MBUNGE wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe (CCM), ametahadharisha kuwa Tanzania inaweza ikajikuta inaongozwa na kundi la watu walioghushi viwango vya elimu, maarufu kwa jina la vihiyo, iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa kudhibiti wimbi la vyeti bandia.
Akizungumza wakati wa mjadala wa Ripoti ya Kamati ya Mambo ya Nje ya mwaka 2006, iliyowasilishwa bungeni juzi, Dk. Mwakyembe alisema kuwa, Tanzania inapaswa kuchukua hatua kudhibiti vyeti hivyo la sivyo, nchi itapelekwa pabaya.
Dk. Mwakyembe, alitoa tahadhari hiyo kufuatia kuwepo kwa wito unaoitaka Tanzania kuboresha viwango vya elimu katika sekta mbalimbali, hasa ufundi, lugha na maadili ya kazi ili kuongeza ushindani katika soko la ajira.
Baada ya kunukuu sehemu ya taarifa hiyo, Dk. Mwakyembe alisema Watanzania wengi wamelewa sifa za kuitwa maprofesa au madaktari, wakati vyeti vyao havistahili waitwe hivyo.
“Hivi vyeti feki vinapatikana kwenye vyuo vikuu vyetu na hata baadhi ya wahadhiri wanavyo… tusipokuwa makini nchi hii itakuja kuongozwa na ‘vihiyo’, ni lazima tuwe makini katika hili,” alisema Dk. Mwakyembe bila kumung’unya maneno.
Aidha, alibainisha chuki yake dhidi ya kitendo cha kuwavisha watoto wa chekechea majoho wakati wa kuhitimu na kusema hali hiyo itawafanya kudharau elimu ya juu.
“Kumvisha mtoto wa chekechea joho ni utamaduni wa kilimbukeni, enzi zetu joho huvaliwa na msomi aliyehitimu shahada, hivyo ilimtamanisha mtoto kusoma hadi kufikia elimu ya juu.
“Joho ni nguo ya kisomi, tena inavaliwa wakati wa kupongezwa baada ya kuhitimu na kufaulu vizuri, sasa Watanzania wamegeuza… mtoto akivikwa joho anapomaliza chekechea anatosheka na kuona hakuna haja ya kuendelea kwa kuwa ameshapongezwa,” alisema kwa ukali Dk. Mwakyembe.
Akiwasilisha taarifa hiyo, mwenyekiti wa kamati hiyo, Anna Abdallah, alisema kuwa upo wasiwasi katika soko la ajira na kuna uwezekano mkubwa kwa nafasi nyeti nchini kuchukuliwa na wageni.
Naye Beatrice Shelukindo (Kilindi-CCM) aliungana na kilio cha watu wengi kuhusu uteuzi wa watendaji kadhaa.
Lakini alielekeza mchango wake katika uteuzi wa mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchi za nje na kutaka Bunge lihusishwe kwa namna fulani katika uteuzi huo.
Shelukindo alitaka majina ya watu watakaoteuliwa kuwa mabalozi, yapitishwe aidha bungeni moja kwa moja, au katika kamati husika, ili yajadiliwe kabla ya kuthibitishwa.
“Wakati mwingine uteuzi wa mabalozi hauzingatii sifa wala vigezo, hali inayofanya kumteua mtu asiye na uwezo kiutendaji na hata elimu yake kuwa ndogo.
“Kama vile haitoishi, anaweza kuteuliwa mstaafu au mtumishi aliyevurunda hapa nchini, anapelekwa nje kama balozi… wapo waliobobea kwenye nafasi hizo, nashauri pia uwepo umri wa kustaafu,” alisema Shelukindo.
Katika mchango wake, Charles Kajege (Mwibara-CCM), alitaka serikali kufanya mchakato wa kupata hatimiliki ya majengo ya ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji ili kuwa na uhakika nayo.
Aidha, baadhi ya wabunge walishauri kuongezewa nguvu kwa balozi za Tanzania nje ya nchi ili kuleta ufanisi na kutekeleza diplomasia ya kiuchumi.
Wabunge hao walitoa mfano wa ubalozi wa Tanzania mjini Geneva, Uswisi, kuwa una maofisa watano hali inayokwamisha utendaji ikilinganishwa na nchi nyingine zenye idadi kubwa ya maofisa katika balozi zake.
Baada ya wabunge mbalimbali kuwasilisha hoja zao, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Seif Iddi, alisema wizara yake itazingatia mapendekezo yaliyotolewa.
Kuhusu hatimiliki ya majengo ya ubalozi huko Msumbiji, alisema serikali inaendelea kufuatilia jambo hilo na itatoa taarifa baada ya kukamilika.
Alisema kuwa, uhaba wa fedha ndio unakwamisha mipango mingi ya serikali na kuahidi kuongeza idadi ya maofisa, hususan wenye utaalamu wa kutosha wa masuala ya uchumi na biashara kwa ajili ya ubalozi wa mjini Geneva.