Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Serikali yapewa siku 21 kuwarejesha wanafunzi
Serikali yapewa siku 21 kuwarejesha wanafunzi
By Habari Tanzania | Published  04/19/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Agnes Mlundachuma


SAKATA la mgomo wa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, limechukua sura mpya siku moja baada ya Baraza la Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwasimamisha masomo wanafunzi hao kwa muda usiojulikana.

Sasa, wanasiasa wameingia katika suala hilo, wakiwaunga mkono wanafunzi hao waliogoma na kuipa serikali siku 21 kuwarejesha shuleni haraka.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, viongozi wa vyama vitatu vya upinzani, waliitaka serikali kuhakikisha inawapa wanafunzi hao ufadhili wa asilimia 100 wa masomo.

Iwapo serikali itashindwa kufanya hivyo katika kipindi cha siku 21, viongozi hao walitishia kuchukua kile walichokiita, hatua za kisiasa na kisheria.

Tamko hilo limetolewa kwa pamoja na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Tanzania Labour (TLP), kupitia mkutano wao na waandishi wa habari, uliofanyika jana kwenye ofisi za makao makuu ya NCCR, jijini Dar es Salaam.

Tamko hilo la wenyeviti wa taifa wa vyama hivyo, lilisomwa na James Mbatia ambaye pia alimwakilisha, Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema wakati, Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF aliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wake, Wilfred Lwakatare.

Akisoma tamko hilo, Mbatia ambaye naye alipata kufukuzwa moja kwa moja Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kwa sababu ya mgomo, alisema kuwa, wakiwa Watanzania wanaipa serikali siku 21 iwarejeshe wanafunzi hao masomoni bila masharti na itekeleze madai yao yote mara moja.

Alisema kuwa, hatua ya kisiasa ndio watakayoitumia zaidi kwa kuhamasisha wananchi kote nchini kugoma na kuandamana ili serikali itambue kuwa inaendesha nchi kwa shinikizo na si kwa ridhaa ya wananchi.

“Tutawahamasisha wananchi nchini kote waunge mkono ili haki zao zisichezewe na wachache kwa kuwa elimu ni haki ya msingi na kikatiba na ndio uhai wa nchi.

“Kinachoendelea hapa nchini ni kitu cha kusikitisha sana kwa kuwa ni wanafunzi hawa hawa ambao wengi wao walishindwa kulipa karo ya sh 70,000 wakiwa shule za sekondari, watapata wapi sh 500,000 sasa, wakati wanatoka katika familia zilizo katikati ya lindi la umaskini?” alihoji Mbatia.

Alisema kitendo hicho cha wanafunzi kugoma kinaonyesha wazi kuchoka kwao kupelekwa kama kondoo kwa kudanganywa na ubwabwa, soda, fulana na kapelo zenye rangi ya kijani na tatizo la maprofesa kujikomba kwa wanasiasa hali inayofanya taaluma kuwa siasa.

Aidha, kwa niaba ya viongozi wenzake, Mbatia alimuomba Rais Jakaya Kikwete atimize ahadi yake ambayo aliitoa wakati akiwapa wanafunzi wa vyuo vikuu kadi za UVCCM, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Februari mwaka huu.

Alimtaka Kikwete aache kile alichokiita usanii na ujanja ujanja katika kuongoza nchi.

Alisema kitendo cha kufukuza wanafunzi hao kinatisha kwa kuwa rais aliwaahidi wanafunzi hao wakati alipowapa kadi za kujiunga na UVCCM kuwa, hakuna mwanafunzi kutoka familia maskini ambaye atafukuzwa chuo kwa kushindwa kulipa asilimia 40.

“Lakini cha ajabu, kama si kichekesho, wanafunzi hao wamefanyiwa kitendo cha kinyama cha kupewa saa moja kutoonekana eneo la chuo... waende wapi usiku huo?” alihoji.

Akinukuu taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, alisema serikali kwa muda mfupi tu imeweza kutumia kiasi cha sh bilioni 978 kwa ubadhirifu na kushindwa kuwapa wanafunzi fedha wanazodai ambazo hazifiki hata sh bilioni 50.

Alisema serikali inakiuka katiba kwa kuwa suala ambalo wanataka wanafunzi hao si la hisani, bali ni la lazima kwa kuwa tamko la ulimwengu la haki za binadamu, linasema kila mtu ana haki ya kupata elimu.

