BARAZA la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, limetangaza kuwasimamisha masomo kwa muda usiojulikana, wanafunzi wote wa shahada za awali kufuatia mgomo waliouitisha kuishinikiza serikali iwaongezee fedha za mikopo.
Uamuzi huo unawaathiri maelfu ya wanafunzi katika kampasi za Mlimani, Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi na Usanifu Majengo (UCLAS), Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu Chang’ombe (DUCE), MUCE na Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC).
Tangazo la kusimamishwa kwa wanafunzi hao, lilitolewa jana mchana, na wanafunzi hao walitakiwa wawe wameshaondoka katika maeneo ya vyuo vyao ifikapo jana saa 12 jioni.
“Wanafunzi wote wanatakiwa wawe wameondoka katika maeneo ya chuo na katika mabweni ya chuo ifikapo saa 12 jioni,” ilisema sehemu ya taarifa iliyosambazwa jana na uongozi wa UDSM.
Taarifa hiyo ilionya kuwa, wanafunzi watakaoonekana katika mabweni baada ya saa 12:00 jioni jana, wangechukuliwa hatua kali.
Hata hivyo, uamuzi huo hauwahusu wanafunzi wa kigeni wa muda mfupi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uamuzi wa kuwasimamisha masomo wanafunzi hao, ulifikiwa katika kikao maalumu cha Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kilichofanyika jana.
Tangu juzi, mamia ya wanafunzi walianza mgomo wakilenga kuishinikiza serikali iwapatie asilimia 100 ya fedha za mkopo wa kugharamia masomo yao. Kwa mujibu wa utaratibu unaotumika hivi sasa, serikali inatoa asilimia 60 tu na asilimia 40 inayobaki, wanafunzi wanawajibika kujilipia wenyewe.
Akizungumzia uamuzi huo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema kuwa Baraza limelazimika kuchukua uamuzi huo kwa sababu wanafunzi hao wachcahe waliokuwa wamegoma, walikuwa wamesababisha kusimama kwa programu za chuo hicho.
“Waliogoma ni kama wanafunzi 400 au 500, lakini walikuwa wanawalazimisha na wengine wasiingie madarasani. Leo (jana) asubuhi wapo waliojaribu kuingia (madarasani), lakini walitolewa kwa nguvu,” alisema.
Profesa Mukandala alisema kuwa, mgomo huo uliwaathiri hata watu ambao hawahusiki, na kwamba wanafunzi waliokuwa wamegoma walikuwa wanatoa vitisho kwa wanafunzi ambao hawakutaka kujihusisha na mgomo, pia kwa walimu.
“Population (uwingi wa watu) katika jumuiya ya chuo kikuu sasa hivi ni zaidi ya watu 10,000, sasa tumeona hawa wachache wasiwasababishie usumbufu watu wengine wengi,” alifafanua.
Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO), Mtatiro Julius, alipinga amri hiyo.
Alisema hawawezi kuondoka bila kujua hatma ya wanafunzi waliowaweka madarakani.
“Hatua ya kufunga chuo haitoshi wala si suluhu ya matatizo, na kabla ya kuondoka, inatubidi tujue hatma ya madai yetu ya kuitaka serikali kugharimia asilimia 100 ya gharama za masomo kwa wanafunzi,” Julius alisema kwa msisitizo mbele ya umati wa wanafunzi waliokuwa wanamshangilia.
Julius aliwatia moyo wanafunzi hao kwa kuwaambia wasiondoke mpaka wapate maamuzi ya bunge la serikali ya wanafunzi ya vyuo hivyo.
“Nawaomba msiondoke mpaka mpate maamuzi ya mwisho kutoka bunge lenu, ambalo linakwenda kukaa muda huu (jana majira ya saa 10), nawaomba msiogope wala kutishika na amri ya kuondoka chuoni, kwani hakuna mwenye ubavu kuwaondoa kutoka eneo hili,” alisema kwa kujiamini.
