MFANYABIASHARA maarufu wa jijini Dar es Salaam, Yusuf Manji, amesurika kufa baada ya gari lake kugonga nguzo wakati akikwepa magari ya msafara wa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.
Akizungumza na Tanzania Daima juzi ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Manji alisema ajali hiyo ilitokea mwishoni mwa mwezi uliopita, katika Barabara Sekou Toure eneo la Coco Beach.
Manji alisema ajali hiyo ilitokea ghafla wakati gari alilokuwa akiendesha likiwa katika mwendo wa kilometa 120 kwa saa, jambo lililomfanya avamie nguzo iliyo pembeni ya barabara wakati akijaribu kukwepa msafara wa magari ya Waziri Mkuu.
“Nilipata ajali katika eneo la Coco Beach, pale kwenye muinuko, unajua Jumapili huwa hakuna magari mengi, nilikuwa ‘nadrive’ mwenyewe, spidi kama 120 kwa saa, sasa wakati napanda ule mwinuko, ikatokea gari ya polisi inayoongoza msafara wa magari ya Waziri Mkuu.
“Nilijitahidi kupunguza ili nipaki pembeni, msafara huo upite, lakini bahati mbaya nikavamia nguzo ambayo sikuiona pembeni ya barabara, niliumia mkono na hapa kichwani, lakini sasa ninaendelea vizuri.
“Nimekuwa sipo ofisini kwa mwezi mzima, wiki hii ndiyo nimeanza kazi, lakini sikuwaambia watu wengi, na hata Yanga hawakujua, sikuwaambia kwa sababu sikutaka ‘wapanic’,” alisema Manji.
Akizungumzia hali ya afya yake, Manji alisema sasa ni nzuri na anaendelea na kazi zake kama kawaida baada ya kutokuwepo ofisini kwake kwa muda wa mwezi mmoja.
Miongoni mwa mambo ambayo Manji alisema anatarajia kuanza kuyafanyia kazi, ni pamoja na ubomoaji wa jengo la Salamander baada ya serikali kuliondoa katika orodha ya majengo yasiyotakiwa kubomolewa kwa vile yanalindwa na sheria ya hifadhi.
Alisema tayari amekwishapata ruhusa ya kuliendeleza eneo hilo kwa kulibomoa jengo lililopo sasa na kujenga jingine la kisasa.
Manji alilinua jengo la Salamander kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na akatangaza kuwapa notisi wapangaji waliokuwemo katika jengo hilo kuondoka kupisha ujenzi wa jengo jipya la kisasa.
Hatua hiyo ya Manji, ilizua mjadala mkali baada ya kubainika kuwa jengo hilo ni moja kati ya majengo ambayo yamo katika orodha ya hifadhi ya kale, hivyo halipaswi kubomolewa.
Vyanzo vya habari kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii vililieleza gazeti hili kuwa Ofisi ya Mambo ya Kale iliamua kupinga uamuzi huo na kukata rufaa kwa Baraza la Mawaziri ili litengue uamuzi wa kuuzwa kwa jengo hilo.
Aidha, ilielezwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe naye alichochea utata wa suala hilo baada ya kutengua uamuzi wa mtangulizi wake katika wizara hiyo, Anthony Diallo wa kuliweka jengo hilo katika orodha ya majengo ya hifadhi ya kale.
Uamuzi wa mwanzo uliochukuliwa na Diallo ulikuwa ukiyaweka katika orodha ya hifadhi ya mambo ya kale majengo na maeneo 49 jijini Dar es Salaam na 193 nchi nzima kwa ajili ya kutunza historia ya nchi.
Lakini aumuzi huo uliibua mvutano baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambayo ilipinga kuchukuliwa kwa hatua hiyo bila kushirikishwa.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilipinga hatua ya Diallo kwa maelezo kuwa amekiuka sheria kwa vile haimpi ubavu wa kufikia uamuzi huo bila kumshirikisha waziri mwenzake wa Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi.
Wizara ya Ardhi ilitumia sheria kumpinga Waziri Diallo ambaye inadaiwa kuwa, pamoja na nia yake nzuri ya kuitaka kuhifadhi historia ya nchi, lakini alipotoshwa na baadhi ya wasaidizi wake katika uamuzi alioufikia.
Upotoshwaji huo ndio uliompa nguvu Maghembe ya kubadilisha maamuzi hayo ya Diallo.
Hata hivyo, Maghembe naye alikutana na kikwazo baada ya Idara ya Mambo ya Kale kuiomba serikali kuingilia kati kuzuia uamuzi wa Prof. Maghembe wa kuruhusu kuvunjwa kwa jengo hilo.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya Idara ya Hifadhi ya Mambo ya Kale, viliieleza Tanzania Daima kuwa, uongozi wa idara hiyo uliamua kupingana na Prof. Maghembe na kuliandikia Baraza la Mawaziri, ukiliomba lizuie uvunjwaji wa jengo hilo kwa sababu athari zake ni kubwa kwa taifa.
