KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, amewatuhumu viongozi wa Serikali ya Zanzibar kuwa wanachangia visiwa hivyo kukosa haki zake ndani ya Muungano.
Amesema viongozi hao wamekuwa “wakitetereka” kisiasa hasa yanapofika maamuzi mazito yanayohusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Maalim Seif aliyasema hayo jana katika mahojiano maalumu na waandishi wa habari yaliyofanyika nyumbani kwake Mtoni, Unguja, wakati wa kuadhimisha miaka 43 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema athari za kiuchumi zinazoikumba Zanzibar zimechangiwa na viongozi kukubali kupitisha marekebisho ya 11 ya Katiba ya Muungano ya mwaka 1994, yaliyoondoa madaraka ya Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Muungano.
Maalim Seif alisema yeye binafsi alisimama imara kupinga suala hilo kwa vile nafasi hiyo ndiyo iliyokuwa kiungo katika Muungano.
Alisema kitendo cha Rais wa Zanzibar kuingia katika Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano kama waziri asiye na wizara maalum, hakileti sura nzuri katika uimarishaji wa Muungano.
Kwamba tatizo kubwa linalowakumba Wazanzibari waliopo madarakani ni kuweka mbele maslahi ya kisiasa badala ya nchi.
“Mimi binafsi nilipinga suala hili hadharani, lakini wenzangu walishindwa kuniunga mkono,” alisema.
Hata hivyo alisema Muungano umeleta faida kubwa hasa kutokana na wananchi kutumia lugha moja ya Kiswahili pamoja na kujenga udugu kati ya wananchi wa Zanzibar na wale wa Tanzania Bara.
Alisema kama Muungano usingekuwapo, Zanzibar ingekuwa katika mwelekeo mbaya wa kidemokrasia, kwa vile Rais wa Kwanza wa Zanzibar alitamka kwamba Zanzibar haitakuwa na uchaguzi hadi baada ya miaka 50.
Katibu mkuu huyo wa CUF alisema siasa za kibabe zilijitokeza sana baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964, lakini kutokana na uimara wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, viongozi walikumbushwa kuzingatia demokrasia na haki za binadamu na kuiepusha nchi kuelekea kubaya.
Alisisitiza kuwa kabla ya kero nyingine za Muungano kujadiliwa, lazima Zanzibar irejeshewe nafasi ya Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Muungano, badala ya kutumia utaratibu wa mgombea mwenza.
Maalim Seif alisema iwapo Rais wa Zanzibar atakaa meza kubwa na viongozi wenzake, atakuwa na nguvu za maamuzi badala ya kuingia kama mjumbe katika Baraza la Mawaziri.
Hata hivyo alisema kero za Muungano lazima zijadiliwe kwa uwazi, ikiwamo kushirikishwa wananchi kutoa maoni yao juu ya mfumo wa Muungano wanaoutaka.
“Serikali msijadili kero za Muungano kabla ya kupata maoni ya wananchi, kwani Wazanzibari wengi wanalalamika Zanzibar inamalizwa kiuchumi,” alisema Maalim Seif na kuongeza “maisha ya Zanzibar ni ghali kuliko ya ‘Bongo’.”
Aliutaja mfumo mbaya wa kodi kwenye sekta ya biashara Zanzibar kuwa imewaangusha wafanyabiashara wengi na baadhi wamehamia katika soko la Tanzania Bara.
Alieleza kushangazwa na Serikali ya Muungano kuweka viwango sawa vya kodi wakati kuna tofauti kubwa za kiuchumi na kutoa mfano kuwa Zanzibar inakusanya shilingi bilioni tano kwa mwezi wakati Tanzania Bara inakusanya shilingi zaidi ya bilioni 200.
Akizungumza kuhusu hali ya chama chake, alisema bado kiko imara na anaamini kuwa kitaingia madarakani wakati wowote iwapo uwanja wa demokrasia utawekwa sawa katika uchaguzi.
“Sina wasiwasi wowote…naamini iko siku CUF itakaa madarakani kwa vile ni chama chenye malengo kama yale aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere alipokuwa akipambana na Waingereza,” alisema Maalim Seif.
Akizungumzia kushindwa kwa CUF kuingia katika chaguzi kadhaa zilizopita, alisema chama chake kinashindwa kuingia madarakani kutokana na uwanja wa demokrasia kuwa mchafu, hasa serikali kutumia vyombo vya dola kusimamia maamuzi ya demokrasia.
Alitoa rai kuwa ili demokrasia ya kweli iweze kupatikana katika uwanja wa uchaguzi, wenyekiti wa Tume za Uchaguzi na makamishna wao wateuliwe na watu wanaoaminika katika jamii, badala ya kuteuliwa na Rais ambaye ni kiongozi wa chama kinachoshiriki uchaguzi.