Hata hivyo, wanafunzi wengi walitii amri ya baraza la chuo na Tanzania Daima ilishuhudia wanafunzi hao katika mabweni yaliyopo sehemu ya Mlimani, hosteli za Mabibo na Sinza, wakitoa vitu vyao nje na kutafuta usafiri wa kuwaondoa maeneo ya chuo.
Kutokana na uwingi wao, hali hiyo ilisababisha msongamano mkubwa wakati wanafunzi wakigombea magari kwa ajili ya kupakia mizigo yao.
Ulinzi uliimarishwa katika barabara zote huku askari wa chuo hicho wakishirikiana na polisi wa kawaida kufanya ukaguzi kwa kila gari linaloingia na kutoka sehemu ya Mlimani na hosteli ya Mabibo.
“Hebu tazama wanafunzi hawa walivyo na mabegi makubwa na vifaa vyao mbalimbali kama TV na kompyuta, wanavyotaabika kutokana na kufukuzwa katika hosteli, hii inasikitisha, inatia huruma, walio wengi hawana ndugu zao karibu wala hawana uwezo wa kuchukua usafiri binafsi, badala yake wametapakaa barabarani wakiomba msaada wa lifti huku wakiendelea kusubiri daladala,” alisema mpita njia mmoja.
Tanzania Daima ilishuhudia msongamano wa wanafunzi wakitoka na kuingia, huku wengine wakilaumu kitendo hicho na kujutia uamuzi wao ambao umewagharimu.
Wanafunzi mbalimbali wa mwaka wa kwanza na wa pili ambao walizungumza na Tanzania Daima, walionyesha masikitiko yao juu ya hatua ya uongozi wa chuo hicho dhidi yao na kuilaani serikali ya awamu ya nne kwa kupuuzia madai yao.
Akizungumza na gazeti hili baadaye, Julius alisema hali hiyo si matatizo kwao kwa kuwa wanatafuta haki yao ya msingi.
“Wao wameamua kufunga chuo, acha kifungwe, vijana warudi kwao, maana wao hawaelewi chochote, wanataka kauli ile ya rais itekelezwe,” alisema.
Kabla ya uamuzi huo wa kuwasimamisha masomo vijana hao, Profesa Mukandala aliwaambia waandishi wa habari kuwa, tatizo hilo la mgomo lilikuwa likifukuta kwa muda mrefu na walijaribu kulisuluhisha bila mafanikio.
Kwa mfano, alisema kuwa baada ya kuona kuwa wanafunzi wengi hawana uwezo, uongozi wa UDSM uliamua kusitisha mpango wa matibabu kwa wanafunzi, ambao kila mmoja alitakiwa ajigharamie sh 100,000.
Kuhusu suala la asilimia 40 ambayo wanafunzi hao wanataka ilipwe na serikali, Profesa Mukandala aliwalaumu wanafunzi hao kwa kukosa subira, kwani Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msolla aliwaahidi wanafunzi kuwa wavute subira hadi Agosti, wakati hilo linashughulikiwa.
Aidha, alibainisha kuwa chuo kilikuwa tayari kulishughulikia suala la mafunzo kwa vitendo, ambalo lilikuwa ni moja ya madai ya wanafunzi hao, wakitaka waongezewe fedha za mafunzo kwa vitendo.
“Haya yote tuliyotaka kuyafanya ni kwa sababu hatutaki kuvuruga utaratibu wa chuo. Kama wakigoma wanaporudi lazima waje na asilimia 40, fedha za matibabu na pesa ya mafunzo ya vitendo,” alisema Profesa Mukandala.
Alisema alipokuwa akizungumza na wanafunzi hao, alisisitiza kuwa mgomo huo ni gharama kubwa kwa chuo kwa sababu zinatumika karibu sh milioni 100 kwa siku wakati kazi hazifanyiki, walimu hawafundishi, mitambo haitumiki pamoja na kuharibu ratiba za chuo.