya Waziri Meghji, Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP) alionya akisema kuwa, jukumu la maendeleo ya nchi linamhusu kila Mtanzania, hivyo kuendelea kuwategemea wahisani kunaweza kukwamisha shughuli muhimu za maendeleo.
Alisema mara nyingine, wahisani hawatimizi ahadi zao kwa wakati, hali inayowalazimu wananchi wachangie fedha katika kutimiza miradi ya maendeleo iliyoainishwa kwenye bajeti.
“Mimi nashauri ahadi za wahisani zisiingizwe kwenye bajeti, kwani fedha zao haziji kwa wakati. Hali hiyo inawafanya wananchi waingie mifukoni mwao kuchangia maendeleo... shughuli za maendeleo ya nchi kutegemea wafadhili inaonyesha kuwa bado tunatawaliwa kisirisiri,” alisema Cheyo.
Aidha, aliishauri serikali kuweka mipango ya maendeleo sanjari na fedha za ndani za kutekeleza mipango hiyo ili kurahisisha ufanisi wake na si kuwagandamiza wananchi kwa kuwalipisha michango isiyowahusu.
Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), aliitahadharisha serikali katika kubuni njia nyingine za kuondoa mfumuko wa bei kwa kusisitiza shughuli za uzalishaji mali miongoni mwa wananchi.
“Suluhisho la kuondoa mfumuko wa bei ni kuongeza shughuli za uzalishaji mali... hapa tukiulizana nani anafanya kazi za kilimo, hakuna… kila mmoja anategemea mishahara au posho,” alisema Kabwe.
Alipongeza ongezeko la mapato lililofikia sh bilioni 259.9 hadi kufikia Machi mwaka huu na kuhoji sababu za kupanda kwa kiwango cha matumizi yanayofanywa na watawala wa serikali ya awamu ya nne.
“Mheshimiwa mwenyekiti, Mamlaka ya Mapato inafanya vyema katika makusanyo, lakini kwa nini tunatumia kuliko tunavyoingiza? Hili ni jambo la kujiuliza,” alisema Kabwe.
Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee (CHADEMA), naye alipongeza kazi ya ukusanyaji wa mapato inayofanywa na TRA, lakini akaungana na Kabwe kuhoji jinsi makusanyo hayo yanavyotumika.
Alisema: “Tumetumia sh bilioni 81 kwa ajili ya umeme na baada ya muda mfupi mvua zikaanza kunyesha kwa wingi, hivyo fedha tuliyowekeza kwenye umeme imepotea bure... hapa tunaona jinsi matumizi yalivyo mabaya… mambo ya Richmond na dada yake Dowans tutayajadili, hayajaisha.”
Katika mchango wake, George Lubeleje (Mpwapwa-CCM), alilenga kutaka kuwepo kwa uhuru miongoni mwa mihimili ya utawala. Aliitaka serikali kutenga fungu la fedha kwenye bajeti yake kila mwaka kwa ajili ya Idara ya Mahakama.