WABUNGE wamekataa uharakishwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki kwa kile walichoeleza kuwa, Tanzania haijajiandaa kushindana na nchi wanachama wa shirikisho hilo.
Wakitoa maoni yao kwa kamati ya kukusanya maoni ya muundo wa shirikisho la Afrika Mashariki jana mjini hapa, baadhi ya wabunge walionyesha hofu ya wazi kwa Tanzania kujiunga na shirikisho kutokana na nchi wanachama kuwa mbele kimaendeleo kuliko Tanzania.
Mbele ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Profesa Samweli Wangwe, wabunge hao walisema, uharakishwaji wa shirikisho hilo utaleta madhara kwa Watanzania ambao uchumi ni mdogo ukilinganisha na Kenya.
Mbunge wa Longido, Michael Laizer (CCM), alisema kabla ya kujiunga na shirikisho hilo, lazima tujiulize kilichotushinda kwenye jumuiya.
Alisema, wafugaji wa Kitanzania wanaoishi mpakani mwa Kenya na Tanzania hawaruhusiwi kupeleka ng’ombe nchini Kenya wakati wafanyabiashara wa Kenya hawana kizuizi kuleta ng’ombe wao kuwauza Tanzania.
Alisema thamani ya fedha za Kenya ni kubwa kuliko ya shilingi ya Tanzania jambo litakalosababisha matatizo kwa Watanzania kununua ama kuuza bidhaa kwenye soko la Kenya.
Naye, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Joyce Masunga, alisema kabla serikali haijaamua kuharakisha kujiunga katika shirikisho, lazima iwape nafasi Watanzania kujiuliza kama wameweza kufanikisha kwa asilimia 100 muungano kati ya Tanganyika Bara na Visiwani.
“Jamani, hivi haya tuliyonayo kuyatatua inakuwa mbinde tutaweza kweli tukiwa kwenye shirikisho, mi nadhani tujiulize ya muafaka wa CUF na CCM mbona hatujaumaliza… naomba waheshimiwa wabunge tusikubali haraka hizi, hazina baraka.
“Kazi inayofanywa na kamati hiyo chini ya Profesa Samwel Wangwe ni sawa na mwalimu kugawa mitihani ya somo ambalo hajafundisha… ni bora watu wapatiwe elimu kwanza,” alisema Masunga.
Mbunge huyo pia alisema hakuna haja ya kamati hiyo kuendelea na kazi yake kwa kuwa inatumia fedha nyingi ambazo zingefaa kusaidia wananchi katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo.
Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Mnyaa (CUF), alisema upo uwezekano kuwa haraka zinazofanywa na serikali kuhusu uharakishwaji wa shirikisho hili unatokana na nguvu za mashirika ya nje.
“Nina hofu kuwa pengine haraka hizi zinatokana na nguvu ya makampuni makubwa yanayotaka kupata faida kubwa, yameamua kuweka shinikizo katika hili kwa lengo la kutumaliza kabisa kwa niaba ya wakazi wa Mkanyageni, nasema tusiharakishe ujio wa shirikisho hili, lije hata baada ya miaka 80,” alisema Mnyaa.
Kadhalika, alisisitiza kuwa pamoja na kuangalia katika sekta ya uchumi na siasa, ni lazima tujiulize wenzetu wamejipanga vipi vilevile tuangalie baadhi ya nchi zilizowahi kuwa shirikisho na sababu ya kujitoa kwake.
Akitoa maoni yake Mbunge wa Dole, Juma Suleiman Nh’unga (CCM), alimtaka Rais Jakaya Kikwete, kusitisha majukumu ya kamati hiyo kwa kuwa hakuna sababu ya kuwaletea Watanzania shirikisho litakalowaumiza.
Akiendelea kutoa maoni yake, mbunge huyo alisema iwapo serikali italazimisha uharakishwaji wa shirikisho hilo, alishauri Zanzibar ijiunge kama nchi inayojitegemea na si sehemu ya Tanzania.
Mbunge huyo alihitimisha kwa kusema: “Namuomba Mheshimiwa Rais, asitishe mara moja shughuli za shirikisho hili maana kama tukiingia basi, Zanzibar iwe nchi inayojitegemea, isiingie kama sehemu ya Tanzania… kwanza hizo fedha zinazotumika kwenye kamati zilistahili kupelekwa kwenye majimbo kwa ajili ya miradi ya maendeleo.”
Tofauti na wabunge wengine, Chacha Wangwe, Mbunge wa Tarime (CHADEMA), alisema wananchi wa jimbo lake wanahitaji uharakishwaji wa shirikisho hilo mapema zaidi kwa kuwa wanaishi mpakani.
Wangwe, alisema wananchi wanafanya ulinganisho katika suala la ardhi kati ya Kenya, Tanzania na Uganda na kuona kuwa wakazi wa nchi jirani wanafaidi ardhi yao kwa kuwa kila mmoja anamiliki eneo lake.
“Serikali inahitaji kufanya tathimini ya ardhi kabla ya kuharakisha kuingia katika shirikisho hili… wananchi wa mpakani wanafanya ‘comparison’ kati ya nchi zinazowazunguka na kuona wapi bora zaidi,” alisema Wangwe.
Aidha, katika kikao cha Bunge kilichopita, Wangwe aliliambia Bunge kuwa atalipa kodi yake nchini Kenya ambako kuna miundombinu mizuri na huduma bora kwa wakazi wake kuliko kuitoa kodi hiyo kwa Serikali ya Tanzania.
Kamati hiyo ilimaliza kazi yake na inaendelea kukusanya maoni kwenye maeneo mengine nchini.