Mmoja wa maofisa waandamizi wa idara hiyo ambaye alizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini kwa sababu si msemaji, alisema Salamander ni moja kati ya majengo yaliyohifadhiwa kisheria, hivyo kitendo cha kulivunja, ni uvunjaji sheria.
Alisema iwapo jengo hilo litavunjwa, itakuwa ni kwa sababu ya shinikizo la baadhi ya wafanyabiashara ambao wako tayari kupindisha sheria za nchi kwa maslahi yao binafsi.
Ofisa huyo alionya kuwa, iwapo Baraza la Mawaziri litabariki kupindishwa kwa sheria na jengo hilo likavunjwa, sheria haitaheshimiwa tena na utendaji kazi wa Idara ya Mambo ya Kale utakuwa mgumu kwa sababu sheria zitakuwa hazifuatwi.
Hata hivyo, uchunguzi wa kina wa gazeti hili, ulibaini kuwa maamuzi ya sasa ya Prof. Maghembe ambayo yanatofautina na ya Diallo yanatokana na nguvu aliyonayo ya kupindishwa kwa sheria iliyotumika kuyatangaza maeneo hayo kuwa katika orodha ya hifadhi.
Tanzania Daima iligundua kuwa, Mwanasheria wa Wizara ya Maliasili na Utalii alimpotosha Diallo ambaye alisaini waraka wa uhifadhi wa majengo hayo 193 hapa nchini.
Uchunguzi ulionyesha kuwa mwanasheria huyo alimshari Waziri Diallo kutumia kifungu namba 3 (2) cha sheria ya mambo ya kale iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1979 kinachosomeka kuwa:
“Waziri baada ya kujadiliana na Waziri anayehusika na mambo ya ardhi, kupitia tangazo gazetini atatangaza sehemu au jengo au eneo kuwa eneo la hifadhi.”
Sheria hii ilikuwa ikimbana Diallo kwa sababu kabla ya kuchukua uamuzi wa kutangaza kuyahifadhi majengo hayo, alipaswa kuwasiliana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhusu nia yake hiyo.
Sheria iliyopaswa kutumiwa na Diallo ni namba 3 (1) iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1979 inayoeleza kuwa, waziri kupitia gazeti la serikali atatangaza mahali au majengo yoyote yenye maslahi ya kihistoria kwa ajili ya kulindwa na sheria hii.
Mapungufu hayo ya kisheria yalitumiwa na mnunuzi wa jengo la Salamander kulalamika kwa viongozi wa juu kitaifa pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa, ambalo ndilo mmiliki wa Salamander na aliyeliuza jengo hilo, kudai kuwa hakutetendewa haki.
Uchunguzi zaidi ulibainisha kuwa, katika kuishinikiza serikali isalimu amri, mfanyabiashara huyo ambaye alinunua jengo hilo kwa sh milioni 267, alidai kuwa yupo tayari kuliachia iwapo atalipwa sh milioni 700.
Kutokana na shinikizo hilo, Idara ya Kuhifadhi Mambo ya Kale ililazimika kukubaliana na uamuzi wa Waziri Maghembe wa kuliondoa jengo katika orodha ya hifadhi, baada ya Waziri Mkuu kuhoji sheria iliyotumika na kubaini kuwa ilikosewa.
Hata hivyo ilielezwa kuwa idara hiyo iliamua kukubaliana na uamuzi wa kuliondoa jengo hilo katika orodha ya hifadhi ili kuwaridhisha baadhi ya wanasiasa waliokuwa mstari wa mbele kutetea kuvunjwa kwake.
Lakini iliamua kuliandikia Baraza la Mawaziri ili liliangalie upya suala hilo na ikaliomba lizuie kuvunjwa kwa sababu itakuwa ni aibu kwa taifa.
Mmoja wa wataalamu wa Idara ya Mambo ya Kale, alieleza kuwa shinikizo lililopo kuhusu kuvunjwa kwa jengo la Salamander ni la viongozi wa kisiasa ambao wana maslahi binafsi katika uvunjaji huo.
Alisema idara imeamua kuliandikia baraza la mawaziri na kuwatahadharisha kuhusu uwezekano wa kupotea kwa historia ya Jiji la Dar es Salaam iwapo uamuzi wa kulivunja utapitishwa.
Aliyataja baadhi ya majengo mengine ya kale yaliyohifadhiwa kuwa ni pamoja na Ikulu, Hospitali ya Ocean Road, Mahakama ya Biashara na Kanisa la Mtakarifu Joseph.
Jengo la Salamander lilijengwa mwaka 1898 kama bwalo la maofisa wa Jeshi la Ujerumani na baadaye Waingereza walikuja kulitumia kama duka kubwa la dawa.
Baada ya Tanganyika kupata uhuru, serikali ililiweka jengo hilo chini ya miliki ya Shirika la Nyumba la Taifa.