WAKATI hali haijatulia serikalini kutokana na ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inayoonyesha ubadhirifu wa mabilioni ya shilingi, imegundulika kuwa Wizara ya Maji imeajiri wahandisi ambao wamekuwa wakipokea mishahara kwa muda wa miezi sita sasa bila kufanya kazi.
Uchunguzi wa Tanzania Daima umebaini kuwa, wahandisi hao walioajiriwa kwa ajili ya mradi wa maji vijijini kwa mkataba wa mwaka mmoja, lakini miezi sita baada ya kuajiriwa kwao, imefahamika kuwa hawajaanza kazi kwa kuwa miradi hiyo haijafikia hatua ya wao kushirikishwa.
Hata hivyo, kuna madai ya kuwepo kwa msuguano wa chini kwa chini kati ya Wizara ya Maji na ile ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kutokana na ukweli kuwa TAMISEMI tayari inao wahandisi wa maji karibu katika kila halmashauri hapa nchini.
Habari zimebainisha kuwa, TAMISEMI haikupendezwa na uamuzi wa Wizara ya Maji kuajiri wahandisi wakati wapo tayari iliowaajiri kwa ajili ya kufanya shughuli zinazohusu miradi ya maji vijijini.
Hata hivyo, Tanzania Daima imebaini kuwa, tangu Novemba mwaka jana, Wizara ya Maji ilipoajiri wahandisi hao 104 kwa mkataba wa mwaka mmoja katika mradi wa maji vijijini unaofadhailiwa na Benki ya Dunia pamoja na wahisani mbalimbali, mpaka sasa mradi huo haujaanza.
Imebakia miezi sita kabla ya muda wa mkataba huo kumalizika, lakini hakuna dalili kuwa maandalizi ya mradi yatafikia hatua ya wahandisi hao kutumika kwa kazi waliyowekeana mkataba na serikali.
“Rais wetu ana kazi kubwa, hebu fikiria kumekuwa na wahandisi walioajiriwa na TAMISEMI ambao wanalipwa, na tena wameajiriwa wengine wapya ambao nao wanalipwa, lakini mpaka sasa hawajaanza kufanya kazi yao kwa kuwa mradi wa maji bado haujaanza,” alisema mfanyakazi mmoja wa Wizara ya Maji ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Baadhi ya wafanyakazi wa wizara zote mbili waliozungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutotajwa majina yao, walihoji kwa nini Wizara ya Maji iliamua kuajiri wahandisi wengine, wakati TAMISEMI inao wahandisi wa kutosha kuifanya kazi hiyo.
“Inaonyesha kuna kamsuguano kati ya TAMISEMI na Wizara ya Maji… TAMISEMI inasema ni haki yao kuajiri, cha kushangaza Wizara ya Maji ikaajiri, tena kwa kutangaza nafasi za kazi gazetini… TAMISEMI inashangaa kwa nini wanapelekewa wahandisi wakati wao wana wahandisi wao,” alisema mfanyakazi mmoja.
Hakuna waziri aliyekuwa tayari kuelezea kinagaubana kwa nini mradi huo umechelewa kuanza, lakini alipozungumza, Waziri wa TAMISEMI, Mizengo Pinda, alikanusha kuwepo kwa msuguano kati ya wizara yake na Wizara ya Maji.
Alikiri kuwepo kwa mradi huo wa maji, lakini hakukubali wala kukanusha iwapo Wizara ya Maji imeajiri wahandisi wakati wizara yake inao wa kutosha.
Alichosisitiza ni kuwa, wizara hizo mbili zimekuwa na ushirikiano mzuri katika mradi huo na miradi mingine.
“Upo uhusiano wa karibu kati ya TAMISEMI na Wizara ya Maji. Tunajua wananchi wamekuwa wakilalamika kuhusu mradi huo kwa kuwa kuna kitu watakuwa hawajakijua kuhusiana na mradi huo,” alisema.
Kwa mujibu wa Pinda, kila wilaya imepewa miradi 10 ambayo itatekelezwa vijijini na kila kijiji kinatakiwa kuchangia asilimia 20 ya thamani ya mradi.
Alisema mradi huo unatakiwa uwe na mkandarasi atakayeuendesha, na wahisani kazi yao ni kugharamia mradi husika.
“Baadhi ya maeneo bado hakuna mkandarasi, ila kuna kazi zinazoendelea za kimya kimya ambazo naamini kuwa, kwa kuwa wananchi hawazifahamu, ndiyo maana wanaona unachelewa kwa kuwa matarajio yao ilikuwa ni kupata maji,” alisema Waziri Pinda.
Alisema kuwa baada ya muda mfupi kuanzia sasa kazi za mradi huo zitaanza kuonekana.
“Tusiwaonee watu wa maji jamani,” aliongeza.
Jitihada za kumtafuta Waziri wa Maji, Jumanne Kawambwa, kuzungumzia suala hilo zimegonga mwamba. Kila alipopigiwa simu yake ya mkononi, ilikuwa inaita bila majibu.
Ripoti ya CAG inaonyesha kuwa, wizara 27 na wakala zao sawa na asilimia 39, zilipewa hati chafu zinazoonyesha kuwapo kwa ubadhirifu wa fedha.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baadhi ya wizara zinazoongoza kuwa na matumizi mabaya na hivyo kupewa hati chafu ni pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ofisi ya Waziri mkuu na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Zinafuatiwa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Maji, Mambo ya Ndani, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na Wizara ya Nishati na Madini.