Na Midraji Ibrahim, Dodoma
KAMATI ndogo ya Bunge ya Fedha na Uchumi, imemeuosha mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji na Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF), baada ya kuridhika na thamani ya jengo la Quality Plaza na taratibu zilizofuatwa katika kuuziana.
Hata hivyo, licha ya kamati hiyo kuridhika na masuala mbalimbali, kuna baadhi ya masuala ambayo yametiliwa shaka kwa sababu hayakutimizwa, ingawa imebaini kuwa jengo hilo lilinunuliwa kwa Sh36 bilioni, tofauti na tetesi ambazo zimekuwepo za kununuliwa Sh60 bilioni.
“Kamati baada ya kuangalia mchakato mzima wa ununuzi wa Quality Plaza Ltd, iliridhika kuwa kilichonunuliwa ni jengo lenye hati tisa kati ya 11 na sio hisa,” kamati hiyo ilisema na kuongeza:
“Kamati imebaini kuwa pamoja na kwamba jengo la Quality Plaza Ltd liliuzwa likiwa na wapangaji asilimia 100 kwa mujibu wa mkataba, upo umuhimu wa kuandaa mikakati ya kupata wapangaji wengine kabla ya muda wa mkataba huo kumalizika.”
Kamati hiyo, chini ya Mwenyekiti wake, Elisa Mollel, iliundwa baada ya Kamati ya Kudumu ya Fedha na Uchumi, kutaka kupata ukweli juu ya ununuzi wa jengo hilo ambalo ulizua malalamiko mengi.
Mojawapo ya hadidu za rejea ilikuwa ni kubainisha thamani ya jengo hilo kabla na baada ya kuuzwa, kama kweli wamiliki wa Quality Plaza waliuza asilimia 100 na sababu za PSPF kununua asilimia 100, tofauti na kawaida yao ya uwekezaji shirikishi.
Zingine ni kubainisha mgawanyo wa hisa za Quality Plaza Ltd kabla na baada ya uwekezaji wa PSPF, iwapo njia za kuwapata wathamini wa jengo zilikuwa sahihi na kama utaratibu wa zabuni ulifuatwa.
Taarifa hiyo ambayo iliwasilishwa jana bungeni ilisema, kamati iliridhika kuwa uwekezaji huo ulilenga kununua jengo badala ya hisa kama ilivyoainishwa kwenye ripoti mbili za tathmini ya jengo, tofauti na taarifa ya PSPF ambayo walionyesha kuwa walinunua hisa.
Kamati hiyo ilibaini kuwa hakuna fedha zilizolipwa katika Kampuni ya Quality Plaza Ltd wakati wa ongezeko la mtaji, kutoka Sh30 bilioni hadi Sh36 bilioni, kama azimio la wakurugenzi wa Quality Plaza lilivyokusudia Oktoba 24, 2004.
“Ripoti ya mtathimi wa serikali ilionyesha thamani ya jengo kwa utaratibu wa income approach ni dola za Marekani 37 milioni na replacement cost approach ni dola za Marekani 32 milioni. Ripoti ya mtathmini binafsi ilionyesha kuwa mapato ni dola za Marekani 38.5 milioni na gharama za marekebisho ni dola za Marekani 32.5 milioni,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Inasema kutokana na kodi ya pango, PSPF inapata dola za Marekani 173,789.5 kwa mwezi ambazo ni sawa na dola 2,085,474 kwa mwaka.
Kamati hiyo pia ilibaini kuwa wamiliki wa Quality Plaza waliuza asilimia 100 ya asilimia 95, kama hati mbili za hisa, kati ya 11 za jengo hilo zinavyoonyesha.