ADHABU ya kifungo cha miaka 30 jela kwa watuhumiwa wa makosa ya ujambazi wanaotumia silaha haitoshi, na serikali imeshauriwa kuangalia uwezekano wa adhabu kwa makosa hayo kuwa kifo cha kunyongwa.
Ushauri huo wa aina yake, ulitolewa jana na Mbunge wa Nungwi, Ame Pandu Ame (CCM), bungeni mjini Dodoma jana.
Ame alitoa ushauri huo ambao unaweza ukaibua ukinzani mkali wa hoja, hasa kutoka kwa watetezi wa haki za binadamu, baada ya Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, Mohamed Aboud, kujibu swali la msingi la mbunge huyo aliyetaka kufahamu nani anayevunja haki za binadamu kati ya jambazi anayeua au raia anayepambana na jambazi kwa kuliua.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Aboud, alisema: “Katika hali hiyo, mtu yeyote atakayetenda ujambazi dhidi ya mtu mwingine atakuwa amevunja sheria za nchi.”
Aboud alisema kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba, kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria.
Jibu hilo la Aboud lilitokana na swali alilouliza mbunge wa Chwaka, Yahya Kassim (CCM), aliyehoji iwapo ni halali kwa mtu kujihami dhidi ya jambazi kwa kumuua.
Aidha mbali ya hilo, Naibu Waziri Aboud alilieleza Bunge kuwa, ipo sheria ambayo inamlinda mwananchi anayejihami dhidi ya mtu anayetaka kuhujumu uhai wake.
“Ikiwa mtu amekusudia kuhujumu maisha yako, hapo una haki ya kujitetea na kunusuru kwa kumuwahi yeye kwanza kabla hajakatisha maisha yako… lakini tuangalie na mtu huyo ana nini cha kutishia uhai wako.
“Mfano anakuja kibaka anaiba chupa ya chai, huyo haina haja ya kumpiga bastola ya kichwa na kumuua… lakini litakapotokea jitu lina bastola, rungu au panga, hapo unashauriwa na wewe kujihami,” alihitimisha Aboud.