Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Ni kwa nini wabunge wamefunga midomo?
Ni kwa nini wabunge wamefunga midomo?
By Habari Tanzania | Published  04/21/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

LEO tunaandika suala hili kwa mara ya sita. Msimamo wetu katika hili ni bayana. Imani yetu katika maamuzi haya ni kwamba, Watanzania tumeibiwa mali na viongozi wetu walioamua kuitumia vibaya dhamana ya madaraka tuliyowapa.

Kikao cha Bunge kimemalizika mjini Dodoma jana. Wabunge wanaondoka Dodoma wakiwa wamezungumza na kupitisha maamuzi mengi tu mazito, likiwamo lile lililokuwa likisubiriwa na wengi, la Sheria ya Rushwa ambayo tumeaminishwa kukubali kuwa, itaiongezea nguvu na uhuru wa kufanya kazi, Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKURU).

Pamoja na kukiri kuwa Bunge lililoisha limeweka rekodi yake, bado tunaamini limemalizika likiwa limeacha pasipo kujadiliwa kwa baadhi ya masuala ya msingi kabisa.

Kwanza, Bunge limemalizika pasipo kuzungumzia kwa kina utata uliozingira mkataba kati ya TANESCO na Kampuni ya Richmond iliyoshindwa kuzalisha umeme wa kukodi hata kufikia hatua ya kuuza mkataba wake kwa kampuni nyingine ya Dowans.

Lakini kama hiyo haitoshi, Bunge pia kama tulivyopata kusikia siku zilizopita, limeshindwa kujadili lolote kuhusu kashfa ya ununuzi wa rada iliyonunuliwa Uingereza, japo katika hatua fulani katika kikao hiki hiki cha Bunge serikali iliwahi kutoa takwimu zilizokuwa zikionyesha namna ilivyokuwa na manufaa makubwa tangu ilipoanza kufanya kazi mwaka 2003.

Tatu na kubwa ambalo Bunge limeshindwa kujadili, ni lile linalohusu hatua ambayo serikali imefikia kuhusu marekebisho ya mikataba ya madini iliyoligharimu taifa hasara ya mamilioni kama ilivyopata kuahidiwa na Rais Jakaya Kikwete siku chache tu baada ya kuingia madarakani.

Ingawa yote hayo ni muhimu, Bunge hilo pia, limeshindwa kujadili au japo kudodosa kuhusu ulipofikia uamuzi wa serikali wa kuzirejesha baadhi ya nyumba ambazo ziliuzwa kwa viongozi wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa. Hii hasa ndiyo hoja kuu ya maoni haya.

Kwetu sisi wa Tanzania Daima, ukimya huu wa wabunge wetu, waliokuwa na fursa nyingi za kulivalia njuga suala hili, hata kama ikibidi kuandaa hoja binafsi, ni wa kukatisha tamaa.

Tunasema ni wa kukatisha tamaa kwa sababu suala hili ni moja ya mambo ambayo kwa kiwango kikubwa yalipingwa na watu wengi wakati wa utekelezwaji wake, hata kufikia hatua ya malalamiko haya kumfikia Rais Kikwete.

Mbele ya waandishi wa habari, Kikwete alilitangazia taifa hili, mwanzoni mwa Oktoba mwaka jana kuwa, tayari serikali ilikuwa imeshaanza kuchukua hatua, ambazo zitawezesha kurejeshwa kwa baadhi ya nyumba hizo za serikali alizosema ziliuzwa kwa makosa.

Ingawa tulikuwa miongoni mwa Watanzania walioipokea kauli hiyo ya Kikwete kwa mikono miwili, msimamo wetu tangu wakati huo umekuwa wazi kabisa kwamba, msamiati wa ‘baadhi ya nyumba’ unapaswa kuondolewa kabisa na badala yake urejeshwaji unapaswa kuwa wa ‘nyumba zote’ zilizouzwa.

Tunasema hivyo tukiamini kwa dhati kabisa kuwa, uamuzi mzima wa kuziuza nyumba hizo ulifanywa pasipo kuweka mbele maslahi ya taifa, na hivyo unapaswa kufutwa ili kumaliza fedheha hiyo ya kihistoria ambayo tutaendelea kuilalamikia siku nenda siku rudi.

Tunaamini unyeti wa maeneo zilikojengwa nyumba hizo, umuhimu wa nyumba zenyewe na ukweli kwamba, uongozi ni dhana ya kupokezana vijiti kama alivyopata kusema Rais Kikwete, uamuzi wowote wa kuipokonya serikali rasilimali yake muhimu, unapaswa kufutwa pasipo kuangalia matokeo ya kufanya hivyo. Tulitegemea wabunge wangeliona hili.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.