Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  BOT sasa yatetea matumizi serikalini
BOT sasa yatetea matumizi serikalini
By Habari Tanzania | Published  04/24/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
*Yasema tathmini nzuri mwisho wa mwaka
*Yasisitiza nakisi katika bajeti kitu cha kawaida
*Yasema hadi sasa mambo bado shwari
*Kasi ya kukua kwa uchumi yadorora

Na Mwandishi Wetu

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetetea matumizi ya serikali na kusema si vema kupima ongezeko la matumizi  katika kipindi hiki, kwani takwimu sahihi zitapatikana Juni 2007 ili kujua kama serikali imetumia zaidi ya makadirio yake ya bajeti.

BoT ilitoa ufafanuzi huo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari juzi, baada ya gazeti la Mwananchi kuripoti hivi karibuni kuwa serikali imetumia Sh978.8 bilioni zaidi ya bajeti katika kipindi cha Juni mwaka jana hadi Februari mwaka huu.

Katika taarifa hiyo, BoT inasema ni vema kusubiri hadi mwisho wa bajeti  ya serikali Juni 2007 ili kupata uhakika kama kuna ongezeko la matumizi kuliko ilivyopagwa katika bajeti.

"Ni vema tusubiri hadi mwisho wa mwaka wa bajeti ya serikali mnamo mwezi Juni 2007 ndipo tutakapopata uhakika wa nakisi halisi ya bajeti ya serikali iliyojitokeza ikilinganishwa  na ile iliyopangwa  katika kipindi hicho," ilisema taarifa hiyo iliyotolewa na Naibu Gavana wa BoT.

Taarifa hiyo inasema kwa kawaida,  bajeti ya serikali huanza kutumika kuanzia Julai mosi ya kila mwaka na kumalizika Julai 30, na kwamba ni bora matumizi ya bajeti yakawa yanapimwa kwa mwaka husika wa fedha.

"Bajeti ya serikali inapokuwa na naksi, haimanishi kuwa serikali imetumia zaidi ya bajeti yake. Kwani inawezekana nakisi ilipangwa tokea mwanzo wa mwaka. Ni vema pia ifahamike kuwa, nakisi  ya Sh978.8 bilioni inatokana na vyanzo vya ndani tu vya mapato ya serikali," ilieleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Naibu Gavana, kama misaada toka nje ambayo ilifikia Sh801 bilioni ingeongezwa katika vyanzo vya mapato ya Serikali, nakisi ya bajeti  ya serikali kufikia Februari mwaka huu ingekuwa Sh177.3 bilioni, ikilinganishwa na nakisi ya Sh888.6 bilioni iliyopangwa katika bajeti ya serikali kwa mwaka 2006/07

"Bila ya shaka na ili kutoa taarifa sahihi ukilinganisha nakisi iliyopangwa na ile iliyofikiwa hadi Februari, bado hali ya usimamizi wa matumizi ya bajeti ni nzuri," taarifa hiyo ilisema. Hata hivyo, wakati BoT wanasema si vema kupima matumizi ya bajeti, yenyewe kila mwezi imekuwa ikipima matumizi ya serikali na bajeti iliyopangwa.

Wakati huo huo, mwandishi wetu Midraji Ibrahim, anaripoti kutoka Dodoma kuwa ukuaji wa uchumi umeporomoka kwa asilimia moja, ikilinganishwa na ukuaji halisi wa asilimia 6.8 mwaka 2005.

Makadirio  ya ukuaji kwa mwaka 2006 yalikuwa asilimia 5.9 na mwaka 2007, ilikuwa asilimia 7.3, lakini takwimu zinaonyesha ulikuwa kwa asilimia 5.8 mwaka jana.

Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Dk Juma Ngasongwa alisema, kupungua kwa ukuaji wa pato la taifa mwaka 2006, kumetokana na ukame ulioathiri uzalishaji wa chakula na umeme.

“Kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia pia kuliathiri uchumi na kupanda kwa gharama za uzalishaji na utoaji wa huduma. Ikizingatiwa sekta ya kilimo ndio inachangia sehemu kubwa ya pato la taifa, athari  ya ukame kwa uchumi wetu ilikuwa kubwa,” alisema Dk Ngasongwa.

Hata hivyo, Waziri wa Fedha, Zakia Meghji alisema tatizo la umeme lililoendelea hadi Desemba 2006, halikuwa na athari katika ukusanyaji mapato ya ndani.

Katika kupindi hicho, mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 7.3, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 4.3 mwaka 2005 na kwamba, kutokana na mvua zilizonyesha msimu huu, mavuno yake yatapungua kasi ya mfumuko wa bei.

Dk Ngasongwa alisema makusanyo ya ndani yamekuwa yakiongezeka kutoka asilimia 13.8 ya pato la taifa mwaka 2004/05 hadi asilimia 14.3 mwaka 2005/06. Katika mwaka 2006/07, mapato ya ndani yanatarajiwa kufikia asilimia 14.5 ya pato la taifa.

Alisema mahitaji makubwa ya fedha za kigeni mwaka 2006, yalitokana na kuongezeka kwa uagizaji bidhaa za mafuta kutoka nje na thamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya Marekani kushuka. Januari mwaka jana, dola moja ilibadilishwa kwa Sh1,183.4, Juni ilikuwa Sh1,250 na Novemba ilibadilishwa kwa Sh1,303.2.

Kuhusu muongozo wa bajeti ya muda wa kati 2007/08, Dk Ngasongwa alisema, unahimiza msukumo katika ukamilishaji wa miradi ya miundombinu iliyoanzishwa kwa ajili ya kuunganisha nchi.

“Nchi yetu ilipata mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za jamii...katika kutekeleza azma hii, maeneo ya elimu ya sekondari na elimu ya juu yamepewa kipaumbele maalum,” alisema Dk Ngasongwa


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.