Kidole chaelekezwa kwa serikali ya chuo Na Waandishi Wetu
UONGOZI wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam umeanza mchakato wa kutafuta viongozi wa mgomo, huku ikionekana wazi kunuia kuwachukulia hatua viongozi wa Serikali ya Wanafunzi (Daruso-Mlimani) kwa tuhuma za kuhusika moja kwa moja kuchochea mgomo huo.
Taarifa iliyotolewa jana na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, ilisema hatua ya kuwasimamisha wanafunzi ni ya muda, ili kutoa nafasi kwa uongozi wa chuo kuchunguza vinara wa mgomo huo, kisha kuwachukulia hatua zinazostahili.
"Tumesikitishwa sana na tabia hii isiyofaa ya wanafunzi iliyosababisha hasara kwa chuo na taifa na imetushangaza kwamba ni kwa nini wanafunzi wametumia njia hiyo wakati wanajua kabisa kwamba kuna njia za kistaarabu zaidi za kushughulikia matatizo hayo, " imesema taaifa hiyo
Hata hivyo, taarifa hiyo imeushutumu moja kwa moja uongozi wa Serikali ya wanafunzi ya chuo hicho (Daruso-Mlimani), kuwa watuhumiwa namba moja hasa Rais na Waziri Mkuu wa Daruso.
Kufuatia mgomo huo Baraza Kuu la Chuo hicho April 17 liliwasimamisha masomo wanafunzi wote wa shahada ya kwanza wa chuo hicho, katika kampasi zake za mlimani, Chuo Kikuu kishiriki cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC), Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi na Usanifu Majengo (UCLAS), Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa (MUCE) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu (DUCE).
Makamu Mkuu huyo alisema kabla ya kutokea hali tete chuoni hapo, yeye binafsi na manaibu wake walifanya jitihada kutafuta suluhu, lakini hawakupewa ushirikiano na uongozi wa Daruso.
Alisema pamoja na mambo mengine, uogozi wake uliunda kamati ya pamoja kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo, hasa juu ya kupunguzwa kwa asilimia 40 ya fedha za mafunzo kwa vitendo, lakini kabla kamati hiyo haijaanza kazi viongozi wa Daruso walijitoa hivyo kuifanya kamati kushindwa kufanya kazi.
Profesa Mkandala alisema kimsingi uongozi wa chuo haustahili lawama, kwani umekuwa ukifanya kazi kwa kutekeleza maamuzi ya Serikali iliyoweka kiwango cha mkopo wa ada na mafunzo kwa vitendo wa asilimia 60 kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza.
Alisema wanafunzi wote waliojiunga mwaka huu wa masomo wanaopata mikopo yao chini ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), walitakiwa kujilipia asilimia 40 iliyobaki na wanaoendelea wakipewa asilimia 100 ya mikopo.
Alisema hata alipokutana na wanafunzi hao Ferubruari 3, mwaka huu katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Rais Jakaya Kikwete, alieleza wazi kwamba Serikali inatafuta namna ya kutatua tatizo hilo, lakini wasitegemee kutatuliwa katika kipindi cha mwaka huu wa fedha.
Profesa Mkandala alieleza kwamba baada ya kusikia vuguvugu la wanafunzi kutaka kugoma Aprili 10, mwaka huu alifanya kikao na Waziri Mkuu wa Daruso, Waziri wa Mikopo, Waziri wa Taaluma na Waziri wa Fedha, kisha kukutana na baraza zima la Mawaziri April 14.
Taarifa hiyo ilieleza kwamba, pia Aprili 13, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia alikutana na viongozi hao wa wanafunzi kuwasihi kuwa wavumilivu wakati serikali inashughulikia suala hilo, lakini kikao hicho hakikuzaa matunda.
Alisema awali viongozi hao wa Daruso badala ya kuwatuliza wenzao, ilipofika usiku wa Aprili 14 wakaitisha Bunge lao na kutoa azimio kumtaka Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kutoa tamko juu ya suala hilo ndani ya siku mbili.
Makamu Mkuu wa Chuo alisema pamoja na jitihada za uongozi kukutana na wawakilishi wa wanafunzi likiwamo Bunge lao, viongozi waandamizi walipuuza na badala yake wakahamasisha mgomo na kutishia kuwashughulikia watakaokaidi.
Taarifa hiyo ilidai kwamba Aprili 16, asubuhi viongozi hao waliwapitia wanafunzi na wahadhiri madarasani katika sehemu ya Mlimani kisha kuendelea katika kampasi nyingine za Ijmc, Duce, Muce na Uclas kuwahamasiha kugoma.
Profesa Mkandala alieleza kwamba uongozi wa chuo utaendelea kuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau wengine katika kutafuta njia bora ya ulipiaji gharama za elimu ya juu.
Waziri Mkuu wa Daruso Mlimani, Julius Mtatiro, alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya taarifa hiyo alisema kwamba tayari wameshaitisha kikao cha viongozi kuijadili.
"Sisi ni viongozi, kwa hivyo kushutumiwa ni jambo la kawaida, tumepanga kukaa kuijadili na tutaitolea tamko baadaye," alisema Waziri Mkuu huyo.
Kama ilivyo kwa wanafunzi wa chuo hicho, pia wenzao wa shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) waligoma na kusimamishwa masomo juzi.
Mbali na ahadi za mara kwa mara za Serikali kuhusu azima yake ya kuboresha elimu ya juu, kumekuwa na mfululizo wa matatizo katika kutoa mikopo na kuwafanya wanafunzi kugoma na kuandamana mara kwa mara.
Historia inaonesha kwamba mwaka 1990 viongozi na wanafunzi kadhaa wa UDSM walisimamishwa kisha wengine kufukuzwa kabisa wakidaiwa kuongoza mgomo huo. Pia kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya kuadhibiwa viongozi wa wanafunzi wakati wa migomo.
Kutoka Irimga, Hakimu Mwafongo anaripoti kwamba wanafunzi 1,500 wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Mkwawa (MuCE) wameonekana wakihaha mjini Iringa baada ya kutimuliwa chuoni
hapo.
Wanafunzi hao walionekana kuzagaa mjini wakilalamika kuwa hawana fedha za nauli ili waweze kurudi kwao, hasa wale wanaotoka nje ya mji wa Iringa.
Baadhi yao wamelazimika kuuza vitu vyao ikiwemo simu za mikononi, mabegi ya nguo na nguo ili wapate nauli na fedha kwa ajili ya kulala katika
nyumba za wageni siku waliyotimuliwa.
Katika jiji la Dar es Salaam, baadhi ya wanafunzi wameonekana wakiwa katika mitaa ya Sinza wakirandaranda kwenye makundi, ambapo wengi wao walisema hawana nauli ya kurejea mwakao na kwamba wanaishi kwa jamaa na kwa wanafunzi ambao wazazi wao wanaishi Dar es Salaam.