“Kwa hiyo, kitendo cha kuwafukuza wanafunzi hao, kinaonyesha kuwa serikali haipo makini katika kupanga na kuchagua maamuzi na hicho ni kifo cha taifa,” aliongeza na kusisitiza kuwa, kigezo kikubwa cha kupima utaifa ni elimu.

Aliongeza kuwa, kufungwa kwa chuo kikuu kunafundisha kuwa baadhi ya wahadhiri waliokabidhiwa kuongoza vyuo vikuu nao wamechoka kifikra, na wameridhia kutokana na hasira yao inayotokana na mishahara midogo ambayo wanapewa.

Naye mwanasheria wa siku nyingi aliyepata kuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dk. Sengondo Mvungi, alisema wanafunzi hao hawakutakiwa kufukuzwa kwa kuwa sheria inasema kuwa mwanafunzi atafukuzwa iwapo tu, atagoma, kukataa kuzungumza na kufanya uharibifu wa mali.

“Lakini wanafunzi hao walikuwa tayari kuzungumza, hivyo walipaswa kusikilizwa… kugoma ni haki yao na kitendo cha wanafunzi hao kugoma kimeonyesha ni jinsi gani walivyo wasomi, kwani msomi yeyote ambaye anafundishwa na mhadhiri makini, hawezi kupelekeshwa kama kondoo kwa kukubali kila kitu,” alisema Dk. Mvungi.

Dk. Mvungi ambaye ni mwanasheria wa NCCR-Mageuzi, alisema iwapo wanafunzi hao wangekaa na kukubaliana na mambo wanayotendewa, wasingekuwa na sifa ya usomi.

Hata hivyo, alisema kilichotakiwa ni watawala kufikiria mara mbili juu ya mgomo huo na si kuwafukuza kwani hicho ni kitendo cha aibu ambacho hata yeye kinamfanya aone aibu kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Abdallah na Jackson from Mbeya)
    Rating
    SERIKALI YA AWAMU YA NNE YA TZ IMEJAA USANII NA U JUU JUU TU. HAINA UKOMAVU.
    Tunaomba tuliweke suala hili wazi kabisa machoni pa watanzania wote.Kiujumla watanzania walimchagua Kikwete bila kumjua.Hii ni brunder kubwa ambayo ilifanywa na watanzania 2005.Serikali hii inaendeshwa KISHIKAJI TUU. It is the most unprinciple government since independence. Ni serikali inayopenda kujipatia SIFA bila kuzingatia ufanisi.Lazima watanzania wote tuungane tuitoe 2010. Tunachoomba vyama vya upinzani waungane na kupanga namna watakavyogawana madaraka katika serikali mpya watakayoiunda 2010.Ikulu na ofisi ya waziri mkuu ni moja ya ofisi zenye matumizi mengi kupindukia. Kwa nini wanashindwa KUWAKOPESHA WANAFUNZI PESA KIDOGO KAMA HIZO, WAKATI WAO WAMEFUJA BILIONI KARIBIA 1000 kwa muda wa miaka miwili tuu! kIKWETE AND lOWASA ARE NOT TANZANIANS THAT IS WHY THEY ARE NOT SERIOUS IN DEALING WITH DELICATE ISSUES FACING THE COUNTRY. These are professional thieves.They must go home on 2010.We call upon opposition parties to make a memorandum of Understanding(MoU)so as to have one candidate whether it is Lipumba, Mbatia, Mrema, that we dont care. what we need is to remove CCM from power.
    The current government is less concerned with priorities in dealing with problems facing people. What is REAL MADRID to a poor mwananchi of Ndongosi or Karatu? But the government is spending billions for such a stupid thing! Kikwete ni mtu munafiki sana mwenye ahadi za za uongo ambazo inabidi amuahidie mke wake na familia yake, siyo kuwadanganya wa wananchi wa TZ kama watoto wake.
     
  • Comment #2 (Posted by John)
    Rating
    Hapo bwana umesema ukweli na kutoa akili mpya. The only way to remove CCM is for the opposition parties tounite in 2010. Kikwete and his corrupt government must be voted out. We are tyred with the leadership of these thieves. Watanzania lazima tufungue macho, wasomi twende vijijini tukahamasishe watu juu ya mkakati wa kuiondoa CCM 2010.
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.