HADI sasa, Waziri wa fedha, Zakia Meghji, ameshindwa kutoa hadharani, jibu la barua aliyoandikiwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba. Katika barua hiyo, Profesa Lipumba alimtaka Meghji amfahamishe fedha za bajeti ya matumizi ya Ikulu zinawekwa katika fungu gani, kwani alikuwa (Meghji) amekanusha taarifa ya awali ya Profesa Lipumba kwamba fedha hizo zinakuwa katika fungu liitwalo Consolidated Fund.
Profesa Lipumba, mchumi kitaaluma, aliyasema hayo wakati akichambua matumizi ya serikali na moja kati ya mambo makubwa aliyobainisha ni matumizi makubwa serikalini. Profesa Lipumba alisema kuwa matumizi ya serikali, hasa hasa ya Ikulu, yalikuwa yamezidi kiwango cha fedha kilichokuwa kimetengwa kupitia bajeti.
Lakini wakati tunaendelea kulisubiri jibu la Meghji kwa Profesa Lipumba, mambo mawili yametokea. Kwanza, Benki Kuu ilitoa taarifa iliyoonyesha kiujumla kuwa matumizi ya serikali yameziki kiwango cha fedha zilizotengwa katika bejeti kwa mabilioni ya shilingi.
Wakati hayo yanatokea, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) naye akaibuka na ripoti yake iliyoonyesha ubadhirifu wa hali ya juu wa fedha za serikali. Ikumbukwe kuwa fedha hizi ni zile zilizomo kwenye bajeti iliyokwishapitishwa.
Ripoti hii inauhusu mwaka wa fedha 2005/06, lakini kilichomo ni marudio ya yaliyopata kutokea miaka yote iliyopita. Haitii wasiwasi kwamba hata sasa tunavyozungumza, hali ya matumizi ya fedha za serikali imebadilika sana. Imebadilika kwa sababu ubadhirifu huo ulitokea katika mwaka ambao serikali haikuzidisha matumizi yake. Sasa inaonekana wazi kuwa matumizi ya serikali yamezidi. Hii ina maana kuwa na ubadhirifu nao umezidi.
La sivyo, Rais Jakaya Kikwete asingelazimika kukatisha mapumziko yake katika visiwa vya karafuu na kuelekea Dodoma kuwaweka chini watendaji wake huku ajenda kuu ikiwa ni ripoti hiyo ya CAG.
Lazima kuna kitu amekigundua katika ripoti hiyo. Ndiyo, alionyesha wazi tangu mwanzoni kuwa kuendelea kuzikalia ripoti za CAG hakuleti maana ya ofisi hiyo kuwapo, na alitaka kuitumia fursa hiyo kuonyesha kuwa kweli halipendi jambo hilo.
Lakini hali hiyo ya ubadhirifu inapotokea wakati BoT imeshaeleza kuwa serikali imezidisha matumizi kwa mabilioni ya shilingi, na Rais anakuwa mkali namna hii, lazima watu wahisi kuwa kuna jambo.
Kama kiongozi mkuu, Rais Kikwete anapaswa kuwa mkali wa watendaji serikalini wanaotumia vibaya fedha ambazo ni jasho la walipakodi.
Kwa Watanzania wa kawaida, ripoti ya CAG inakatisha tamaa kwani kinachoonekana kwao ni kuwa wakati wanajifunga mikanda na kufanya kazi kwa bidii, wanajikamua na kulipa kodi ili kuijenga nchi yao kwa moyo wao wote, matunda ya mbegu wanayopanda yanaliwa na wenye ‘meno’ makali na ‘matumbo’ mapana.
Siku za nyuma, ripoti hizi za CAG zimewahi kuhojiwa, baadhi ya wabunge walishawahi kuuliza bungeni na jibu la haraka haraka lililowahi kutolewa ni kuwa ripoti inaonyesha mambo ya zamani, yaliyokwishahojiwa na kujibiwa, hivyo hayana maana tena.
Walidhani tumewaamini, kumbe watu waliamua kunyamaza kimya baada ya kuona kuwa wameamua ‘kufunika kombe mwanaharamu apite’, wakishindwa kujua kuwa ipo siku, hata kama ‘mwanaharamu hajapita’, atatokea mtu atakayethubutu kulifunua kombe. Na ‘mwanaharamu atakapopita’ wakati kombe lipo wazi ataona kilichomo ndani na kwa hakika atakitamani, ama kwa kutaka kukila au kutaka kujua kwa nini hicho kipo hivyo.
Rais Kikwete amejiingiza katika mkumbo wa kutaka ripoti za CAG zihojiwe, na walioorodheshwa kwa ubadhirifu wahojiwe pia ili maelezo ya kina yapatikane kuhusiana na matumizi hayo yanayotia kizunguzungu.
Sijui kama na yeye ataambiwa kuwa hiyo ni ripoti ya mambo yaliyotokea zamani - yalikwishahojiwa. Kama mkimwambia hivyo sawa, lakini niwaombe jambo moja, kama mambo hayo yalishahojiwa na kujibiwa, basi tupatieni hayo majina na sisi akina pangupakavu ili tuyafahamu, tusije tukaendelea kuwalaumu siku zote kumbe wala hamna hatia.
Jambo la mwisho kwa Rais Kikwete. Ni vizuri umetaka wizara, idara, taasisi na vitengi vilivyoonyeshwa katika ripoti kuwa vimetumia vibaya fedha za serikali, ni vema uhakikishe kuwa ofisi yako nayo, yaani Ikulu, inakaa na kujadili na ikishamaliza kufanya hiyo, itupatie majibu kuhusiana na tuhuma hizi za kuzidisha matumizi ya fedha za bajeti.
pnyanje@yahoo.com