WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, amesema kuwa lengo la serikali ni kuona kuwa elimu ya vyuo vikuu nchini inatolewa bure siku hali ya uchumi itakapotengemaa.
Lowassa aliyekuwa akizungumzia msimamo wa serikali kuhusu mgomo na hatimaye kusimamishwa masomo kwa wanafunzi wa shahada za awali wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliyasema hayo bungeni jana jioni wakati akiahirisha kikao cha Bunge.
Akikariri ahadi na dhamira ya Rais Jakaya Kikwete kwa wanafunzi hao, Lowassa alisema pamoja na yaliyotokea, nia ya serikali ni kuwawezesha wanafunzi wengi kupata elimu ya juu kwa gharama nafuu.
“Katika ahadi yake, aliyoitoa Februari 5 mwaka huu kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya CCM, Rais Kikwete alisema hakuna mwanafunzi atakayekosa elimu ya juu kutokana na umasikini wa wazazi wake.
“Ahadi hiyo imeleta kadhia kwa wanafuzni hao ambao walitaka serikali kuwaondolea gharama ya asilimia 40 ya mkopo wanayotakiwa kulipa baada ya serikali kukubali kuwakopesha asilimia 60 kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu.
“Hata hivyo, utekelezaji wa ahadi hiyo haujafanyika hali inayosababisha baadhi ya wanafunzi hao kugoma kuingia darasani kutokana na ukosefu wa fedha,” alisema Waziri Mkuu.
Mwanzoni mwa wiki hii, wanafunzi wa shahada za awali katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani (UDSM) na wale wa vyuo vikuu vishiriki vya Usanifu wa Majengo (UCLAS), Chuo cha Ualimu Chang’ombe (DUCE), Chuo cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUCHS) na Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC), walifanya mgomo kushinikiza serikali iwalipie asilimia 100 ya ada kwa ajili ya masomo yao.
Akielezea uamuzi huo wa wanafunzi, Lowassa alisema kuwa walikosa subira juu ya ahadi iliyotolewa na Rais Kikwete ya kuwalipia asilimia 100 ya ada wanafunzi wasio na uwezo wa kufanya hivyo.
“Serikali ilitegemea wanafunzi wa vyuo vikuu kuwa na subira kwa ajili ya ahadi yenye nia ya kutekelezwa, lakini kutokana na hali hiyo ya vurugu iliyojitokeza, uamuzi wa viongozi wa chuo kuwasimamisha masomo wanafunzi hao ni sahihi kabisa… serikali inalifanyia kazi suala hilo kwa kuzingatia hali ya fedha na mpango wa bajeti ya mwaka 2007/2008,” alisema Lowassa.
Waziri Mkuu alisema uongozi wa chuo ulilazimika kukifunga baada ya kuona viashiria vya kuzuka kwa vurugu kwenye vyuo hivyo, uamuzi ambao serikali inauunga mkono.
Aliendelea kulihutubia Bunge kuhusu mgomo huo na kusema, uongozi wa chuo uliamua kulegeza masharti ya ulipaji wa asilimia 40 ili kuwawezesha wanafunzi hao kuendelea na masomo, kujadili na kuona jinsi ya kupunguza gharama za mafunzo kwa vitendo kwa kuwapanga katika maeneo jirani.
Alisema kuhusu gharama za matibabu ambazo ni sh 100,000 kwa kila mwanafunzi, chuo kilikubali kusitisha uchangiaji wa fedha hizo hadi hapo baadaye, lakini kwa hivi sasa kinachukua hatua za haraka za kurejesha hali ya kawaida katika vyuo hivyo.
Siku moja baada ya mgomo huo, Jumanne wiki hii, Baraza la UDSM lilitangaza kuwasimamisha masomo kwa muda usiojulikana, wanafunzi wa shahada za awali waliosababisha kusimama kwa taratibu za masomo na kazi chuoni hapo.
Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Professa Rwekaza Mukandala, karibu sh milioni 100 hupotea kwa siku kutokana na migomo ya wanafunzi.
Baada ya kusimamishwa masomo kwa wanafunzi hao,baadhi ya wanasiasa wa upinzani waliipa serikali siku 21 ili kuwarejesha wanafunzi hao vyuoni na kutoa ufadhili wa ada zao kwa asilimia 100 na wakasema kuwa, iwapo itashindikana, watachukua hatua za kisiasa na kisheria.
Wanasiasa hao walisema watawahamasisha wananchi kote nchini, kuandamana na kugoma ili serikali itambue kuwa inaendesha nchi kwa shinikizo na si kwa ridhaa ya wananchi.
Siku mbili baada ya uongozi wa chuo kuwasimamisha masomo, ulitoa masharti magumu tisa ambayo wanafunzi hao watapaswa kuyatimiza ili waweze kurejea na kuendelea na masomo yao.
Wakati huohuo, Shabani Matutu anaripoti kuwa; viongozi wa vyama vya upinzani Tanzania Labour (TLP) na Chama cha Wananchi (CUF), wamepinga masharti yaliyotolewa na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ya kuwataka wanafunzi warudi wakiwa wamemaliza madeni kwa wale wanaodaiwa na kusema kuwa kauli hiyo haikidhi madai ya msingi.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti, viongozi hao walipinga masharti hayo na kusema kuwa bado serikali haijajitosheleza kwa kutatua madai yao ya msingi huku wakisisitiza kuwa madai yao ya kuifungulia serikali mashtaka iwapo hawatawaondolea asilimia 40 ni ya msingi.
Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema alisema kuwa wao hawapo tayari kufuta tamko lao la kutoa siku 21 kwa serikali ya kuhakikisha wanawarudisha wanafunzi hao ikiwa ni pamoja na kuwaondolea kikwazo cha malipo ya asilimia 40 na kuwaongezea fedha ya mazoezi ya vitendo.
“Tutasimama kidete kuhakikisha elimu ya juu haiaribiwi na serikali hii, kwani njama za kuiharibu tumegundua, njama zao hizo za kutaka kuwaondoa watoto wa maskini ili wawape elimu watoto wa matajiri,” alisema Mrema.
Aliiponda kauli hiyo kwa kusema ni kauli ya kujikosha, kwani haina msingi ambao utaweza kusababisha kuachana na uamuzi wetu wa kutoa siku 21 na tumedhamiria kwenda mahakamani kwa nia ya kuinusuru elimu ya juu.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Alfred Lwakatare pia ameipinga kauli hiyo ya serikali na kudai kwamba haikidhi madai ya msingi na badala yake imeongeza ugumu zaidi.
“Kauli hiyo ameitoa kwa makusudi ili kuwapa nafasi watoto wa matajiri huku wakiwaacha watoto wa walalahoi wakikosa elimu ya juu, kwani wameamua kuwaambia warudi na asilimia 40 ili wakikosa warudi nyumbani na wawaachie nafasi wenye uwezo, sisi hatutaki Tanzania ifike huko,” alisema Lwakatare.
Alisema kuwa hivi sasa si muda wa kuwapatia masharti ya kurudi chuoni na badala yake wangerudishwa bila masharti yoyote ambapo wangeamua kuachana na maandamano hayo.
Waziri Mkuu wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho (DARUSO), Mtatiro Julius, alisema kuwa jana walikuwa katika kikao ambacho watatoa tamko lao leo baada ya kupitisha maazimio ya Bunge lao.