Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kikwete kitanzini
Kikwete kitanzini
By Habari Tanzania | Published  04/22/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Mwandishi Wetu


WANAFUNZI wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, wamemuingiza Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika orodha ya marais wote wanne wa Tanzania, ambao kwa zaidi ya miaka 40 wamekuwa kwa nyakati tofauti wakishindwa kukidhi matakwa ya kitaaluma ya wasomi hao.

Kuingia kwa Kikwete katika kundi la watangulizi wake watatu, kumeandika historia nyingine inayoonyesha kuwa, viongozi wakuu wote wanne, katika taifa hili katika vipindi tofauti, wamepita katika tanuru la moto mkali unaowashwa na wasomi wanaotoka katika chuo kikuu kikongwe kabisa hapa nchini, ambacho kilisajiliwa rasmi kama chuo kikuu cha taifa, Julai mosi mwaka 1970, ingawa tayari kilikuwa kimeshakuwa na hadhi hiyo tangu mwaka 1963.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, chenye historia ya migomo inayoweza kuzidi 10 tangu kuanzishwa kwake, kimerudia kile ambacho mwaka 1965, kiliongozwa na wanafunzi wa zama hizo kama akina Samuel Sitta ambaye sasa ni Spika wa Bunge na marehemu Wilfred Mwabulambo waliokuwa wakipinga kukwatwa kwa fedha zao kwa ajili ya kuchangia Jeshi la Kujenga Taifa.

Mgomo huo ambao ulikwenda sambamba na wanafunzi hao kubeba mabango yaliyokuwa yakidai kuwa ‘serikali ya kikoloni (iliyokuwa imeangushwa mwaka 1961) ilikuwa ni bora kuliko ile ya kizalendo’, ulimkera Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa Rais na Mkuu wa Chuo Kikuu hicho, hata kufikia hatua ya kuwachapa viboko baadhi ya vinara wa mgomo huo.

Mwalimu Nyerere alionja joto jingine la mgomo wa wanafunzi hao miaka sita baadaye, wakati wanafunzi katika chuo kikuu hicho, walipogoma tena kupinga kufukuzwa nchini kwa mwenzao Mkenya, aliyekuwa kiongozi wao wakati huo.

Kama hiyo haitoshi, mwaka 1978, Mwalimu alijikuta katika wakati mwingine mgumu wakati wanafunzi wa chuo hicho walipogoma wakipinga wabunge kujiongezea mshahara wakati taifa likiwa katika wakati mgumu wa vita dhidi ya aliyekuwa kiongozi wa Uganda, Idi Amin Dada.

Migomo ya zama za Mwalimu ilitokea wakati chuo kikuu hicho, kilipokuwa kikishiriki kikamilifu katika vuguvugu la hoja za zama za vita baridi, enzi hizo wasomi wengi wa hapo wakiongozwa na wahadhiri wao wanamapinduzi kama akina Walter Rodney, Wadada Nabudere, Issa Shivji na wengine wengi.

Mwenendo huo wa wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kuendelea kugoma ulipamba moto hata wakati Ali Hassan Mwinyi akiwa rais na mkubwa kati ya hiyo ni ule wa mwaka 1990 ulioilazimisha serikali kukifunga chuo hicho kwa mwaka mmoja, hatua ambayo kwa miaka mingi imeendelea kuvuruga mwenendo wa mambo chuoni hapo.

Aidha, ni katika kipindi hicho hicho cha Mwinyi, kilichokwenda na mabadiliko mengi ya kimataifa na kitaifa yakiwamo ya kumalizika kwa vita baridi na kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi, ndipo tena mwaka 1991/92 wanafunzi waligoma na serikali ikaamua kuwafukuza moja kwa moja wanafunzi 10 waliotajwa kuwa viongozi wa vurugu hizo.

