ENEO la ufukwe wa Bahari ya Hindi, kisiwani Mafia, limevamiwa na raia wa kigeni wanaodaiwa kupora mazao ya baharini na kuharibu mazingira kwa kiwango kikubwa.
ENEO la ufukwe wa Bahari ya Hindi, kisiwani Mafia, limevamiwa na raia wa kigeni wanaodaiwa kupora mazao ya baharini na kuharibu mazingira kwa kiwango kikubwa.
Eneo lililovamiwa liko katika Kijiji cha Jimbo, Kata ya Kilongwe, Tarafa ya Kaskazini katika Wilaya ya Mafia.
Habari zilizoifikia Tanzania Daima, kutoka Taasisi ya Utafiti wa Viumbe vya Majini (TAFIRI), zinaeleza kuwa wavamizi hao wamekata miti mingi aina ya mikoko kwa ajili ya kuchimba mabwawa ya kufugia samaki aina ya kamba, kinyume cha sheria za nchi.
Watafiti wa taasisi hiyo wameeleza kuwa, shughuli za ufugaji zinazofanywa na wageni hao, zinasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira ya baharini kwa sababu zinafanywa kienyeji, jambo linalohatarisha uhai wa baadhi ya viumbe vya baharini katika eneo hilo.
Wakizungumza kwa sharti la majina yao kutotajwa gazetini kwa sababu ya usalama wa kazi zao, walisema uchunguzi wao umebaini kuwa, wageni hao waliidanganya serikali kuwa, wanahitaji eneo dogo, katika pwani hiyo ya baharini kwa ajili ya kuanzisha mradi wa kufuga kamba.
Walisema hawakubaini katika uchunguzi wao iwapo serikali ilitoa eneo lililoombwa kwa wageni hao au la, lakini walibaini kuwa Mbunge wa Mafia, Abdulkarim Shah, ndiye aliyeshinikiza kutolewa kwa eneo hilo.
Walisema tayari wageni hao wamekwishachimba mabwawa 16 kwa ajili ya kufugia samaki aina ya kamba, na sasa wanakata miti aina ya mikoko, ambayo inalindwa na sheria kutokatwa, kwa ajili ya kupanua eneo lao la mradi wa ufugaji.
Taarifa zaidi ya watafiti hao, inaeleza kuwa, wageni hao tayari wamekwishaanzisha miradi mingine kadhaa katika eneo hilo la ukanda wa pwani, ikiwemo ya kutotolesha vifaranga vya kamba na wamejenga kiwanda cha kusindika kamba.
Walisema kuanzishwa kwa miradi hiyo kumewatia shaka, kuwa kuna uwezekano wa kuwepo uvuvi mkubwa wa samaki aina ya kamba kutoka baharini, ambao husindikwa katika kiwanda hicho kisha kusafirishwa kwenda kuuzwa nje ya nchi bila serikali kujua wala Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoza ushuru kama inavyotakiwa.
“Tumechunguza na kubaini kuwa, wageni hawa wanatotolesha vifaranga, wana shamba la kufugia na wana kiwanda cha kusindika samaki aina ya kamba. Serikali haina habari kama kamba wanavuliwa kwa wingi baharini, wanasindikwa na kusafirishwa kwenda kuuzwa nje, na TRA wanakosa pesa nyingi tu kwa biashara hii,” alisema mmoja wa watafiti hao.
Habari zaidi zimedai kuwa, katika kipindi cha miezi mitatu ya mwishoni mwa mwaka jana, wageni hao walivuna tani 43 za kamba na kwenda kuziuza nje ya nchi, lakini haifahamiki kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ililipwa kodi ya biashara hiyo ya mazao ya baharini.
Aidha, habari zinadai zaidi kuwa, mradi huo wa ufugaji kamba, unachangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira ya bahari kwa vile maji machafu na yenye kemikali yanayotokana na ufugaji huo, hutitirishwa moja kwa moja baharini, jambo ambalo haliruhusiwi kwa mujibu wa taratibu za ufugaji.
Alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu taarifa ya watafiti hao, Shah alidai kushangazwa nayo kwa sababu serikali imebariki shughuli zinazofanywa na wageni hao.
Alisema wageni hao wanamiliki kampuni inayoitwa Alpha Klust, na kwamba waliingia nchini mwaka 1998 wakiwa na meli iliyokuwa ikielea baharini.
