CHAMA cha Wananchi (CUF), na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), vimeanza kujipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Wakati CUF inakuja na mpango wa kuanzisha kituo cha televisheni na redio kwa ajili ya kurusha matangazo yake na propaganda za chama, CHADEMA inakuja na mfumo wa mabalozi kama wale wa nyumba kumi kumi.
Matangazo ya redio na televisheni ya CUF, yatakuwa yakirushwa kutoka Dar es Salaam na kwa kuanzia, yatasikika katika maeneo ya Ukanda wa Mashariki, Kati, Kusini na Zanzibar.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, alisema hayo jana wakati akitoa muhtasari wa ziara yake na Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba, nchini Taiwan.
Alisema CUF imegundua mawasiliano ya umma ni kitu muhimu, hasa kwa kuzingatia wafanyabiashara wengi bado wako nyuma katika kusaidia vyama vya upinzani kwa hofu ya kuathirika kimaslahi.
Maalim Seif alisema katika hatua ya awali, wanatarajia kurusha matangazo katika eneo la umbali wa kilometa 250 ili wanachama na wananchi waweze kufahamu sera za CUF na mikakati ya chama hicho.
Mbali na kuzungumzia kuanzisha kituo cha redio na televisheni, Maalim Seif alisema chama hicho kitatumia uzoefu wa kisiasa kutoka nchini Taiwan kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaanguka katika uchaguzi ujao.
Alisema CUF imefungua ushirikiano na chama tawala cha Taiwan DPP na kuchukua mikakati kadhaa ikiwemo ya uimarishaji chama na kufanikisha kampeni.
Maalim Seif alisema walipokuwa Taiwan kuanzaia Aprili 12, mwaka huu, alikutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia siasa, Mkurugenzi wa Taiwan anayehusika na Mambo ya Afrika na baadaye kushiriki katika semina ya kimataifa, iliyojadili hali ya kisiasa na uchumi.
Alisema CUF, kimekubaliana na Taiwan kuongeza uwezo wake katika utendaji wa shughuli za kisiasa na kubadilishana uzoefu juu ya uendeshaji wa kampeni na wabunge na wawakilishi kupata uzoefu utakaosaidia kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, alisema CUF itachukua uzoefu wa mawasiliano ya umma katika utendaji wa shughuli zake kwa kuandaa programu maalumu za mafunzo ya kisiasa yatakayojenga uwezo wa utendaji wa viongozi wa ngazi ya matawi hadi taifa.
Alisema vyama vya upinzani nchini, vinashindwa kufikia malengo ya kisiasa kutokana na kukabiliwa na matatizo kifedha na hivyo kushindwa kufanya kazi za kisiasa vijijini.
Alieleza kwamba, wafanyabiashara wengi wamekuwa wakiisaidia CCM pekee na kuviacha vyama vya upinzani kwa kuhofia maslahi yao.
“Mwenyekiti wetu wa CUF ameshaandika barua kama 1,000 kwa wafanyabiashara wakubwa, lakini hawataki kujitokeza kusaidia kwa kuhofia maslahi yao ya kibiashara kuathirika.
“CUF tumebakia tukiungwa mkono na wamachinga na wafanyabiashara wa jua kali, lakini hawa hawa wanaotupiga chenga ndio watakaokuja kubadilika na kutuunga mkono tukiingia madarakani,” alisema Maalim Seif.
Kwa upande wa CHADEMA, imesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana kuwa, inaanzisha muundo mpya utakaoiwezesha kutengeneza mtandao mpana kuanzia ngazi ya balozi, mtaa, kata hadi taifa, utakaoiwezesha kushinda uchaguzi mkuu mwaka 2010.
Utaratibu huo ambao ni matokeo ya mkutano maalumu wa Agosti 13 mwaka jana, umeanza kutumika katika majimbo matatu kama majaribio.
Majimbo hayo ni Ubungo la Dar es Salaam, linaloongozwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Vijana, David Kufulia, Jimbo la Kiteto, Manyara linaloongozwa na Katibu Mtendaji Ofisi ya Katibu Mkuu na Jimbo la Tunduru, Ravuma, linaloongozwa na Benson Kigaila ambaye ni Mkurugezi wa Mafunzo wa CHADEMA.
“Iliamuliwa kuwa badala ya kuanza mchakatao huu nchi nzima, ni vema tukaanza na majimbo matatu ya majaribio ili kupata picha kamili namna ya kutekeleza mpango huu mkubwa na wenye gharama, lakini ni muhimu sana kwa mustakabali wa demokrasia na ustawi wa taifa letu,” ilisema taarifa ya chama hicho, iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Erasto Tumbo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya kufanya majaribio katika majimbo hayo matatu, majaribio mengine yatafayika katika mikoa ya Kigoma (jimbo la mjini), likiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Shaibu Akwilombe, akishirikina na viongozi wa wilaya, kata na vijiji, Mkoa wa Rukwa katika Jimbo la Mpanda litaongozwa na kada mwandamizi wa CHADEMA ambaye hakutajwa jina katika taarifa hiyo.
Ilisema taarifa hiyo kuwa, ili kujipatia wanachama wengi, chama hicho kimedhamiria kufanya mikutano ya hadhara kwa lengo la kuwahamasisha wananchi katika mitaa, vijiji na vitongoji vyao ili kujiunga na harakati za kisiasa kupitia CHADEMA, kuimarisha mtandao wenye nguvu kuweza kuisimamia serikali iliyoko madarakani katika ngazi husika ili itimize wajibu wake.
Mtandao huo ni mkakati maalumu wa kujiandaa na uchaguzi mkuu wa 2010, ambapo chama hicho kimejiwekea malengo kufikia mwaka huo, kiwe kimeukamilisha kwa nchi nzima ili kuleta tumaini jipya katika siasa za Tanzania.
“Tunalenga kuwahamasisha Watanzania wajiunge na harakati za kisiasa kwa kuwaelimisha namna maisha yao yanavyodunishwa na maamuzi ya kisiasa na kuifanya nchi yenye utajiri kama Tanzania kuzidi kuzama katika lindi la matatizo ya umasikini. Hivyo watu safi wajiunge na CHADEMA ili kuonyesha tofauti,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.