Miongoni mwa wanafunzi waliofukuzwa wakati huo, ni pamoja na aliyepata kuwa Mbunge wa Kyerwa, Benedicto Mutungirehi (TLP) na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye sasa hivi ni mmoja miongoni mwa wanasiasa waliotangaza kuunga mkono wanafunzi waliosimamishwa safari hii.

Hata baada ya Mwinyi kumaliza miaka yake 10 akiwa amezozana kwa muda mrefu na wanafunzi wa chuo kikuu hicho, Benjamin Mkapa alijikuta akirithi mwenendo huo wa mambo katika kipindi chote alichokuwa rais (1995-2005).

Mchakato wa kuchangia elimu ulioanza wakati wa uongozi wa Mwinyi zama Mkapa akiwa Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, ndiyo hoja ambayo imeendelea kuwa kidonda kikuu kwa wanafunzi wa chuo hicho, uongozi wa chuo na serikali hadi hivi leo.

Miaka 13 sasa tangu kuanza kwa uchangiaji wa elimu ya juu, mizozo isiyoisha kati ya serikali na wanafunzi ambayo Kikwete ameirithi kinyume cha matakwa yake, imeendelea kuwa kitanzi kigumu kwa viongozi wakuu na Aprili 21 mwaka 2004 hali hiyo ilipata kumlazimu Mkapa kukifunga chuo kwa muda, kama ilivyotokea hivi sasa.

Miaka minne tu tangu aingie madarakani, Februari 16 mwaka 1999, Mkapa alipohutubia jumuiya ya chuo kikuu, alikiri kuhusu kuporomoka kwa ubora wa elimu ya chuo kikuu kulikochangiwa pamoja na mambo mengine, kuendelea kupungua kila mwaka kwa kasma iliyokuwa ikitengwa kwa ajili ya chuo kikuu hicho.

Akitoa takwimu, Mkapa alisema hadi wakati huo, serikali ilikuwa ikitoa shilingi 29 tu kwa kila shilingi 100 ambazo chuo hicho kilikuwa kikihitaji tofauti na ilivyokuwa mwaka 1984/85 wakati chuo kikuu hicho kilipokuwa kikipata sh 96 kwa kila sh 100 kilizoomba.

Wakati huo, Mkapa alisema, serikali ilikuwa imefikia hatua ya kukipa chuo kikuu hicho asilimia 4 tu ya mahitaji yake yote ya kibajeti kiasi ambacho alikiri ni kidogo.

Hali hiyo ambayo imeendelea kuwa mbaya kadri siku zinavyokwenda mbele, ndiyo ambayo leo hii imesababisha mwenendo wa mambo chuoni hapo kuwa mbaya na pengine kumaliza ndoto za Kikwete kuwashawishi wanafunzi vinginevyo.

Hata hivyo, tofauti na ilivyopata kuwa kwa watangulizi wake, Kikwete na wengi wa wasaidizi wake wakuu, wanaingizwa katika tanuru hilo linaloendana na tuhuma nzito na ngumu dhidi ya serikali, wao wenyewe wakiwa ni zao la chuo kikuu hicho, tofauti na ilivyokuwa kwa watangulizi wake wote watatu.

Kwa maelezo yoyote yale, Kikwete anaingia katika mtego huo akiwa hajajiandaa vya kutosha, hasa kutokana na kuingia madarakani akionekana kuungwa mkono na sehemu kubwa ya wanajumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Wiki moja kabla hajatangaza rasmi kuwa angechukua fomu ya kugombea urais, Kikwete alipata wakati mgumu kuwaeleza wanafunzi wa chuo kikuu hicho waliokuwa wamemzonga wakimtaka atoe msimamo wake mapema, wakiahidi kuwa wangemuunga mkono.

Aidha, wakati akitangaza uamuzi wake huo mwanzoni mwa 2005, Kikwete mwenyewe alisema alifikia uamuzi wa kugombea baada ya kushauriwa kufanya hivyo na makundi mbalimbali, akilitaja kundi moja kuwa ni la wasomi.

