Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kabwe amtumia Kikwete, Warioba kuibana serikali
Kabwe amtumia Kikwete, Warioba kuibana serikali
By Habari Tanzania | Published  04/17/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Mwandishi Wetu


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), jana alimlazimisha Waziri Mkuu, Edward Lowassa kusimama na kuliahidi Bunge kuwa, serikali itawasilisha muswada wa mabadiliko ya sheria ya uchaguzi itakayozungumzia pamoja na mambo mengine masuala yanayohusu matumizi ya fedha wakazi wa uchaguzi.

Lowassa alilazimika kusimama na kutoa ahadi hiyo baada ya Kabwe kuibana serikali na kutaka ifanye marekebisho kwa kuingiza katika muswada wa sheria ya rushwa, masuala yanayohusu rushwa wakati wa uchaguzi.

Kabwe katika hoja yake, alirejea hotuba ya Rais Jakaya Kikwete na akanukuu Ripoti ya Tume ya Jaji Joseph Warioba ambazo zote kwa nyakati tofauti zilikuwa zikionyesha kuwa, rushwa lilikuwa ni tatizo katika uchaguzi.

Akinukuu hotuba ya Kikwete, Kabwe alisema kuwa ipo hatari, nchi ikawekwa rehani iwapo hali hiyo itaachwa iendelee kama ilivyo sasa.

Hoja hiyo ya Kabwe ilizusha mjadala, pale alipotaka kiongezwe kifungu katika sheria kitakachozungumzia rushwa katika siasa katika muswada wa rushwa ambao ulikuwa ukijadiliwa.

Kutokana na hoja hiyo ya Kabwe, Lowassa alilazimika kulieleza Bunge kuwa, serikali itaandaa na kuwasilisha muswada wa sheria mpya ya uchaguzi ambayo itazingatia masuala ya matumizi ya fedha katika kampeni na rushwa katika uchaguzi.

Lowassa alisema nia ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali, ni kuhakikisha kuwa, muswada wa sheria hiyo unawasilishwa bungeni kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Licha ya kuwashukuru wabunge, hasa wa kambi ya upinzani kwa kujipanga vizuri kuujadili muswada wa rushwa, Lowassa aliwataka waelewe kuwa ni Rais Kikwete ndiye aliyetoa kauli kuhusu suala hilo.

“Sasa wanaposema serikali haina commitment, ni commitment gani wanayoizungumzia kupita kauli thabiti kama hii?” alihoji Lowassa.

Hata hivyo, baada ya mjadala mzito, Bunge jana jioni lilipitisha muswada wa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa wa mwaka 2007 uliosomwa kwa mara ya pili na ya tatu na kuwasilishwa bungeni mwishoni mwa wiki, ukiwa na marekebisho kadhaa.

Licha ya michango ya wabunge wakati wanachangia, mjadala mwingine uliibuka wakati Bunge lilipokaa kama kamati, kujadili muswada huo kifungu kwa kifungu.

Walioongoza hoja hizo ni wabunge wa kambi ya upinzani, hasa wale wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambao mara kwa mara walisimama wakitoa hoja na kutetea hoja zao, ingawa nyingi zilikataliwa.

Katika mjadala wa jumla, awali, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM), aliishauri serikali kuwatumia wataalamu wa vyuo vikuu vilivyopo nchini, katika kupitia mikataba ambayo inadhaniwa kuwa ni mibovu, ambayo inaonekana kuwa ilisainiwa chini ya mazingira ya rushwa.

“Wataalamu wa vyuo vikuu wanao uwezo mkubwa wa kuchangia mawazo katika kupitia mikataba, ambao wataifanya mikataba husika iwe na manufaa kwa Watanzania wote,” alisema.

Katika mchango wake, Zambi alisema Watanzania wengi wanaamini kuwa, wanaosaini mikataba wanakula rushwa kutokana na mikataba hiyo kuonekana kuwa haijali maslahi ya nchi.

Alisema kuwepo kwa asilimia 10 katika mikataba, ni chanzo pia cha kuwapo kwa mikataba mibovu na yenye madhara kwa jamii, hivyo wote wanaohusika kusaini mikataba hiyo wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.

Alibainisha kuwa, wala rushwa wakubwa wanafahamika, lakini tatizo limekuwa hakuna mtu mwenye kuthubutu kumfunga paka kengele.

Zambi alitaka kutokuwapo kwa ubaguzi wa kusema kuwa rushwa nyingine ni ndogo na nyingine kubwa, bali rushwa ipimwe kutokana na umuhimu wa huduma inayotolewa rushwa husika.

“Kwa mfano, mtu anakwenda hospitali akiwa na mgonjwa, anaombwa rushwa ya sh 5,000, anakuwa hana, mgonjwa wake anakosa huduma na kupoteza maisha. Rushwa hiyo ni kubwa sana na haiwezi kufananishwa na ofisa aridhi anayeomba laki tano ili atoe kiwanja,” alisema.

Alisema kuwa rushwa ya ngono bado ni tatizo kubwa linalosababisha kuendelea kuwepo kwa watendaji wabovu serikalini na katika taasisi mbalimbali, kwani wengine wanapatiwa kazi kwa kutoa ngono wakati hawana sifa zinazostahili.

Zambi pia ameitaka serikali kuwawajibisha wafanyakazi wa mahakama wanaohusika katika upotevu wa mafaili ya kesi za wananchi, kwani huenda wanapewa rushwa ili kusaidia upotevu huo.

Akichangia muswada huo, Mbunge wa Muleba Kaskazini, Ruth Msafiri (CCM), aliishauri serikali kuwaaibisha wala rushwa wanapobainika kama wao wanavyolidhalilisha taifa.

Alisema mbali na adhabu nyingine wanazopatiwa wala rushwa, pia wanastahili kuchapwa viboko ili waaibike na iwe fundisho kwa wala rushwa wengine maana wanapotozwa faini, hutoa sehemu ya fedha hizo walizochukua kupitia rushwa.

Alisema adhabu nyingine inayostahili kwa watoaji na wapokea rushwa, ni kufukuzwa kazi, kunyang’anywa leseni za biashara.

Wabunge wengine waliochangia muswada huo, walishauri Mwendesha Mashitaka (DPP) asihusishwe katika kesi za rushwa kama ilivyo kwa kesi za Mamlaka ya Mapato (TRA).


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.