* Tanzania inapoteza sifa za kina Ikhangaa?
Mashindano ya Flora London Marathon yamemalizika kwa wakenya kuibuka kidedea kwenye nafasi za mbio ndefu baada ya Martin Lel kumshinda mkenya mwenzie Felix Limo aliekuwa bingwa mwaka jana.
Mashindano hayo yalishirikisha wakimbiaji zaidi ya elfu thelathini ambao wengi wao ni watu wa kawaida kabisa ambao wamedhamini vyama visivyo vya kiserikali vinavyosaidia makundi ya kijamii yenye kuhitaji misaada, hufanyika kila mwaka na kudhaminiwa na kampuni ya siagi na vyakula ya Flora.
Bingwa wa mwaka huu, Martin Lel alimaliza mbio hizo za maili 26 baada ya kukimbia kwa masaa mawili, dakika saba na sekunde arobaini na moja ambapo aliwashinda kwa sekunde sita tu mshindi wa pili Ghoumri na mkenya Felix Limo. Hata hivyo mwanariadha mwingine maarufu Haile Gabresselassie wa Ethiopia alishindwa kumaliza mashindano hayo baada ya kuishiwa na pumzi akiwa amekimbia maili kumi na tisa tu.
Martin Lel alimweleza mwandishi wa habari hizi kuwa anaona ni fahari kwa Afrika nzima kwa Waafrika kushinda nafasi zote tatu za juu kwa upande wa wanaume, ''nachukulia ni fahari kwangu, kwa nchi yangu ya Kenya na pia Afrika nzima kuweza kushinda tena'' alisema.
Hata hivyo mwafrika pekee kushinda kwa upande wa wanawake alikuwa ni Gete Wami kutoka Ethiopia ambae alipata ushindi wa pili nyuma ya mchina Chunxiu Zhou aliemaliza kwa muda wa masaa mawili, dakika ishirini na moja na sekunde 45.
Hata hivyo mashindano hayo hayakuwa na mwanariadha hata mmoja kutoka Tanzania. Mbio za London Marathon ni moja ya mbio maarufu sana duniani ambazo zinaambatana na kitita cha dola laki moja kwa mshindi wa kwanza na mikataba kadhaa ya matangazo ya bidhaa za michezo. Hii inaashiria kuwa Tanzania inaelekea kupoteza sifa yake katika mchezo wa riadha ukilinganisha na miaka ya themanini enzi za kina Filbert Bayi na Juma Ikhangaa.