Siku za mwisho mwisho za kampeni, katika hali iliyokuwa ikionyesha kumuunga mkono kwa dhati, sehemu kubwa ya wanafunzi wa chuo kikuu hicho, waliandaliwa kikao maalum na Kikwete ambacho pamoja na kupokea kadi za uanachama wa CCM, walitamka rasmi kumuunga mkono katika harakati zake.

Uhusiano wake na wanafunzi ulianza kuingia doa taratibu, hasa baada ya mwaka jana kugoma kwa muda kabla ya kushawishiwa kurejea madarasani na Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Profesa Peter Msolla na Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo, Nimrod Mkono.

Aidha, kikao alichofanya Kikwete na wanafunzi hao mwanzoni mwa mwaka huu, siku chache baada ya kugoma kwa muda na akatoa ahadi ya kuyashughulikia madai yao ya kupinga kuchangia asilimia 40 ya gharama za elimu yao, kilifufua tena uhusiano ambao dhahiri ulianza kuonekana kuporomoka.

Uamuzi wa wanafunzi hao kuamua kugoma moja kwa moja, hata kufikia kukataa ushauri wa uongozi wa chuo chao wa kuwataka warejee masomoni, huku wakiwa wamebeba mabango ya kuikejeli serikali, kwa mara ya kwanza yalitoa ishara mbaya dhidi ya mahusiano yao na dola.

Maneno yaliyokuwa katika mabango yale, kama vile; ‘serikali ya kishikaji’, ‘tumechoshwa na ahadi hewa,’ ‘Mbowe tusaidie’ na mengine mengi, yalianza kutoa mwelekeo wa wanafunzi hao kukatishwa tamaa na serikali ambayo awali walionekana kuiunga mkono.

Mabango hayo kwa mara nyingine tena, yalihamisha madai ya kitaaluma ya wanafunzi hao na kuwa ya kisiasa, kama ilivyopata kuwa tangu mwaka 1965, ulipofanyika mgomo wa kwanza kabisa.

Mwenendo huo wa mambo ulirejesha tena historia ya wanasiasa kuweka miguu katika migomo ya wanafunzi, kama walivyopata kufanya akina Mabere Marando, Prince Bagenda, Christopher Mtikila na wengine wengi mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Uamuzi wa vyama vitatu vya upinzani vya NCCR-Mageuzi, TLP na CUF kuyaunga mkono madai ya wanafunzi waliogoma na kuipa serikali siku 21 kuwarejesha shule, ikiwa ni pamoja na kuwafutia masharti ya kuchangia asilimia 40, yameibadili kabisa hoja ya msingi ya wanafunzi hao kupinga utekelezaji wa sera ya uchangiaji wa elimu ya juu iliyoanza miaka 12 iliyopita.

Uamuzi huo hivi sasa umeingiliwa kati na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho kinapinga kuingizwa kwa masuala ya kisiasa katika madai hayo.

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa, viongozi wawili vijana wa chama hicho, John Mnyika na Kabwe Zitto ambao nao ni zao la migomo ya chuo kikuu hicho, wanawaongoza wanachama wenzao wa chama hicho katika kutafuta namna ya kumaliza mzozo kati ya wanafunzi na uongozi wa chuo kwa njia za amani.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu jana, Zitto alithibitisha kufikiwa kwa msimamo huo ndani ya chama chao na akasema kwao wao, elimu ndiyo jambo la msingi kwa wanafunzi.

Hata hivyo, Zitto alisema uamuzi wa serikali kuamua wanafunzi wachangie asilimia 40 ya gharama za elimu na ule wa kuwalipia wale tu waliopata daraja la kwanza na la pili ni wa kibaguzi na unakwenda kinyume cha Sheria Namba 9 ya mwaka 2004 iliyounda Bodi ya Mikopo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.