Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Polisi vyeo kama JWTZ
Polisi vyeo kama JWTZ
By Habari Tanzania | Published  04/18/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Happiness Katabazi


JESHI la Polisi limefanya mabadiliko ya nembo za vyeo za maofisa wake wa juu vinavyovaliwa mabegani, kwa kuanza kutumia mfumo ambao kwa kiwango kikubwa unafanana na ule wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), imebainika.

Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima umebaini kuwa, mabadiliko hayo yalianza rasmi nchini kote Aprili mosi mwaka huu, kutokana na agizo la Mkuu wa Jeshi hilo Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema.

Habari ambazo gazeti hili limezipata kutoka ndani ya jeshi hilo zinaeleza kuwa, mabadiliko ya nembo za vyeo yameanzia kwa maofisa wenye cheo cha Mrakibu wa Polisi (SP) hadi IGP.

Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa, mabadiliko hayo hayatawagusa askari wasio na kamisheni, wenye vyeo vya chini na kati kama vile makoplo, masajenti na warakibu wasaidizi (ASP).

Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina kwa kuwa si wasemaji rasmi wa jeshi hilo, baadhi ya maofisa waandamizi wa polisi, waliithibitishia Tanzania Daima kuwako mabadiliko hayo.

Walisema mabadiliko ya nembo hizo za vyeo, ni moja ya mchakato wa maboresho katika Jeshi la Polisi na kulifanya lichukue sura halisi ya kijeshi kama ilivyo katika mataifa mengi mengine duniani.

Kwa mujibu wa maofisa wa jeshi hilo, pamoja na mabadiliko hayo ya nembo kufanana kwa kiwango kikubwa na zile za Jeshi la Wananchi, majina ya vyeo vya maofisa hao wa polisi yataendelea kuwa yaleyale ya awali.

“Lengo la mabadiliko haya ni maboresho… mchakato wa maboresho katika jeshi letu... hivyo wananchi wasiogope kuona maofisa wa jeshi hili kuwa na nembo tofauti kwa kuwa nembo hizo nyingine zilizobadilishwa zinafanana na zile za JWTZ,” alisema ofisa mmoja mwandamizi wa jeshi hilo.

Uchunguzi wa Tanzania Daima umeonyesha kuwa, baada ya mabadiliko hayo, nembo ya cheo cha Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) itakuwa ni ngao ya taifa, nyota moja na kitala.

Aidha, maofisa wa cheo cha kamishna (CP), wao watavaa nembo yenye ngao ya taifa na kitala, pasipo kuwa na nyota, huku manaibu kamishna (ACP) nembo yao ikiwa ni kitala na nyota moja.

Mtitiriko huo wa kinembo kuanzia kwa IGP hadi kwa ACP, utafanana kimpangilio na ule wa kuanzia vyeo vya Jenerali, Luteni Jenerali na Meja Jenerali katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

Kwa upande wa makamishna wasaidizi waandamizi (SACP), kwa sasa watavaa nembo zenye ngao ya taifa na nyota tatu, kama wanavyovaa mabrigedia jenerali wa JWTZ.

Aidha, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi (ACP) ambaye awali alikuwa anavaa nembo ya mwenge tu, kwa sasa anavaa nembo yenye ngao ya taifa na nyota mbili, sawasawa na wanavyovaa makanali wa JWTZ.

Hata hivyo, juhudi za kumpata msemaji wa jeshi hilo, Essaka Mugassa, ili athibitishe hayo, hazikufanikiwa kwa maelezo kwamba yupo likizo.

Alipotafutwa kwa simu juzi, msaidizi wa msemaji huyo, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Juma Ally, alisema hawezi kuzungumzia hilo na badala yake alilitaka gazeti hili kufika kwa muhusika wa jambo hilo Kamishna Msaidizi wa Polisi, P.S. Saranga. Hata hivyo, ofisa huyo alipofuatwa ofisini kwake jana, hakuwepo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.