“Hawa si wageni tu, ni wawekezaji, waliingia nchini mwaka 1998 wakiwa na meli iliyokuwa ikielea baharini na baadaye nilikuja gundua walikuwa wakijishughulisha na mambo ya uvuvi.
“Nilipochaguliwa kuwa mbunge, tuliwashawishi waje nchi kavu, wakakubali, wanafuga, wamejenga kiwanda cha kusindika kamba eneo la Kilindoni na wameajiri watu wetu wengi.
“Ninachojua mimi, wananunua samaki aina ya pweza na ngisi kwa ajili ya biashara zao, lakini kamba ndio kwanza ninasikia kutoka kwako, kwa sababu kwanza hawapatikani hapa, wanapatikana Rufiji,” alisema mbunge huyo.
Alisisitiza kuwa, kabla kiwanda hicho ambacho hakueleza kunasindika samaki wa aina gani hakijajengwa, aliwasaidia wawekezaji kupata vibali vyote vinavyohusika kwa ajili ya kufanya shughuli zao hapa nchini na kwamba hata uvuvi wanaoufanya, una baraka za serikali.
Akizungumzia mradi wa ufugaji samaki aina ya kamba, Shah alisema ulianzishwa mwaka 2001 na kwamba serikali ilitoa eneo la jangwa (ambalo halikuwa na mmea wowote) kwa kampuni hiyo kwa ajili ya kuchimba mabwawa ya kufugia kamba.
“Wanafuga kwa ruhusa ya serikali, maliasili waliruhusu, watu wa mazingira waliruhusu na wataalamu wa chuo kikuu pia walihusika kutoa ruhusa hiyo, sasa hawa wataalamu wa TAFIRI wametokea wapi?” alieleza na kuhoji Shah.
Alipoulizwa kuhusu kukatwa kwa miti ya mikoko, alisema jambo hilo ni geni kwake na atalifuatilia baada ya kikao cha Bunge kwa sababu miti hiyo hairuhusiwi kukatwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Hata hivyo, alilieleza gazeti hili kuzungumza na mmoja wa maofisa wa kampuni hiyo aliyemtaja kwa jina la Joshua Meshack, kuwa ndiye mwenye mamlaka ya kutoa tamko kwa niaba kampuni hiyo.
Alipotafutwa kwa njia ya simu, Meshack, kwanza alihoji ni kipi kilichokuwa kikitakiwa kuandikwa na gazeti hili, na alipoelezwa, aliomba muda wa kufuatilia madai hayo na kuahidi kupiga simu katika ofisi za gazeti baada ya saa moja kwa ajili ya kutoa ufanunuzi.
Baada ya muda huo kupita, Tanzania Daima ilimpigia tena Meshack na alipopatikana, alisema kwamba bado anajadiliana na wakurugenzi wa kampuni na aliomba habari hiyo isiandikwe mpaka hapo atakapowasiliana na gazeti hili.
Katika hatua ya kushangaza, Meshack hakupiga simu kama alivyoahidi na alipotafutwa siku zilizofuata, kila mara simu yake ilikuwa inaita na kisha kukatika.
Juzi jioni, simu ya Meshack ilikuwa ikiita bila majibu na baadaye ikawa haipatikani kabisa.
Habari zaidi zilizopatikana kutoka TAFIRI jana, zilieleza kuwa, serikali ya awamu ya pili iliwahi kuingia katika mgogoro mkubwa na wataalamu wa hapa nchini na nje baada ya kulitoa eneo hilo kwa mwekezaji aliyetajwa kwa jina la John Normann.
Ilielezwa kuwa, kwa mara ya kwanza, mwanzoni mwa miaka ya 90, Normann aliomba eneo hilo kwa serikali kwa ajili ya kuanzisha mradi wa kufuga kamba na serikali iliridhia ombi hilo.
Uamuzi huo wa serikali ulipingwa na wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakiongozwa na Marehemu Profesa Seith Chachage na wataalamu wengine wa mazingira wa mashirika ya kimataifa.
Pingamizi hilo la wasomi na wataalamu wa mambo ya mazingira, lilikubaliwa na Benki ya Dunia ambayo ilisitisha uamuzi wake wa awali wa kutoa fedha kwa Normann kwa ajili ya kufadhili mradi.
Jitihada za gazeti hili kuwasiliana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe kuzungumzia suala hilo, ziligonga mwamba baada ya simu yake ya kiganjani kutopatikana kwa muda mrefu.