WAZIRI Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Shamsi Vuai Nahodha, amesema kwamba ujenzi wa Bandari ya Malindi utaendelea kwa kujengwa bandari ya tuta, kama ilivyokubaliwa na wafadhili na serikali.
Aliyasema hayo jana wakati akikifunga kikao cha Baraza la Wawakilishi kilichomalizika kwa mjadala mkali juu ya kukwama kwa mradi wa bandari hiyo ya Malindi, ambao ulipangwa kukamilika Novemba mwaka jana.
Mradi huo ulikwama baada ya kugundulika kuwa bandari hiyo ilikuwa imeoza kwa kiasi kikubwa na kwamba inahitaji kujengwa upya, lakini Shirika la Bandari Zanzibar lilipinga kujengwa bandari kwa mfumo wa tuta kwa madai utaleta athari kimazingira.
Nahodha alisema serikali inalazimika kukubaliana na maamuzi yaliyofikiwa, ili kuhakikisha ujenzi huo unaendelea na kuanzia sasa mjadala juu ya mfumo gani wa bandari utumike umefungwa.
“Bandari ya Malindi hali yake ni mbaya na kama tutaendelea na msimamo wa kukataa bandari ya tuta, wajenzi wanaweza kuondoka na kutuachia mashimo,” alisema Waziri Kiongozi.
Alieleza kwamba serikali inapenda ijengwe bandari ya nguzo, lakini wafadhili wanataka bandari ya tuta kutokana na gharama kubwa za ujenzi wa bandari ya mfumo wa nguzo.
Alieleza kwamba serikali ilikubali uamuzi wa kukubali ujenzi wa bandari ya tuta si kwa sababu inapenda, bali haifurahii kuona bandari hiyo inabaki katika hali ya uchakavu kama ilivyo sasa.
Kwa maana hiyo, alisema serikali haina njia nyingine ila itashirikiana na wajenzi wa mradi huo, yaani Kampuni ya Pihl kutoka Denmark, ili kuhakikisha athari za kimazingira hazitokei.
Hatua hiyo ya SMZ inakuja baada ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kupinga ujenzi wa bandari ya mfumo wa tuta kwa madai wamepokea taarifa za kitaalamu kuwa mfumo huo wa tuta utaleta athari kubwa kimazingira katika eneo hilo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mawasiliano na Ujenzi ya Baraza la Wawakilishi, Ali Suleiman aliwaambia wajumbe wenzake kuwa, serikali lazima iangalie upya mfumo wa ujenzi wa bandari ya tuta kutokana na athari zake kimazingira.
Alisema kwa mujibu wa wataalamu wa sayansi baharini ni kwamba vyombo vya abiria vitashindwa kufunga gati pamoja na meli kushindwa kushusha mizigo pale bahari inapochafuka kwa vile mawimbi yatashindwa kutawanyika.
Hadi sasa kampuni ya ujenzi ya Pihl kutoka Denmark inaidai SMZ fidia ya sh bilioni 13 kutokana na kuchelewesha mradi huo, ambao awali ulipangwa kugharimu kiasi cha sh bilioni 41.
Hata hivyo, wajumbe wa Baraza wa kambi ya upinzani walisema mradi wa ujenzi huo ulikuwa ukichechemea kutokana na baadhi ya watu kuweka maslahi mbele badala ya nchi na kushauri mikataba yote sasa iwe inakaguliwa na wajumbe wa Baraza kabla ya kufikiwa na serikali.
Habari zilizopatikana zinasema kwamba